Home Uncategorized KUREJEA LIGI KUU BARA, WAKATI MZURI KUTATHMINI UBORA WA LIGI KUU BARA…

KUREJEA LIGI KUU BARA, WAKATI MZURI KUTATHMINI UBORA WA LIGI KUU BARA…



Na Saleh Ally
SERIKALI imepitisha kurejea kwa Ligi Kuu Bara na huu utakuwa ni wakati mzuri wa kuufanya ule mjadala wetu kwa vitendo. Kwamba wachezaji wa kigeni wabaki hao 10 kwa kila timu au wapunguzwe.


Nazungumzia mjadala unaohusiana na kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni au wabaki vilevile.


Kila mmoja atakuwa anashiriki kivyake, kwa maana ya kuwa na kile anachokiamini ingawa nimekuwa nina angalizo katika hizi pande mbili. Moja, watu wasifanye mambo kisiasa, badala yake hata kama ni maoni, iwe kwa kuangalia uhalisia hasa.


Pili, wanaohusika walio na meno, basi wasiwe na uamuzi tayari lakini wakasema mashabiki watoe maoni na hapa ilikuwa vizuri kuwatumia zaidi wataalamu badala ya mashabiki tu ambao wanaweza pia kuamua mambo kishabiki zaidi.


Mpira si kazi ya mashabiki unapozungumzia masuala ya ufundi, haya hufanywa na wataalamu na mashabiki wakamalizia kushangilia ambayo ni furaha yao.

Hivyo, wanaweza kushirikishwa mashabiki lakini wataalamu kwa maana ya wale wanaotambua uhakika wa mambo kama makocha, wachezaji wenyewe, viongozi wa klabu, vyama, shirikisho, ikiwezekana hata wachumi na kadhalika, wakapewa nafasi kubwa pia.


Wakati tunasubiri hayo, huu ni wakati mzuri wa kuanza kufanya tathmini kwa vitendo kwa kuwa Ligi Kuu Bara inarejea.

Tulishaanza, tumekwenda zaidi ya nusu, unapozungumzia suala la msimu wa 2019/20. Unaona Yanga ndiyo wana mechi nyingi, ni 11. Wengi ni tisa na wachache 10.

Kama utazijumlisha zinatosha sana kwetu kufanya tathmini ya wachezaji wa kigeni ndani ya soka ya Tanzania na hapa tutakuwa na majibu baada ya msimu kwisha.

Ukiangalia kwa wafungaji, anaongoza Meddie Kagere, raia wa Rwanda mwenye asili ya Uganda. Huyu pia ndiye mfungaji bora wa msimu uliopita.

Angalia wanaomfuatia watatu wote ni wazalengo na kila mmoja ana mabao 11 ya kufunga. Hawa ni Yusuf Mhilu (Kagera Sugar), Reliant Lusajo (Namungo FC) na Paul Nonga kutoka Lipuli FC na baada ya hapo kuna mchanganyiko wa wenyeji na wageni katika mabao 9 na 8.

Braise Bigirimana, Mrundi wa Namungo FC na Peter Mapunda wa Mbeya City, kila mmoja ana mabao 9 huku watatu wakiwa na mabao nane kila mmoja ambao ni mzalendo Daruwesh Saliboko wa Lipuli FC na wageni wawili, David Molinga (Yanga) na Obrey Chirwa wa Azam FC.

Ushindani huu, mwisho wa ligi unaweza kufanya tathmini ukaona, kiasi gani wageni wamefanikiwa na wenyeji wamefanyaje. Lazima kutakuwa na mabadiliko, unaweza kushangaa mwenye mabao saba leo akamaliza na 15 au zaidi, inategemea.

Pia hapa tunaweza kupima kuwa wageni wamekuwa kipimo cha mabadiliko au kujituma kwa wazawa kwa kiasi kipi? Wanasaidia au hakuna lolote? Pia tunaweza kuangalia, kiwango bora cha wageni kama kilionekana, kimesaidia kuwaamsha wenyeji na kimekuwa chachu ya mabadiliko kwao? Hapa tutakuwa tunazungumzia suala la ufungaji.

Upande wa asisti, yaani wataalamu wa kutengeneza basi za mwisho za mabao, unaona walionazo nyingi, kuna wageni na Cleotus Chama raia wa Zambia ana nane, ni wachache wanaoweza kumkaribia au kuwa sawa naye kama Lucas Kikoti wa Namungo FC.

Wakati ligi ikiisha, tutaona. Wenyeji walikuwa na mchango upi katika kitengo hiki cha uzalishaji mabao halafu tutaangalia kwa wageni pia na mchango wao ulivyokuwa katika timu zao.

Lengo litakuwa ni kuangalia ubora wa wageni kama umekuwa chachu ya mabadiliko. Ninaamini mwenyeji yeyote anajua kama atajituma na kufanya vema mbele ya wenyeji na wageni, thamani yake itakuwa kubwa.

Mfano, katika safu ya ulinzi tumeona, Bakari Nondo Mwamnyeto licha ya kuwepo kwa wachezaji wengi wa kigeni katika nafasi yake, yeye ameendelea kuwa gumzo katika usajili ujao.

Mwamnyeto anaonekana ndiye beki gumzo zaidi unapozungumzia usajili kwa ajili ya msimu ujao wa 2020/21.

Nondo anaweza kuwa sehemu ya tathmini kwamba wageni wamechangia nini kwake. Hasa washambulizi au viungo washambulizi, walifanya kipi yeye kuwa bora au anaona wachezaji wazawa tu wangechangia kumfikisha alipo?

Mechi hizi zilizobaki, halafu tukijumlisha na zile ambazo tayari zimeshajenga takwimu, zitatusaidia kupata majibu na ninaona huu ni wakati mzuri kwa kuwa tuna nafasi ya kutathmini huku tukiiangalia ligi yenyewe.

Wakati wengine tutapata maoni kupitia takwimu, kuzungumza na wachezaji hapo baadaye, sasa tukiwa tunafuatilia mechi tutakuwa na nafasi ya kuona je, wageni kwa idadi yao, wanastahili kubaki wachezaji 10?

Kikubwa wakati tunafanya tathmini, tuweke katika mioyo yetu kuwa hii tunafanya kwa ajili ya mpira wetu na nchi yetu. Kusiwe na majibu ya mfukoni, kusiwe na matakwa binafsi, kusiwe na kutaka kuonyesha au kushindana kutaka kuonyesha ukubwa na kadhalika.

SOMA NA HII  LAMINE MORO AONGEZA MKATABA YANGA