Home Uncategorized UTATU MTAKATIFU SIMBA WAKOMBA MILIONI 300

UTATU MTAKATIFU SIMBA WAKOMBA MILIONI 300


Utatu hatari Simba, kipa Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe wametikisa kiberiti kwa kugoma kusaini mikataba mipya wakitaka wapewe mkwanja mrefu zaidi.

Wachezaji hao walijiunga na Simba misimu miwili iliyopita wakitokea Azam FC na sasa mikataba yao imemalizika hivyo wapo kwenye mazungumzo ya kuongeza mingine.

Simba chini ya mwekezaji wao bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ imetangaza kufuru ya usajili kwa kuhakikisha inawasajili wachezaji wowote itakayohitaji kuwasajili kwa dau lolote la usajili.

Mo alisisitiza juzi Jijini Dar es Salaam kwamba hawatamuachia mchezaji yoyote mzawa mzuri aondoke Simba.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, uongozi wa timu hiyo hivi karibuni ulishindwa kufikia muafaka na wachezaji hao katika dau la usajili ambalo kila mmoja alikuwa akihitaji Sh mil 100.

Habari zinasema uongozi wa Simba wenyewe uliweka dau la Sh mil 80 kwa kila mmoja lakini kwa nyakati tofauti walikataa na kuomba waongezewe Sh mil 20 ili zifikie 100.

Aliongeza kuwa, uongozi huo upo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa wachezaji hao watatu kwa dau la milioni 300 baada ya kumsainisha nahodha wa timu hiyo, John Bocco.

“Wachezaji watatu ambao ni Manula, Nyoni na Kapombe tayari wamekubaliana baada ya kufikia muafaka mzuri wa kuwaongezea mkataba kwa kila mmoja kumpatia Shilingi Milioni 100.

“Hivyo, itatumika Shilingi Milioni 300 katika usajili wao wa wachezaji hao watatu na kikubwa wanachosubiria ni kuwapatia fedha hizi kabla ya kusaini mkataba,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa katibu wa timu hiyo, Anold Kashembe kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Uongozi upo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji ambao amependekeza kuwaongezea mikataba kwa wale ambao imemalizika.

“Na kati ya hao wapo akina Nyoni, Manula na Kapombe, hivyo basi tusubirie kwanza mara baada ya kufikia muafaka mzuri kati yao basi tutaweka wazi kwani wachezaji ni wengi tuliokuwa nao kwenye mazungumzo,” alisema Kashembe.

SOMA NA HII  WAWILI WASEPA NA TUZO AFRIKA KUSINI MASHINDANO YA Cosafa