Home Uncategorized NIYONZIMA APEWA MZIGO YANGA

NIYONZIMA APEWA MZIGO YANGA


Akianza kibarua cha kukinoa kikosi cha Yanga, kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Luc Eymael amempa jukumu zito kiungo mchezeshaji fundi Mnyarwanda Haruna Niyonzima la kupiga kona na faulo kwenye mechi watakazozicheza.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu kocha huyo akabidhiwe jukumu la kukinoa kikosi hicho kinachowania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu unaotetewa na watani wao, Simba

Kocha huyo amekabidhiwa kikosi hicho baada ya timu hiyo kumsitishia mkataba aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Mkongomani Mwinyi Zahera kabla ya Charles Mkwasa kukaimua nafasi hiyo kwa muda wa mwezi mmoja na wiki moja.

Jumanne ya wiki hii wakati Yanga ikifanya mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar, Spoti Xtra lilikuwepo mazoezini hapo na kumshuhudia kocha huyo akimtaka kupiga kona na faulo zote zitakazokuwa zikitokea upande wa kushoto ambazo awali zilikuwa zikipigwa na Mrisho Ngassa na David Molinga.

Lakini katika mazoezi hayo, pia kocha alionekana mara kadhaa akimuelekeza kiungo huyo mwenye uwezo wa kuchezesha timu jinsi ya kupiga mipira ya kona.

Akizungumzia hilo, Luc alisema kuwa “Ninajaribu kuwaongezea baadhi ya vitu vya ufundi ambavyo nimeviona hawana na lengo ni kuhakikisha ninaifanya timu inakuwa bora itakayoleta ushindani.

“Ndiyo sababu ya leo (juzi) kuwapa program ya kupiga mipira ya kona na faulo za nje ya 18, pia nimewapa mbinu za jinsi ya kushambulia na kuokoa hatari golini kwetu,” alisema Eymael.
SOMA NA HII  YANGA: TUNASUKA KIKOSI MATATA