Home Uncategorized MAKOCHA LIGI KUU BARA: SIMBA WAPEWE KOMBE LAO, KASI YAO NI NOMA

MAKOCHA LIGI KUU BARA: SIMBA WAPEWE KOMBE LAO, KASI YAO NI NOMA


 Makocha wa Biashara United na Namungo wamekiri kwamba kwa kasi hii ya Simba msimu huu, ni vigumu kuwazuia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha wa Biashara United, Francis Baraza, amesema Simba wanayo nafasi kubwa ya kuwa mabingwa msimu huu na hakuna muujiza wowote utakaowazuia kuwa mabingwa.

Kocha huyo alivaana na Simba na kuambulia kichapo cha mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar akiwa amepigwa na Mnyama mechi zote mbili msimu huu.

Kocha huyo aliweka rekodi ya kutopoteza kwenye mechi sita mfululizo lakini akakumbana na kasi ya kimbunga ya Simba iliyompotezea mwelekeo. 


“Kwa jinsi ligi inavyoendelea na namna Simba wanavyocheza ni wazi hakuna wa kuwazuia kuchukua ubingwa, niliwaandaa vijana wangu kuwadhibiti lakini walituzidi uwezo na tumeruhusu mabao mengi kwenye mchezo huu,” alisema Baraza.

Biashara United wanashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 32.

Kwa upande wake kocha wa Namungo, Hitimana Thierry, naye amesisitiza Simba haizuiliki.

Thierry aliiongoza Namungo kuifunga Azam kwa bao 1-0 lakini alishachapwa 3-2 na Simba Uwanja wa Taifa, Dar. 


“Watu wengi wamekuwa wakiniuliza kama Namungo inaweza kushindana katika mbio za ubingwa msimu huu lakini kila mara nimekuwa nikiwajibu kuwa hilo jambo ni kama kujidanganya. 

“Kwani kwa upande wangu nadhani ni vigumu kwa timu yoyote kuizuia Simba kushinda taji la ligi kuu msimu huu kutokana na uwezo ambao wamekuwa wakiuonyesha unaochagizwa na kuwa na wachezaji wa viwango vya hali ya juu,” alisema Thierry.

Namungo imekuwa na kiwango kizuri katika msimu wake wa kwanza tu ikikamatia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kujikusanyia alama 43 katika michezo 23.

SOMA NA HII  YANGA YAJIPA NAFASI YA KUSHIRIKI MICHUANO YA KIMATAIFA