Home Uncategorized KOCHA MBRAZIL APONGEZA SILVER NA FRAGA KUSAJILIWA SIMBA ‘ WAMEPATA VIFAA’

KOCHA MBRAZIL APONGEZA SILVER NA FRAGA KUSAJILIWA SIMBA ‘ WAMEPATA VIFAA’


KOCHA Mbrazil aliyewahi kutamba na Taifa Stars na Azam, Itamir Amorin ameukubali usajili wa Wabrazil uliofanywa na Simba inayojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Agosti 9.

Itamir ambaye aliletwa Tanzania na Kocha Mbrazil mwenye heshima, Marcio Maximo kama msaidizi wake na mtaalam wa viungo wa Taifa Stars, ameliambia Spoti Xtra kwa njia ya simu kutoka Rio De Janeiro nchini kwake kwamba, Simba iko sahihi.

Simba imepanga kusajili Wabrazil watano lakini mpaka sasa imeshawasainisha watatu ambao ni Wilker Henrique
da Silva ambaye ni straika, Gerson Vieira na Tairone da Silva wote wanacheza nafasi ya beki na kiungo kiufasaha.

Itamir akizungumza na Spoti Xtra kwenye mahojiano maalum jana Jumamosi, alisema wachezaji hao watatamba sana Tanzania msimu ujao na watawaziba midomo wengi kwenye ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.

Alisema kwamba; “Nilisikia kuna usajili wa Wabrazil umefanyika Simba lakini nilikuwa sifuatilii sana, baadaye niliposikia na Gerson amesaini ikabidi niingie kiundani nijue kwavile huyo ni mchezaji mzuri sana.

“Nimeanza kumjua Gerson tangu akiwa kwenye timu za vijana za Brazil na kina Neymar, ni mchezaji mzuri sana huyo ndio maana amecheza ligi nyingi kubwa na thamani yake ni kubwa.

“Simba wamepata mchezaji mzuri sana, amekaa kwenye kiwango kwa muda mrefu. Hata Tairone nimemsikia na nimewahi kumuona, nina imani hawa wachezaji wataboresha sana kiwango cha Simba kama wakitumika vizuri,” aliongeza Itamir ambaye amewahi kuwa kocha wa muda wa Azam FC baada ya kutoka Taifa Stars enzi za Marcio Maximo ambaye sasa ni miongoni mwa wachambuzi na wataalam wa takwimu kwenye Copa America.

Kuhusu miundombinu ya Bongo na Wabrazil hao, Itamir alisema: “Sidhani kama suala la viwanja ni tatizo kwao, Brazil imeendelea sana kisoka lakini kuna sehemu nyingine vilevile zina miundombinu mibovu ya viwanja.

“Ukishakuwa mchezaji wa soka lazima ukubaliane na hali halisi na mpaka wao wanasaini Simba nadhani watakuwa wameshaelewa mazingira ya kazi yakoje.

“Hata huku klabu kubwa ndizo zenye viwanja bora, huko kwingine ni ubora wa kawaida. Hata kwenye Copa America inayoendelea hapa kwetu baadhi ya wachezaji wakubwa viwanja vinawapa shida lakini lazima kupambana kupata matokeo, mchezaji mzuri anacheza popote,” aliongeza.

Kocha huyo ambaye kwa sasa yuko kwenye programu za vijana, amesema kwamba yeye na wenzie wamekuwa wakifuatilia na kujua mambo mengi yanayoendelea Tanzania kwavile wameishi kwa miaka mingi na walipenda maisha yalivyokuwa.

Mbali na Wabrazil hao watatu, wachezaji wa kigeni wengine waliomwaga wino Simba ni Claytous Chama, Meddie Kagere na Msudan, Sharaf Eldin Shiboub

SOMA NA HII  NYOTA STARS: INAWEZEKANA KUPATA USHINDI LEO MBELE YA KENYA