Home Uncategorized SAMATTA KUTUA ENGLAND KESHOKUTWA

SAMATTA KUTUA ENGLAND KESHOKUTWA


Inaelezwa kuwa, mshambuliaji wa kimataifa wa KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta anatarajia kuondoka nchini kati ya keshokutwa Ijumaa au Jumatatu kuelekea nchini England kukamilisha mipango yake ya kucheza ligi kuu nchini humo.

Samatta ambaye ni nahodha wa Taifa Stars, anatajwa kugombewa na Klabu ya Leicester City na Middlesbrough zinazoshiriki Ligi Kuu England.

Samatta ambaye aliiongoza Taifa Stars kwenye michuano ya Afcon inayoendelea nchini Misri na kuishia hatua ya makundi, anatakiwa na timu hizo kwa dau lililotajwa pauni milioni 12 ambazo ni zaidi ya bilioni 32 za Kitanzania.

Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita alifunga mabao 23, katika Ligi Kuu ya Ubelgiji, amekuwa akitakiwa na timu nyingi barani Ulaya hasa England ambapo ukiziondoa Leicester na Middlesbrough, pia Aston Villa iliyopanda daraja kushiriki Premier nayo inamuhitaji.

Taarifa za uhakika kutoka katika chanzo cha kuaminika zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo anatarajia kuondoka nchini keshokutwa Ijumaa au Jumatatu ya wiki ijayo kutokana na visa yake kukamilika.

“Samatta bado hajaondoka lakini anatarajia kuondoka Ijumaa au Jumatatu ya wiki ijayo kuelekea zake England kwa ajili ya kukamilisha mipango yake baada ya kukamilisha taratibu za visa yake.

“Kiukweli bado hakuna anayejua atakwenda kucheza timu gani pale kwa sababu mwenyewe na wakala wake wanafanya siri, nadhani wanasubiri hadi kila kitu kikamilike,” kilisema chanzo.

SOMA NA HII  MTUPIAJI NAMBA MOJA MBAO KUSEPA