Home Uncategorized SIMBA, WALTER BWALYA MAMBO SAFI

SIMBA, WALTER BWALYA MAMBO SAFI


STRAIKA namba moja wa Nkana ya Zambia, Walter Bwalya ameweka wazi kwamba amepokea ofa ya Simba na Sportif Sfaxien ya Tunisia.

Mchezaji huyo mwenye asili ya DR Congo amesema kwamba bado wako kwenye majadiliano ambayo yanakwenda vizuri na huenda wakakamilishana muda wowote.

Mchezaji huyo ambaye ni mara ya kwanza kuitaja Simba kwenye mahojiano yake, amesema kwamba viongozi wa Wekundu hao wamemuonyesha ofa ambayo inamshawishi kama ilivyo pia kwa Sfaxien na klabu nyingine za Afrika Kaskazini.

Straika huyo ambaye anacheza timu moja na beki wa zamani wa Simba na Yanga, Hassan Kessy alisema; “Simba wamenipa ofa yao na majadiliano yanaendelea vizuri.”

Lakini habari za uhakika ambazo Spoti Xtra imezipata ni kwamba Simba itamlipa mshahara wa Sh.Mil 9 kila mwezi na dau lake la uhamisho ni nono kwelikweli. Mkataba wa Bwalya na Nkana unamalizika Julai 2021 lakini una kipengele kwamba akipata timu muda wowote anaweza kuondoka.

Simba mpaka sasa imeshamalizana na Francis Kahata wa Gor Mahia ya Kenya huku Mohammed Dewji ‘Mo’ ambaye ni mdhamini wao akitangaza kufanya usajili wa mshtuko msimu huu.

Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems amesisitiza kwamba atasajili wachezaji watano wa kigeni ambao moja ya sifa yao ni kwamba walishacheza kuanzia hatua ya robo fainali ya mashindano ya Afrika. Simba na Yanga zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu

SOMA NA HII  BREAKING: MZEE KILOMONI AKAMATWA WAKATI AKIFANYA MKUTANO NA WAANDISHI WA HABARI