Home Uncategorized CORONA KIPIMO CHA UKOMAVU WA WACHEZAJI

CORONA KIPIMO CHA UKOMAVU WA WACHEZAJI

HALI sio shwari kwa sasa kwa kuwa mambo megi duniani yamesimama na hii inatokana na maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vinaitikisa dunia.
Kwenye kila sekta Corona imegusa na kuweka mtikisiko wake huku maumivu yakiwa ndani ya mioyo ya watu.
Ninaona kabisa mambo yanazidi kuwa magumu katika sekta nyingi lakini haina maana kwamba tunapaswa kukata tamaa hapana ni wakati wa kufanya dua kwa Mungu ili janga hili lipite.
Kila kona wamekuwa na namna yao ya kupambana ili kuchukua tahadhari ambapo kwenye sekta ya michezo ambayo inajumuisha watu wengi asilimia kubwa ligi nyingi zimesimamishwa kwa muda usiojulikana.
Tunaona kuna baadhi ya nchi kama Ubelgiji ligi zao zimefutwa pamoja na ile ya Uholanzi hizi msimu huu hazitaendelea na sababu kubwa ni Corona.
Ujue kuna watu ambao bado wanaichukulia kawaida hili tatizo kiukweli kabisa hili janga ni kubwa na lina balaa lazima tuchukue tahadhari kwa umakini kabisa.
Kila mmoja kwa sasa ni lazima awe balozi wa usalama wa mwenzake ili kuona kwamba kila mmoja anakuwa salama kwa wakati huu ambao upo.
Majirani zetu Kenya, Uganda, Rwanda nao pia wapo kwenye suala la kuchukua tahadhari nasi tusipuuze tufanye hivyo ili kulinda afya zetu na familia pia.
Ligi zote hapa Bongo pia zimesimamishwa hilo lipo wazi na wachezaji wamekosa kucheza kwa muda mrefu haina namna ya kuzuia ni lazima kukubali hali halisi.
Wale ambao wanafikiria hili suala ni jepesi basi kuna ulazima wa kufikiria upya na kuanza kuchukua tahadhari kwa kuwa mambo bado hayajawa shwari.
 Wachezaji kwa sasa wengi wapo majumbani ambapo wanaendelea na program ambazo wamepewa na benchi la ufundi.
Kwa muda huu ni wakati wao kuonyesha kwamba wamepevuka kwa kutimiza yale ambayo wamepewa ili kulinda vipaji vyao.
Kipimo cha wao kuwa peke yao nyumbani ni kufanya mazoezi binafsi na kujisimamia kwa umakini bila kumdanganya mwalimu wao kwa sababu hayupo.
Program zao sasa ambazo wamepewa wanapaswa wazifanye kwa umakini mkubwa bila kukosea kwani ni kazi yao na maisha yao kwa sasa.
Ni wakati wa wachezaji kujipanga wenyewe wakiwa nyumbani na uzuri ni kwamba ratiba inakuwa mikononi mwao wenyewe wanajua namna ya kuipanga kiusawa bila kupangiwa.
Iwapo watashindwa kuwa waaminifu katika kipimo hiki ambacho kimesababishwa na Corona wanaingusha timu jumla pamoja na wao wenyewe kuzidanganya nafsi zao.
Iwapo watakuwa wanafanya mazoezi nyumbani kwa sasa pindi watakaporejea iwe leo ama kesho kwenye mechi za Ligi Kuu Bara mambo yatakuwa wazi na kila mmoja ataona namna ambavyo walikuwa wakijifungia ndani na kufuata zile program walizopewa.
Matokeo yataonekana uwanjani kwani mchezo wa mpira ni namba daima huwa hazidanganyi katika kuleta ukweli wa mambo yale ambayo yamejificha.
Kila mmoja yupo nyumbani kwa wakati huu hilo lipo wazi na hakuna namna ya kumfanya mwalimu awe ndani ya nyumba ya kila mchezaji kutazama kile anachokifanya.
Hivyo leo ligi ikianza itakuwa wazi kwa kila mchezaji ambaye alikuwa anafanya mazoezi ama anarukaruka tu wakati huu wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona.
Hali hii haipo kwetu pekee hata kwa wenzetu ambao wameendelelea huko Ulaya wanapitia ugumu katika kufuatilia mazoezi ya wachezaji pamoja na lishe.
Hivi karibuni tumeskia Manchester United wao wanatoa somo la masuala ya upishi kupitia mitandao kwa wachezaji wao inatokana na kujali na kuhitaji namna gani wachezaji wao wale lakini bado mambo ni magumu.
Ila teknolojia kule mbele kwa wenzetu inawabeba kwani kuna wakati ambao mwalimu anaweza kufanya na wachezaji mazoezi kupitia kwenye mtandao na kila mmoja akamuona mwalimu na wakapeana maelekezo kwa vitendo.
Muda unavyozidi kwenda hali inakuwa tete kwa sasa hivyo ni jukumu sasa la wachezaji kuona namna gani watalinda vipaji vyao ambavyo vinahitaji kulindwa kwa kufanya mazoezi.
Sisi hatupo sawa na mbele kwamba tuanze kufanya mazoezi ya vitendo kwa mtandao ingawa tunafuatilia sio kwa wepesi ule ambao wenzetu wanapata.
Pia na kwa upande wa miundombinu wachezaji wa nje wanakila kitu ndani utakuta mchezaji nyumbani kwake ana uwanja wa kuchezea mpira, sehemu maalumu ya kufanyia mazoezi, bwawa na kila kifaa kinachopatikana kwenye timu.
Kwetu sisi hiyo ni ngumu kuwa hivyo ni wachache sana ambao wanajitambua utakuta wana baadhi ya vitu ambavyo vinawafanya wawe katika ubora.
Yapo aina ya mazoezi ya kufanya kwa wakati huu sio yale magumu sana lakini ni muhimu kuyafanya kwa kuwa vifaa ni hafifu inakuwa ngumu kutimiza zile baadhi ya program kwa ufasaha.
Tuzidi kuchukua tahadhari na kundelea kuomba dua kwa kuwa hali bado sio poa na Serikali inazidi kuongeza nguvu katika kupambana na suala hili hivyo nasi tunapaswa tuunge mkono juhudi za Serikali bila kupinga.
SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTIXTRA ALHAMISI