Home Uncategorized MAKOFI YA MASHABIKI YANGA KWA WACHEZAJI WAO BAADA YA KIPIGO NI TIBA...

MAKOFI YA MASHABIKI YANGA KWA WACHEZAJI WAO BAADA YA KIPIGO NI TIBA MPYA YA SOKA


Na Saleh Ally
BAADA Yanga kuchapwa mabao 3-0 katika siku ya kwanza ya kocha Luc Eymael akiwa ndio amekaa benchi, kama ilivyo ada jazba kutoka kwa mashabiki hutawala.

Kagera Sugar ndio walioifunga Yanga mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, juzi.

Kipigo hiki ni kikali zaidi kwa Yanga, huenda wapo waliotarajia wapoteze mechi yao dhidi ya Simba kwa idadi hiyo. Badala yake mambo yamekwenda kuharibika katika mechi dhidi ya Kagera Sugar ambao chini ya kocha Mecky Maxime, walionyesha soka safi na la kuvutia.

Baada ya mechi hiyo, niliona mashabiki kadhaa wa Yanga wakilalamika, aina ya kulaumu inayofanana siku zote na hasa kwa mashabiki wa klabu hizi mbili za Tanzania, yaani Yanga na Simba.

Wapo waliosema waliacha kazi zao kwenda uwanjani au walitumia nauli zao na kadhalika. Kama ambavyo niliwahi kusema, mishahara haichezi na kulipa mishahara mikubwa si gerentii ya kushinda mechi zote. Pia kama ukitoa nauli au kuacha kazi ukaenda uwanjani, haina maana lazima timu yako ishinde dhidi ya mpinzani inayekutana naye.
Hawa ni kati ya mashabiki wa Yanga ambao niliwaona wanahojiwa na kulalama kuhusiana na timu yao kushindwa kufanya vizuri katika mechi hiyo.

Pamoja na wao, baadhi ya mashabiki waliokuwa nje ya Uwanja wa Uhuru, wao walijipanga na kuachia njia katikati halafu wakawa wanawapigia makofi wachezaji wao wakati wakiingia kwenye gari waondoke.

Mashabiki hao walifanya hivyo kwa takriban dakika nane hivi wakati wachezaji hao wakipita na kuingia kwenye gari muda mchache baada ya kuwa wamepoteza mchezo huo, difensi ikiruhusu mabao matatu bila ya fowadi yao kufunga hata bao moja!

Nilishangazwa kidogo na hali hii, huenda kutokana na uzoefu wangu katika michezo na hasa soka hapa nyumbani. Yanga wanajulikana, ndio waanzilishi wa neno bakora katika soka. Maana wao wachezaji wakikosea, basi wanawavaa na kuwashambulia kwa maneno makali na vitisho na imekuwa kawaida.

Mashabiki wa Simba, wanajulikana kwa kuwadekeza wachezaji na mara nyingi wao huangusha mzigo kwa viongozi wao hata kama mchezaji anakosea. Katika hali ya kawaida kwa wale wachezaji, wangekutana na maneno makali ya kuwashambulia, kuwaonya na kuwatisha.

Wapo wanaosema Yanga walifanya hivyo kwa kuwa siku chache zilizopita, mashabiki wa Simba waliwazomea vibaya wachezaji wao wakati wakiwasili bandarini jijini Dar es Salaam wakitokea Zanzibar ambako walipoteza mchezo kwa kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar.

Hata kama kweli ingekuwa hivyo, bado haifuti kwamba waliofanya hivyo ni mashabiki wa Yanga, mashabiki ambao wanajulikana kwa kuwa wakali, wakorofi lakini leo wamefanya kile ambacho kinafanyika katika mpira wa kiwango cha juu.

Kwamba mashabiki wanajua timu yao inatakiwa kushinda lakini kuna siku inaweza kupoteza na wanatakiwa kuungana na wachezaji wao wanapokuwa wameshinda au wamefungwa. Si sahihi kuungana na wachezaji wenu wanapokuwa wameshinda tu, mnafurahi pamoja. Siku mkipoteza basi, timu inakuwa ya wachezaji, kocha na uongozi tu, mashabiki mnajiengua.

Kumkosoa mtu wakati mwingine unaweza kumueleza bila ya kumfokea na ujumbe ukafika kwa usahihi zaidi. Hili ndilo ambalo wamelifanya mashabiki wa Yanga baada ya wachezaji wao kupoteza kwa Kagera.

Ikifikia siku wamekasirika kwa maana ya kuchoshwa na uzembe, itakuwa kuna wepesi wa kuwaelewa na wachezaji na viongozi watatakiwa kukumbuka tukio hili la kupigiwa makofi ya kuonyeshwa kuwa wako pamoja nanyi licha ya maumivu ya kipigo hicho kikubwa kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara ambacho unaweza kusema ni kikubwa hasa.
 Walichokifanya mashabiki hao mara kadhaa tumekuwa tukiona wanafanya Simba ambao hivi karibuni wao wamewazomea wachezaji wao. Lakini aina hii ya muungano, tumekuwa tukiona Ulaya kwa mashabiki kuwapigia makofi wachezaji wao hata baada ya kupoteza mchezo wakiwaonyesha wanajua kwenye mchezo kuna kupoteza, hivyo wakajiandae wakati mwingine wapambane na kushinda.

Ujumbe wa mashabiki hao umeonyesha kuna mabadiliko yanakuja katika soka na ushabiki wa kuzomea pekee. Lakini wameonyesha kuwa wachezaji wanaweza kupewa ujumbe kwa njia tofauti na kitakachofuata ni wao wenyewe kuamua kuupokea na kuufanyia kazi.
Kushangilia mpira si kulaumu tu, vizuri tukubali wanaopambana wakati mwingine huzidiwa katika mapambano. Hivyo mashabiki wameacha deni lao kwa wachezaji katika njia sahihi, wachezaji nao watatakiwa kulilipa kwa kuonyesha kweli juzi, haikuwa siku yao nzuri na watapambana kusimama tena.


SOMA NA HII  BEI MPYA ZA VING'AMUZI VYA DSTV, MAMBO KWA ULAINII....