Home Uncategorized HATMA YA OKWI, JUUKO YATOLEWA SIMBA

HATMA YA OKWI, JUUKO YATOLEWA SIMBA


WAKATI kukiwa na taarifa za nyota wengi wa Simba akiwemo Juuko Murshid na Emmanuel Okwi kutokuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao, Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Crescentius Magori, amefungukia juu ya hatima ya nyota hao na wengineo.

Juuko na Okwi ambao mikataba yao imemalizika, kuna uwezekano wasiwepo tena kikosini hapo kutokana na Kocha Patrick Aussems kunukuliwa akitaka Juuko aachwe, huku Okwi akipata dili nchini Afrika Kusini. Akizungumzia hatima ya nyota hao na wengine akiwemo Haruna Niyonzima, Magori alisema:

“Unajua hili suala la mikataba ya wachezaji ni siri ya mwajiri na mwajiriwa unatakiwa kulitambulia hilo.

“Ishu ya nani tutaachana naye na nani tutamuongezea mkataba lipo juu yetu na ndani ya wiki hii kila kitu tutakiweka wazi kwa sababu usajili wa wachezaji wa ndani unakwenda hadi mwisho wa mwezi ujao na ule wa kimataifa mwisho Septemba.

“Hivi sasa tunafanya mazungumzo na wachezaji ambao mikataba yao imemalizika, tutakaomalizana nao tutawaweka wazi na wale tutakaoshindwana nao pia watafahamika.”

Mbali na Juuko, Okwi na Niyonzima, nyota wengine ambao mikataba yao inamalizika ni Asante Kwasi, Nicholas Gyan. Simba mpaka sasa imesajili wachezaji wawili wapya wa kimataifa ambao ni Wilker Henrique, Gerson Fraga Vieira raia wa Brazil pamoja na Msudani Sharaf Eldin.

Wazawa ni Beno Kakolanya, Kennedy Juma na Miraji Athuman. Hata hivyo, Simba katika wachezaji wake wa zamani wa kimataifa ambaye ameongezewa mkataba mpaka sasa ni Meddie Kagere. Upande wa wazawa ni Bocco, Tshabalala, Mkude, Erasto na Manula.

Wachezaji wa kimataifa wa Simba waliokuwa wakiitumikia timu hiyo msimu uliopita ni Claytous Chama, Pascal Wawa, Haruna Niyonzima, Juuko Murshid, Asante Kwasi, Nicholus Gyan, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, James Kotei (ameondoka) na Zana Coulibaliy.

SOMA NA HII  TFF WAFUNGUKA MENGINE ISHU YA TIMU KUGOMA KUINGIA VYUMBANI - VIDEO