Home Uncategorized YANGA WAAMUA KUIIGA SIMBA, HIKI NDICHO WADHAMIRIA KUFANYA JUU YA CEO

YANGA WAAMUA KUIIGA SIMBA, HIKI NDICHO WADHAMIRIA KUFANYA JUU YA CEO


Kampuni ya GSM imepanga kuiendesha Klabu ya Yanga kisasa kwa kuleta Mtendaji Mkuu (C.E.O), mpya wa timu hiyo atakayeifanya kuwa ya kisasa ili kufikia mafanikio yao.

GSM ni kati ya wadhamini wa Yanga ambao hivi karibuni ilishinda zabuni ya kuuza jezi za timu hiyo kwenye msimu huu wakitumia kitita cha Sh Bil. 1 huku ikizishinda baadhi ya kampuni.

Kampuni hiyo, pia ilichangia kitita cha Sh Mil. 300, kufanikisha usajili wa wachezaji katika dirisha kubwa kabla ya dirisha dogo linalotarajiwa kufungwa leo saa sita usiku.

Yanga wamefanikiwa kuwasajili nyota watano ambao ni Haruna Niyonzima, Yikpe Gnamien, Ditram Nchimbi, Tariq Seif na Adeyum Saleh.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kutoka ndani ya Yanga, matajiri hao wapo kwenye mchakato wa mwisho wa kumpata C.E.O huyo.

Mtoa taarifa huyo, alisema upo uwezekano mkubwa wa C.E.O mpya akatokea nchini Ghana huku jina lake likifichwa ambaye atajulikana baada ya kufikia makubaliano mazuri ya kujiunga na klabu hiyo.

Aliongeza kuwa C.E.O huyo atakayekuja atapewa mipango mikakati ya kuhakikisha anaitengeneza Yanga ya kimataifa ili kufikia malengo yao na kikubwa ni kufikia malengo waliyojiwekea ya kuifanya klabu hiyo ipige hatua kama Zamalek, Al Ahly, TP Mazembe na Kaizer Chiefs zote za Afrika.

“Wanachokifanya GSM ni kutaka kuisuka Yanga ili iwe ya kimataifa na ndiyo maana kwa kuanza walianza katika kusajili wachezaji wenye uwezo na hadhi ya kufikia malengo makubwa Afrika, hasa katika michuano ya kimataifa.

“Baada ya kufanya usajili huo, GSM wakamleta kocha mpya raia wa Ubelgiji ambaye ni Luc Aymael kabla ya kuleta kocha msaidizi na wa viungo kutoka Afrika Kusini, Riedoh Berdien ambao wote wamesaini mikataba ya mwaka mmoja na miezi sita pekee.

“Hivyo, baada ya kukamilisha hilo la usajili na kulisuka benchi la ufundi kwa kuleta makocha hao, hivi sasa wapo kwenye mipango ya kumleta C.E.O atakayefanya kazi pamoja na benchi hilo kuna baadhi ya watu wanafuatilia hilo na wengine tayari wapo nje ya nchi,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kupitia kwa Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM, injinia Hersi Said hivi karibuni alizungumza na Championi Jumatano na kusema kuwa: “Tupo kwenye mipango mikubwa na mizuri ya kuifanya Yanga iwe ya kimataifa na hayo ndiyo malengo yetu GSM kama wadhamini wa timu.

“Ninaamini tutafanikiwa katika hilo na uzuri, mashabiki wenyewe wanaona kila kitu kinachofanyika kwa uwazi katika timu, hivyo kuna mambo mengi tuliyopanga kuyafanya Yanga kwa kipindi chote tutakachokuwa nacho,” alisema Hersi.
SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATATU

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here