Home Uncategorized POLISI, PRISONS ZANUFAIKA NA MVUA

POLISI, PRISONS ZANUFAIKA NA MVUA


TIMU ya Tanzania Prisons ya Mbeya na Polisi Tanzania zinazomilikiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, wiki hii zimefanikiwa kuondoka na ushindi kwenye mechi zao za Ligi Kuu ambazo ziliahirishwa kuchezwa juzi jioni kutokana na mvua kubwa kunyesha jijini Dar es Salaam na Dodoma na kusababisha viwanja kujaa maji.

Mechi hizo zilizopigwa juzi asubuhi, Prisons iliichapa KMC ya Kinondoni bao 1-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, huku Polisi Tanzania ikiichapa JKT Tanzania bao 1-0 katika Uwanja wa Uhuru.

Prisons ambayo imekimbilia Dodoma na kuufanya Uwanja wa Jamhuri kuwa wake wa nyumbani badala ya Uwanja wa Samora Iringa iliyokuwa ikichezea kama uwanja wa nyumbani kwa muda, ilipata bao pekee dakika ya 22 likifungwa na straika wao mkongwe Jeremiah Juma dakika ya 22.

Timu hiyo yenye maskani yake mjini Mbeya, awali ilikuwa ikitumia Uwanja wa Sokoine mjini humo, lakini ulipigwa marufuku na Bodi ya Ligi, baada ya kuharibiwa kutokana na kutumiwa kwenye shughuli za tamasha la muziki.

Kwa matokeo hayo, timu hiyo imefikisha pointi 21 kwa michezo 17 iliyocheza, huku ikikamata nafasi ya 12.

Kwa upande wa KMC, imefikisha jumla ya pointi 17, kwenye michezo 17, huku pia ikiwa imecheza mechi 17.

Kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salam, Polisi Tanzania ikiwa ugenini iliibuka na ushindi wa bao 1-0, ikiwa ni mechi nyingine ambayo ilibidi ichezwe juzi, lakini ikaahirishwa kwa sababu ya mvua kubwa jijini Dar es Salaam.

Bao pekee lililoipa ushindi Polisi Tanzania lilifungwa na beki wa siku nyingi nchini, Jimmy Shoji.
Kwa matokeo hayo, timu hiyo inapaa mpaka kwenye nafasi ya saba, ikiwa imecheza mechi 17, na kujikusanyia pointi 27.

JKT Tanzania yenyewe iko kwenye nafasi ya nane ikiwa na pointi zake 26, baada ya mechi 17.
SOMA NA HII  LUSAJO AFUNGUKA ISHU YAKE YA KUTUA YANGA