Home Uncategorized TUZIJADILI HOJA ZA ROSTAM MSITARI KWA MSTARI, MIHEMKO KATIKA HILI SI JIBU...

TUZIJADILI HOJA ZA ROSTAM MSITARI KWA MSTARI, MIHEMKO KATIKA HILI SI JIBU SAHIHI

Na Saleh Ally
NILIFIKA nyumbani kwa mwanasiasa maarufu Rostam Aziz baada ya kualikwa kama mkongwe wa masuala ya habari za michezo nchini.
Nilifika pale kwa lengo la kusikiliza kilichokuwa kikizungumzwa na hasa baada ya kuthibitishiwa, suala litakalozungumziwa litakuwa ni la michezo.
Michezo ndiyo maisha yangu ya kila siku. Nilitaka kujua Rostam anazungumzia nini. Wakati nikiwa njiani, niliwaza sana, nikajiaminisha naye alikuwa amepanga kujipambanua kwamba anataka asilimia kadhaa ndani ya Yanga ili kuamsha ushindani kati yake na watani wao Simba ambao tayari wana mwekezaji, Mohamed Dewji maarufu kama Mo Dewji.
Napenda kuwe na ushindani ili michezo ikue. Ile tabia au hisia za kizamani za leo Simba tajiri Yanga masikini au kesho Yanga tajiri na Simba masikini yamepitwa na wakati. Kikubwa ni klabu zote kuwa na fedha, zinazojitambua na ushindani uwe wa kiwango cha juu.
Wakati matarajio yangu yalikuwa ni kumsikia Rostam naye akitia mguu wake Jangwani na kutangaza kutaka uwekezaji, akazungumza mambo tofauti kabisa ambayo kidogo yamewashangaza wengi. 
Rostam alieleza akisisitiza ni “Msimamo” wake, kwamba haamini katika klabu kongwe kama Yanga kumilikiwa na mtu mmoja. Anapinga suala la umiliki kwa mtu mmoja akisisitiza wanachama wanapaswa kuwa na nguvu na klabu yao.
Halafu akasisitiza, kuwa pia anapinga suala la ufadhili ambalo ni njia ya mzunguko ya umiliki. Badala yake yeye anaamini sana suala la udhamini kwa kuwa klabu inapaswa kuwa na njia sahihi za udhamini ambayo itakwenda kwa mikataba kwa maana mdhamini atajitangaza na klabu itaingiza fedha.
Moja ya maswali niliyomuuliza ni kwamba, vipi sasa haidhamini Yanga kwa kuwa yeye ni shabiki tokea darasa la kwanza na sasa ni tajiri na ana makampuni? Jibu alisema analifikiria hilo.
Swali jingine nililomuuliza, nilimueleza kuwa anaamini katika michango ya harambee ambayo haiwezi kuwa na uhakika na uendeshaji wa klabu? Jibu alilotoa ni hapana, kwamba lazima kuwe na mpangilio mzuri wa kuingiza mapato kupitia wadhamini, haki za runinga, viingilio vya uwanjani lakini pia uuzaji wa bidhaa za Yanga kama jezi na kadhalika.
Mwisho nikamkumbusha, kwamba nimeripoti michezo na hasa soka kwa miaka 22 sasa. Najua kuna upungufu mkubwa wa viongozi sahihi kwa maana ya ujuzi kama ilivyo kwa nchi zilizoendelea. Anaweza kusaidia hilo.
Rostam akajibu kuwa ana uwezo wa kufanya mawasiliano na uongozi wa Yanga ulio madarakani na kuwasaidia kwenda nje au kuwaita wataalamu kutoka nje kuja nchini kuwapa mafunzo, fedha zinapoingia Yanga kunakuwa na utaratibu mzuri wa kitaalamu unaoendeshwa na wataalamu.
Naeleza haya kwa kuwa nilikuwa pale, kwamba inawezekana kabisa Rostam akawa na nia tofauti na alichosema, lakini inawezekana tukapitia hoja kwa hoja kujadili hili na kulifanya liwe na afya kwa ajili ya mpira wa nchi yetu.
Asikudanganye mtu, wewe kama ni Yanga hautakwenda Simba, ukiwa Simba, Yanga wanaendelea kuwa sehemu ya maisha yako hasa linapofikia suala la mpira. Ushindani wa timu hizi mbili unatengeneza kukua au muendelezo wa klabu hizi mbili ambazo zilikuwa “damu” moja kabla ya kutengana.
Mazungumzo ya Rostam zaidi yamejumlishwa na suala la uwekezaji wa Simba. Wako ambao wamemlaumu na hata wale waliozungumza maneno mabaya ambayo hayaandikiki. Mawazo yangu maneno hayo, hayakuwa na kipimo tosha cha ujadili wa hoja alizozitoa na badala yake, yakawa ni jazba na mihemko.
Kunapokuwa na mihemko, hakuna nafasi ya kujadili hoja. Pia hakuna sababu ya kumzuia, kumsema kwa maneno makali mtu anayesema “kwa mtazamo wangu”. Bahati nzuri anayesema hivyo ni yule ambaye ni mfanyabiashara mkubwa na suala “Uwekezaji” si geni kwake kwa kuwa amewekeza sehemu nyingi sana.
