Home Uncategorized KWA USHINDANI ULIOPO KWA SASA KILA TIMU ISAJILI KIUFUNDI NA SIO BORA...

KWA USHINDANI ULIOPO KWA SASA KILA TIMU ISAJILI KIUFUNDI NA SIO BORA LIENDE

KATIKA vitu ambavyo viliziangusha timu nyingi zilizoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2018/19 ambao ulimalizika hivi karibuni, ni suala zima la usajili.

Usajili huo ni ule wa dirisha kubwa ambao ulifanyika kabla ya kuanza kwa msimu pamoja na dirisha dogo ambapo una kawaida ya kufanyika mwishoni mwa mwaka.

Timu nyingi zinapomaliza msimu, basi zimekuwa na kawaida ya kufanya usajili wa wachezaji wengi kama vile ndiyo zinaunda timu mpya. Hali hiyo si nzuri katika kujenga timu imara.

Inashauriwa kama unataka kuwa na timu imara na yenye ushindani zaidi, ni lazima uwe na wachezaji wengi waliokaa pamoja na kufahamu mifumo ya timu.

Naweza kutolea mfano kwa timu kama ya Simba ambayo imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 ikiwa ni mara ya pili mfululizo.

Licha ya msimu wake wa nyuma kufanya vizuri, lakini haikuingia kwenye mkumbo wa kusajili wachezaji wengi. Hilo limewasaidia sana.

Simba walifanya usajili katika sehemu chache sana na wachezaji waliochukuliwa ni wale kweli waliokuwa wakihitajika kwa wakati huo. Mwisho wa siku matunda mazuri yameonekana.

Mbali na kuwa na kocha mpya, lakini Simba iliweza kufanya vizuri kutokana na wale wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi cha kwanza, wengi walikuwa pamoja kwa msimu wa nyuma yake. Wakawa wanafahamiana vizuri aina zao za uchezaji.

Hivi sasa nimesikia tena kwamba wana mpango wa kukiboresha kidogo kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao ili wafanye tena vizuri zaidi ya ilivyokuwa msimu huu.

Ukiachana na Simba, kuna timu nimesikia zimeanza usajili wa fujo, zinaonekana kusajili wachezaji wengi wapya ambao kiukweli itachukua muda mrefu kuzoeana na wale waliopo, hapo ndipo shida inapoibuka.

Siku zote timu yenye wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza waliokaa pamoja kwa muda mrefu, huwezi kuifananisha na ile ambayo ina wachezaji wengi wapya wa kikosi cha kwanza ambao kuzoeana kwao inahitaji kupewa muda zaidi.

Timu zetu nyingi zinafeli hapo, zinapofanya usajili, licha ya kufuata ripoti ya mwalimu, lakini wakati mwingine viongozi wanaongeza wachezaji wao kwa mapenzi yao wenyewe, mwisho wa siku timu inakuwa na lundo la wachezaji wasiokuwa na umuhimu.

Hapo utakuta kiongozi analazimisha mchezaji wake aliyemsajili lazima acheze wakati kocha hakuwa na mipango naye. Mvutano unaanza kuibuka.

Usajili huo ni wa kizamani tena ni wa kisiasa na haupaswi kufumbiwa macho, lazima tuukemee kwa lengo la kulitetea soka letu liweze kufika mbali na si kudidimia siku hadi siku.

Kama tukiwa tunaishi kwenye dunia ya sasa ambayo inahitaji zaidi mabadiliko kisha sisi akili zetu zimebaki nyuma zikifikiria zama zile za analojia, tutakuwa tunafeli kila siku halafu tunaanza kumtafuta mchawi anayerudisha nyuma maendeleo ya soka letu.

Jamani tuache siasa katika suala hili nyeti katika timu. Unapokosea kusajili kipindi hiki, sahau kufanya vizuri katika michuano utakayoshiriki.

Huwezi kuwa na timu bora wakati una wachezaji wasiokuwa bora. Lazima uwe na wachezaji bora ambao ndiyo wataunda timu bora.

Inafahamika kwamba dirisha rasmi la usajili halijafunguliwa, lakini kwa hivi sasa timu zinaruhusiwa kufanya mazungumzo na wachezaji wanaowataka lakini ni wale ambao Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeruhusu.

Wachezaji hao ni wale waliomaliza mikataba yao au katika mikataba yao, imebaki miezi sita kabla ya kumalizika.

SOMA NA HII  MSERBIA WA YANGA ATIMKA BONGO