Home Uncategorized HIVI NDIVYO BAO LA MORRISON LILIVYOTINGA BUNGENI

HIVI NDIVYO BAO LA MORRISON LILIVYOTINGA BUNGENI


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Juni 12, 2020 katika kufungia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka 2020-2021 alikumbusha bao la Bernard Morrison dhidi ya Simba katika mechi ya watani wa Jadi
Dk Mpango alikumbushia bao, huku akiwapiga kijembe kimtindo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndungai na Naibu wake, Dk Tulia Ackson wakati akimwagia sifa Rais Dk John Magufuli na kulikumbushia bao hilo lililowalaza njaa Simba katika pambano la watani lililopigwa Machi 8 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
“Mheshimiwa Spika, mwisho, japo si kwa umuhimu Rais wetu ni mkakamavu na mpezni wa maendeleo ya michezo nchini,” alisema Dk Mpango na kuongeza kwenye kufungia hotuba yake kwa kusema; “Mnamfahamu katika ubora wake, mazoezi ya push-ups anazopiga usiige! Mtamkumbuka pia jinsi alivyowaalika Ikulu Dar es Salaam vijana wetu wa timu ya taifa wenye umri chini ya Miaka 17 na makocha wao ili kuwajengea ari ya utaifa na kushinda.
Aidha, naamini hamjasahau siku Mhe. Magufuli alipokwenda Uwanja wa Taifa, kujiionea mpambano wa watani wa jadi, Yanga na Simba na kushuhudia mnyama akipigwa mkuki mmoja wa sumu kali na Bernard Morrison!
Inaonekana Mheshimiwa Waziri Mkuu, na wewe Mheshimiwa Spika na hata Mheshimiwa Naibu Spika machale yaliwacheza mapema siku hiyo hamkuonekana uwanjani,” alisema Waziri Mpango.
Kauli hiyo iliamsha shangwe kwa wabunge, wengine wakipasa sauti wakitaka arudie kauli, kabla ya Spika Ndugai kuwataka wabunge watulie ili Dk Mpango amalizie hotuba yake ya bajeti.
Waziri Mkuu, Majaliwa, Spika Ndugai na Naibu Spika wanafahamika ni miongoni mwa vigogo wanaoishabikia Simba, watetezi wa Ligi Kuu Bara ambao msimu huu wamekwama kuzoa alama za kutosha kwa watani wao, baada ya kuambulia alama moja tu katika mechi zote mbili.
SOMA NA HII  MECHI KALI ZA NIYONZIMA ALIPOKUWA SIMBA HIZI HAPA