Badala ya kuliangalia kwa jicho hasi na kujawa hasira, tunaweza kuangalia kwa jicho chanya kujenga hoja za msingi.
Mimi kabla ya kumkosoa naangalia faida ya mazungumzo yake. Naanza kwa kusema, klabu yenye watu wengi ndiyo mvuto wa wawekezaji, na wawekezaji wanaweza kuingia na kufanya uwekezaji.
Kikubwa kiangaliwe wakati wa mchakato, kusiwe na ujanja ujanja ambao utamfaidisha mwekezaji ambaye huenda anaweza kuwa na hisa chache kuliko hata wanachama.
Wanachama wanaweza kuwa na hisa nyingi lakini wakawa na mgawanyiko kwa kuwa wao si mtu mmoja. Hivyo katiba lazima iwe makini sana kuhakikisha faida ni ya wana klabu na si mwana klabu.
Kwa ile ya Rostam kwamba anaona klabu haiwezi kumilikiwa na mtu mmoja. Kuna jambo ambalo nimeona tunaweza kujifunza. Tukubali kwamba ndani ya klabu hizi kubwa kumekuwa hakuna mfumo mzuri wa uendeshaji.
Mfano leo Yanga wamechangiwa mamilioni, kama uendeshaji hauna kiwango cha juu cha kitalaamu kwa maana ya matumizi bora ya fedha, matumizi muhimu na ya lazima lakini si ili mradi na pia kuwa na watu wenye nia ya maendeleo na ujuzi wa kuyapata, basi itakuwa ni kazi bure.
Kwani mwekezaji anajiunga na klabu kwa sababu ipi. Lazima ameona faida, ameona fursa lakini kuna upungufu ambao yeye kwa kuutumia utaalamu na uzoefu wake, ana nafasi ya kubadilisha mambo yakaenda vizuri na fedha zikaingia kwa wingi.
Sasa kama klabu, bila ya kuwa na mwekezaji halafu waliopo madarakani wakawa na utaalamu wa kufanya mambo kwa ufasaha.
Pamoja na hivyo, wakaajiriwa watu sahihi ikiwezekana hata wale kutoka nje ili kuifanya klabu ijiendeshe kitaalamu zaidi kama ambavyo angeingia mwekezaji na kuisaidia kwa kuajiri wataalamu na kuyapeleka mambo kitaalamu au kiweledi. Saa hapo tatizo ni lipi kama klabu isipokaribisha mwekezaji?
Nani anatambua hadi sasa uwezo wa Yanga kuingiza fedha kwa mwezi, kwa mwaka ni kiasi gani? Hasa kama itakuwa katika mfumo sahihi kabisa.
Sote hatujui, basi kama ni hivyo tunaweza kukubaliana na Rostam kwa muda, Yanga ipite katika utaratibu sahihi, tuone inaweza kujiendesha namna gani na baada ya hapo upungufu uangaliwe na wakati anakaribishwa mdhamini huenda akaingia akijua hasa thamani na ukubwa wa Yanga.
Simba kuwekeza sawa, lakini pia inawezekana Yanga wakapata thamani ya juu kama watajipanga vizuri kwa maana ya kujiendesha kitaalamu.
Mawazo ya Rostam tusiyachukulie kishabiki sana, tuyape nafasi na baada ya hapo tuangalie faida yake, wapi pa kuwekeza na ikiwezekana kama litakuja suala la mwekezaji, kuna uwezekano wa kuangalie uwe wa namna gani.
Kwa wale waliopata nafasi ya kusikiliza mazungumzo yote ya Rostam alisema anapinga klabu kuwa inachangisha watu kupitia harambee. Maana yake anaungana na wengi wanaotaka klabu zijiendeshe kitaalamu na kupata faida. Sasa tatizo liko wapi?
Niwakumbushe, watu wote hawawezi kuwa na mawazo yanayofanana. Ndiyo maana unaona klabu za Ujerumani ni tajiri, uendeshaji wake unapishana kabisa na zile za England ambazo nazo pia ni tajiri. Lakini za England, zinapishana kabisa na zile za Hispania ambazo nazo ni tajiri sana.
Kwa mifumo tofauti, klabu hizi zinaweza kujiendesha na mifumo yote imetengeneza matajiri. Hii maana yake ni hivi, kwamba si lazima kutumia mfumo mmoja au unaofanana ili wote kufikia mafanikio.
Tutumie muda mwingi kujifunza, kukubali maoni na kuyafanyia kazi badala ya kuwa mashabiki tunaopinga na porojo si kwa hoja, badala yake ni kutukana tu au kusema maneno yanayotuonyesha sisi ni watu tusio na lolote linalokwenda kwenye mlango sahihi wa ujenzi wa mafanikio zaidi ya mihemko. 
SOMA NA HII  SIMBA YAMPA MILIONI 173 MORRISON, PANGA LAPITA YANGA, NDANI YA CHAMPIONI JUMATATU

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here