Home Uncategorized KUHUSIANA NA TAIRONE, FRAGA, SIMBA WASISUBIRI HADI SIKUKUU

KUHUSIANA NA TAIRONE, FRAGA, SIMBA WASISUBIRI HADI SIKUKUU

Na Saleh Ally
SIMBA ilianza kuachana na mshambuliaji Wilker Henrique da Silva raia wa Brazil baada ya kukumbwa na majeraha akiwa kambini nchini Afrika Kusini.

Wakati wa maandalizi ya awali ya msimu, Simba ilikuwa katika maandalizi ya msimu nchini Afrika Kusini na Wilker akaonyesha kiwango bora kabisa. Mwisho alipoumia, ikachukua muda mrefu kurejea hadi ilipochukua uamuzi wa kumalizana naye.

Awali ilimpeleka kwa mkopo na baada ya hapo, wiki iliyopita alirejea nchini baada ya kumaliza mkopo wake wa miezi sita lakini amepata timu, yeye na Simba wamemalizana vizuri, kila mmoja kachukua time yake.

Sasa ni imebaki na wachezaji wawili raia wa Brazil ambao ni mabeki na viungo na wote bila ya ubishi wana uwezo wa kuisaidia Simba. Hawa ni Tairone Santos na Gerson Fraga.

Ajabu, unaweza kuona kuwa hata kuwepo kwao Wabrazili hao hakuna faida kubwa kama ambavyo unavyoweza kutarajia kwamba kutokana na kuwa na wachezaji hao, Simba inapaswa kujivunia na kuwatumia ipasavyo.

Nakumbuka niliwahi kukutana na mdau mmoja wa Simba, nikamuuliza vipi wachezaji hao hawatumiki sana. Jibu liliendana na vipande, kwanza inaonekana hawajazoea mazingira ya Tanzania. Pili, walisajiliwa kwa ajili ya michuano ya kimataifa.

Ukimsikiliza vizuri mdau huyo unapata picha halisi, ni sawa na kuwa na mtu ambaye anatembea peku halafu ana viatu vizuri amevihifadhi ndani akisubiri kuvivaa siku ya sikukuu.
Ukiangalia Fraga, bila shaka sote tumemuona, ana uwezo wa kucheza namba nne, sita na zote alizicheza kwa ufasaha mkubwa na kuwavutia watu wengi.

Kama hiyo haitoshi, juzi tumeona akicheza namba nane na kufanya vizuri, ameiongoza Simba kuitwanga Mwadui FC kwa idadi ya mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Wakati Simba inaamua kumtumia Fraga ilikuwa ni baada ya kushindwa kupata katika mechi yake ya kwanza baada ya Ligi Kuu Bara kurejea kutoka katika mapumziko ya Virusi vya Corona.

Sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting unaona kabisa kuwa iliwachanganya Simba na siku wanapata sare hiyo, tatizo lilikuwa ni safu ya kiungo kwa kuwa Muzamiru Yassin hakuwa vizuri. Kumbuka Jonas Mkude anayetegemewa kucheza katika nafasi hiyo ni majeruhi lakini Mzamiru pia alikuwa anatokea katika majeruhi na mechi ilimshinda.

Tena inawezekana kabisa angeweza kutolewa mapema lakini haikuwa hivyo na badala yake alitolewa baadaye sana na unaona hata mabadiliko yanayofanyika si yake kwa ajili ya kukisaidia kiungo cha ukabaji.

Fraga na Tairone wangeweza kuwa msaada lakini Simba ilikuwa inasubiri hadi siku ya sikukuu. Unaweza kujiuliza vipi wamesajiliwa na tatizo ni lipi hasa hadi kunakuwa na uoga wa kuwatumia! Zile hisia za wageni, zimepitwa na wakati, kusema wamesajiliwa kwa ajili ya michuano ya kimataifa, ni upuuzi mkubwa zaidi ya ule wa kwanza. Watakuwa vipi fiti kama hawapati ‘match fitness’ ya kutosha!

Ukiangalia katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting, Simba hawakuwa wakiruka katika suala la upigaji vichwa. Tairone ni mrefu na ana uwezo mkubwa wa kufanya hivyo, yupo lakini Simba inaendelea kusubiri sikukuu.

Viongozi wa Simba wanapaswa kujiamini kutokana na wanachokifanya na kama kuna kamati ya ufundi, pia iwe na nafasi ya kumshauri kocha ambaye mara kadhaa amewapanga Wabrazili hao wakafanya vizuri na ajabu mechi iliyofuata hawakucheza.

Dar es Salaam kutokana na kuwa na viwanja vingi vyenye ubora, huwezi ukasema watashindwa kucheza. Hata hivyo lazima kujikumbusha si kweli kila kiwanja cha Brazil ni nyasi zenye utelezi, kuna sehemu wanavyo kama vya kwetu.

Kusajili wachezaji bora lazima kuwe na faida, hivyo kocha Simba atoe nafasi kwa kina Fraga na Tairone waonyeshe walichonacho ambacho mara kadhaa wamecheza na kimekuwa msaada kwa kikosi hicho.

Ukiwaona wanacheza, hata kama wanakosea lakini kuna mambo mengi sana ya kujifunza kutoka kwao kutokana na ubora wa kazi zao ambazo zina utofauti na aina ya uchezaji wa wachezaji wetu.

Simba inawagharimia, basi kuwe na nafasi na kwao kuweza kuilipa klabu hiyo ili isione ilipata hasara bure wakati wahusika wana uwezo wa kufanya makubwa na kuwa msaada kama wataaminiwa.

Wakati mwingine, mtu hawezi kufanya kila kitu kila wakati. Kuna kufanya kwa kiwango cha juu au cha chini lakini mwenye ubora hafichiki.
SOMA NA HII  POLISI TANZANIA YAPANIA KUPAMBANA TPL