Home Uncategorized MAISHA BANA! GHAFLA KLOPP KAGEUKA MTU WA HOFU TUPU, KADONDOSHA KARIBU KILA...

MAISHA BANA! GHAFLA KLOPP KAGEUKA MTU WA HOFU TUPU, KADONDOSHA KARIBU KILA KITU


Na Saleh Ally
SIKU za furaha na majigambo zimeporomoka haraka sana katika kikosi cha Liverpool, kikosi ambacho kilionekana hakina mfano kwa misimu miwili mfululizo.
Liverpool walikuwa wanaonekana na nafasi kubwa ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England, Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya na kama wakikosea, basi mawili kati ya makombe hayo hawatayakosa.


Kombe pekee walilokuwa wameng’oka mapema ni lile la ligi, maarufu kama Carabao Cup na ilionekana wazi hawakuwa wameweka nguvu na kikosi cha pili kikakutana na kipigo na kutolewa.


Maana yake nguvu zao zikabaki katika EPL, FA Cup na Champions League ambayo tayari wanaishikilia. Pamoja na kwamba Liverpool hamu kuu ni ubingwa wa England lakini kwa timu kubwa kama wao, wanahitaji makombe zaidi ya moja kuendelea kubaki na sifa ya klabu kubwa inayofanya vizuri katika kipindi hiki.


Ndani ya wiki mbili, mambo yamebadilika haraka sana, Liverpool sasa wana nafasi moja tu ya kubeba kombe, nayo ni Ligi Kuu England.


Wiki moja ilianza kwa wao kung’olewa na Chelsea katika Kombe la FA, wakafungwa mabao 2-0 ikiwa ni siku chache baada ya wao kupokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Watford wakipoteza mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England baada ya kuwa wamecheza mechi zaidi ya 40 bila ya kupoteza mchezo hata mmoja.


Unaona baada ya kupoteza mchezo wa ligi, wanakwenda kutolewa katika Kombe la FA, wakiwa na matumaini ya kusonga mbele, nako wanapoteza pia.


Siku chache baadaye, Liverpool wanakutana na kipigo kingine ambacho hakikutarajiwa baada ya kufungwa kwa mabao 3-2 na Atletico Madrid, wakiwa nyumbani Anfield, sehemu ambayo hawakuwa wamepoteza mchezo wa michuano ya Ulaya tangu mwaka 2014.


Kabla, walikuwa wamepoteza mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 Bora mjini Madrid dhidi ya Atletico na matumaini yakawa makubwa kuwa mambo yatakaa sawa Anfield ambako ni “machinjioni” kwa kila mgeni maana ukitua hapo hawakuachi.


Ajabu, Liverpool wameanguka wakiwa nyumbani na unaona ndani ya wiki nne, mkononi wamebaki na kitu kimoja tu ambacho ni Ligi Kuu England.


Liverpool imedondosha karibu kila kitu ilichokuwa inakitegemea, karibu kila kitu ilichokuwa inaamini kitabaki mikononi mwao na sasa ni kama ‘roho’, kilichobaki ni ubingwa wa Ligi Kuu England pekee.


Kweli ubingwa huo ndio walikuwa wanahitaji mashabiki wa Liverpool kwa kuwa wameukosa kwa zaidi ya miaka 30 na wako ambao walianza kuishangilia Liverpool tangu wakiwa shule za msingi na sasa wamemaliza chuo kikuu, hawajawahi kuiona ikibeba ubingwa huo.


Nahodha wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard, tangu ametua Liverpool mwaka 1998 hadi anaondoka 2015, hakuweza kukata kiu hiyo ya Wana Liverpool. Hivyo ni jambo ambalo watakuwa wanalisubiri kwa hamu lakini roho mkononi.


Pekee ambacho sasa kinakuwa ni sehemu ya kile wanachoweza kusimamia ni pengo la pointi katika msimamo wa Ligi Kuu England wakiwa wanaongoza kwa pointi 82 wakati aliye katika nafasi ya pili, Manchester City ana 57.


Pengo la pointi 25, hata kama City akishinda kiporo kimoja maana yake itakuwa pointi 22 pengo, bado ni kubwa sana na ndio silaha ya Klopp kwa sasa.


Liverpool imebakiza mechi tisa ifunge msimu na kama itashinda mechi tano mfululizo tokea sasa itakuwa na mechi 34 na kama Man City atakuwa amepoteza mechi moja au sare, watakuwa na uwezo wa kuwa mabingwa wakiwa na mechi nne mkononi.

Manchester City ndio wanaoweza kuirahisishia Liverpool kubeba ubingwa mapema na hasa kama watapoteza mechi zao ndani ya tano zijazo.


Kama kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kitaendelea kufanya vizuri, kitaendelea kuilazimisha Liverpool kufanya vizuri huku ikisubiri.


Ikitokea Manchester City wakafanya vibaya katika mechi mbili au tatu, nafasi ya Liverpool kutangazwa mabingwa mapema na lazima wataweka nguvu zao zote hapo, basi wanaweza kufuta machungu na kusahau walivyodondosha karibu kila kitu ndani ya mwezi mmoja tu na kubaki na ubingwa wa EPL.

Hofu ya mashabiki wengi wa Liverpool ni timu yao kuanza kuonekana inawezekana kufungika. Namna ambavyo EPL ni ngumu mwishoni wakati wao wakionekana kama wamechoka lakini pia ugonjwa wa Corona unaotokana na virusi vya Covid-19.


Mechi za Premier tayari zimeahirishwa hadi Aprili 4, hofu ni kwamba Liverpool italazimika kuanza upya baada ya ligi kurejea, jambo ambalo linaweza kuwafanya wakalazimika kuanza kutengeneza kasi yao baada ya kurejea.




SOMA NA HII  KIUNGO FUNDI ANAYEKIPIGA KARIOBANG SHARKS AKUBALI KUSAINI YANGA