Home Uncategorized UMAKINI NA TAHADHARI KWA SASA NI MUHIMU

UMAKINI NA TAHADHARI KWA SASA NI MUHIMU

BADO mambo ni magumu kwa sasa na hii ni kutokana na janga la Virusi vya Corona ambavyo vinaendelea kuitikisa dunia kiujumla.
 Sio shule, soka na mikusanyiko isiyo ya lazima kwa nchi nyingi haijaruhusiwa na hii ni kutokana na janga hilo.
 Kupitia mitandao ya kijamii  wachezaji wengi wamekuwa wakiandika kuwa wanatamani kurejea uwanjani  na hawa ni wale wa Bongo na Ulaya.
 Kutokana na janga hili hapa Bongo makocha wamejitahidi kutoa program kwa wachezaji wao kuhakikisha wanaendelea kulinda viwango vyao.
 Ligi Kuu Bara  pamoja na ligi nyingine bado haijafahamika  ni lini rasmi zitarejea kwa sasa hivyo kikubwa kuwa na subira pamoja na dua.
 Wachezaji kadhaa wamekuwa wakionekana wakiendelea na mazoezi yao binafsi kama kawaida bila tatizo lolote.
 Lakini  tunaamini wachezaji wengi wa kibongo watakuwa wanazingatia yale ambayo wamekuwa wakielezwa kufanya na makocha wao ili kulinda viwango vyao.
 Wachezaji wapo majumbani  lakini sasa hivi ni wakati wao muafaka wa kujituma na kuendelea kulinda viwango vyao ili ligi itakaporejea basi  mambo yaweze kwenda sawa.
 Wachezaji ni watu ambao wanajielewa na wanatambua ni kitu gani wanatakiwa kufanya kipindi hiki kwa manufaa yao binafsi pamoja na klabu zao.
 Huko waliko wachezaji sasa wanatakiwa kujituma kwa bidii na kuweka malengo ligi itakaporejea tunaweza kushuhudia mambo mengi ambayo hayakutarajiwa.
 Wachezaji wasipokuwa makini na kuzingatia suala la kujitunza na kufanya mazoezi itakuwa ni jambo rahisi zaidi kwa makocha ligi itakaporejea kuwachuja vizuri hasa kuelekea katika msimu mpya wa ligi.
 Ligi  itakaporejea ni wazi klabu zitakuwa zinaelekea katika kipindi cha usajili wake na nyakati za mwisho ndiyo sehemu muafaka kwa wachezaji kuonyesha kile walichonacho ili makocha waweze kutoa uamuzi sahihi kwa ajili ya usajili mpya.
 Kuna wachezaji wamekuwa na tabia ya uvivu wa kufanya mazoezi wanapokuwa na timu, lakini wakati kama huu unaweza kujiuliza je wale wachezaji kipindi hiki cha Corona wanafanya mazoezi kweli au ndiyo wanaendelea na mambo yao bila kuzingatia kazi zao.
Soka ni mchezo ambao unachezwa hadharani hivyo ligi itakaporejea kila mmoja ubora wake utaonekana pale na  kipindi hiki  makocha watapata wachezaji sahihi sababu Corona kwa upande mmoja au mwingine imekuwa kama kipimo kwa wachezaji kuona kweli wanaweza kuzingatia  program walizopewa au ndiyo wataendelea na ratiba zao binafsi.
SOMA NA HII  KIUNGO MPYA SIMBA AKOMBA MILIONI 138