Home Uncategorized NENDA BABA MKAPA, DAIMA TUTAKUKUMBUKA, UMEACHA ALAMA KUBWA

NENDA BABA MKAPA, DAIMA TUTAKUKUMBUKA, UMEACHA ALAMA KUBWA

Habari za Michezo

USIKU wa kuamkia jana Ijumaa, taifa lilipata msiba mzito, hiyo ni baada ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa kuaga dunia.

Rais Mkapa aliingia madarakani mwaka 1995 ambapo alidumu hadi mwaka 2005 kisha akamuachia kijiti Dk. Jakaya Kikwete.
Enzi za utawala wake, Mkapa alifanya mambo makubwa kwenye sekta ya michezo kati ya vingi alivyovifanya katika kuhakikisha michezo inasonga mbele ni pamoja na:-
UWANJA WA TAIFA

 Moja ya jambo la kukumbukwa ambalo Rais Mkapa ametuachia ni ujenzi wa uwanja mkubwa wa kisasa ambao ni kati ya viwanja bora Afrika.


Ujenzi wa uwanja huu ulianza rasmi mwaka 2005 na kukamilika 2007 huku gharama zake zikiwa ni dola Mil 56 (sawa na Sh Bil 129.3) na unabeba watu 60,000.

Wazo la kujengwa kwa uwanja huu lilikuja baada ya Rais Mkapa kusema kwenye moja ya hotuba zake kwamba: “Nasikia fedheha ninapokwenda mataifa ya wenzetu na kukuta viwanja bora lakini nikiangalia uwanja wetu napata fedheha, nitahakikisha kabla sijaondoka madarakani nawaachia uwanja wa kisasa.”
Sasa uwanja huu ni kati ya vile viwanja ambavyo vimetumika kwenye michezo mikubwa huku mastaa wa kigeni kama Samuel Eto’o, Didier Drogba, Mohamed Salah na wengine wengi wakicheza hapo.
KUTATUA MGOGORO WA FAT NA SERIKALI:
Jambo lingine ambalo wanamichezo tutalikumbuka kutoka kwa Rais Mkapa ni kutatua mgogoro ulioibuka kati ya Serikali na Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF) mwaka 1993 jambo lililosababisha Tanzania kupokonywa uanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutokana na Serikali kuingilia masuala ya michezo ambayo ni kinyume na kanuni za Fifa.

Rais Mkapa aliwatuma mawaziri wa enzi hizo, Profesa Mikol Sarungi na Anna Abdallah na wakakutana na uongozi wa FAT chini ya Katibu Mkuu, Ismail Aden Rage na wakamaliza tofauti zao hatimaye Tanzania ikarudishiwa uanachama wa Fifa.

KUTOA NDEGE NA NAULI KWA SAFARI ZA TIMU YA TAIFA

Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Mkapa ilifanya juhudi za kila namna kuhakikisha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inasafiri bila kikwazo chochote kwenye mashindano na michezo mbalimbali ya nje ya nchi, ambapo Serikali ya awamu ya tatu ilikuwa inatoa nauli na hata usafiri wa ndege kwa timu ya taifa ili iweze kushiriki michuano ya kimataifa.
MAGEUZI MAKUBWA KWENYE SEKTA YA MICHEZO:
Serikali ya awamu ya tatu ilifanya jitihada za dhati katika kuinua sekta ya michezo mbalimbali hapa nchini ikiwemo riadha na mingine jambo ambalo liliifanya Serikali hiyo chini ya Rais Mkapa kuacha alama kubwa kwenye ulimwengu wa michezo nchini.Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya mpendwa wetu amen.
SOMA NA HII  BARCELONA HAWAPOI, WAKIMKOSA LAUTARO BASI MBADALA WAKE NI ISAK