Home Uncategorized WAAMUZI WASIMALIZIE HASIRA ZAO MGONGONI MWA YANGA, SIMBA

WAAMUZI WASIMALIZIE HASIRA ZAO MGONGONI MWA YANGA, SIMBA



Na Saleh Ally
NDANI ya wiki mbili kumekuwa na malalamiko mfululizo kuhusiana na uchezeshaji wa waamuzi katika Ligi Kuu Bara.

Mwanzo ilianza kama vile Simba walikuwa wanapendelewa sana, gumzo likawa ni hilo kwa muda lakini uhalisia ni kwamba waamuzi walikuwa wanaboronga.

Baada ya watu kufumbuliwa macho kwamba ishu haikuwa Simba kupendelewa, walianza kufungua macho yao kwa upana zaidi na kweli wakabaini shida ilikuwa ni uwezo wa waamuzi na si suala la Simba kupendelewa.

Hakuna ubishi waamuzi hasa wale wa pembeni wamekuwa na makosa mengi makubwa na dhahiri walistahili adhabu.

Kama unakumbuka walianza kwa kupewa onyo lakini baada ya hapo ilikuwa utafikiri sasa wameamshwa wazidi kukosea na wahusika wakaona ilikuwa imepitiliza, wakachukua hatua ya kuwapa adhabu kali, mmoja akifungiwa miaka mitatu.

Adhabu kali, lilikuwa ni jambo sahihi kabisa kwao ili kuweka mambo sawa. Kukosea kwa mwanadamu yoyote kunawezekana lakini si kujirudia kwa makosa mfululizo bila ya kujirekebisha.

Adhabu hizo zilizotoka zinaonyesha zimefika “vichwani” mwa waamuzi. Wako ambao wamekuwa wahanga na sasa hawatachezesha au wale waliopewa onyo.

Wako wale ambao hawajaguswa lakini inaonekana wametambua safari hii hakuna mchezo kwa walioboronga, maana yake hofu kuu imetawala miongoni mwao na huenda wamelichukulia kwa papara suala hilo la wao kuadhibiwa. Maana, wamegeuka wenye hofu kupindukia na hofu yao inataka kugeuka uonevu kwa Yanga na Simba.

Hakuna aliyewaambia waamuzi Yanga na Simba wanapaswa kubanwa, au wakipata bao au penalti halali inakuwa si sahihi. Lakini inawezekana miongoni mwao wamefikiri namna hiyo, si jambo sahihi.

Baada ya waamuzi kupewa adhabu, mechi ya kwanza Simba kurudi uwanjani ilikuwa dhidi ya JKT Tanzania ambayo iliisha kwa mabingwa hao watetezi kupoteza kwa bao 1-0.

Simba wamefungwa bao hilo la kichwa halali na hakuna ubishi, waamuzi wote wawili walifanya kazi yao vizuri. Baadaye kipindi cha pili Simba nao walifunga bao zuri kupitia kiungo Mbrazil, Gerson Fraga, ajabu mwamuzi msaidizi wa pili ambaye alikuwa makini wakati JKT Tanzania wakifunga, akalikataa.

Siku iliyofuata, Yanga ilishuka dimbani kuivaa Ruvu Shooting, mechi ikaisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0, likifungwa na David Ndama Molinga. Kabla ya bao hilo, Yanga walipata penalti halali kabisa, kiungo wao wa pembeni Bernard Morrison akiangushwa dhahiri ndani ya 18 na waamuzi wote wawili akiwemo msaidizi namba moja wakiwa karibu kabisa.

Ajabu wote walisema ni kona badala ya goal kick. Kwa sababu kama ni halali, waliamua kusema haikuwa penalti, basi mpira haukutolewa na Morisson wa Yanga badala yake ulitolewa na Mghana huyo kwa kuwa hakuna mchezaji wa Shooting aliugusa mpira badala yake mwili wa mchezaji huyo wa Yanga ambaye aliangushwa.

Jambo zuri sana kupunguza makosa yanayoepukika, jambo sahihi kabisa kuongeza umakini na si sahihi wala vema hata kidogo waamuzi kuanza kuona Yanga na Simba wanapendelewa hata kwenye haki.

Wanachopaswa ni kutoingia kwenye maneno ya kishabiki wala kutojaribu kuwaridhisha mashabiki kuona Simba na Yanga hawafungi au wanapoteza michezo kwa nia ya kuondoa yale mawazo kuwa wanapendelewa.

Kama wanashinda hata kwa mabao 10 kwa kila mechi na ni halali kabisa, basi wapewe nafasi wafanye yao na waamuzi wafanye kazi yao vizuri ya kuamua kwa usahihi wakifuata kwa ubora na weledi sheria 17 za soka.

Kuendelea kuzikandamiza Yanga na Simba kwa lengo la kuzikomoa, au kutaka kufurahisha wengine, si jambo jema. Badilikeni. 

SOMA NA HII  USHINDANI NDANI YA LIGI KUU BARA UNAHITAJIKA, TIMU ZIBORESHE VIKOSI MSIMU UJAO