Home Uncategorized YANGA YAINGIA ANGA ZA BEKI ANAYEKIPIGA ZAMBIA, AKUBALI KUTUA MAZIMA

YANGA YAINGIA ANGA ZA BEKI ANAYEKIPIGA ZAMBIA, AKUBALI KUTUA MAZIMA


JINA la beki wa pembeni Mtanzania anayekipiga Klabu ya Nkana ya nchini Zambia, Hassan Kessy, limejadiliwa na Kamati ya Usajili ya Yanga na kukabidhiwa kwa Kocha Mkuu Mbelgiji, Luc Eymael huku Kessy mwenyewe akisisitiza kuwa yupo tayari kujiunga Yanga.
Kessy ni kati ya wachezaji wanaotajwa hivi sasa kuwaniwa na Yanga katika kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo imepanga kukisuka kikosi chao ili kichukue makombe.
Beki huyo ni mchezaji huru hivi sasa kwa mujibu wa kanuni za Fifa kutokana na mkataba wake kumalizika Agosti, mwaka huu, hivyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu nyingine itakayomhitaji.
Taarifa zinaeleza kuwa Yanga inataka kumsajili beki huyo kwa ajili ya kuiboresha safu hiyo ya beki ya pembeni inayochezwa hivi sasa na Juma Abdul na Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kocha ndiye aliyependekeza usajili wa beki wa pembeni katika kuiboresha na Kessy ndiye aliyependekezwa na baadhi ya viongozi wa Yanga.
Aliongeza kuwa jina la Kessy tayari limekabidhiwa kwa kocha ambaye yeye ataamua asajiliwe au vipi, hivyo kama akikubali basi haraka atapewa mkataba wa miaka miwili.
“Kessy ndiyo jina la kwanza la beki wa kulia lililopendekezwa na mabosi wa Yanga ambao tayari wamempatia kocha ambaye yeye ndiye atakayeamua hatima yake.
“Kocha anamtaka beki mwenye uwezo na uzoefu wa kucheza michuano ya kitaifa na kimataifa, hivyo upo uwezekano mkubwa wa Kessy kusajiliwa na Yanga,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Kessy kuzungumzia hilo alisema: “Mimi mkataba wangu unatarajiwa kumalizika mwezi Agosti, hivyo nipo tayari kujiunga nayo kwani nimepata taarifa za kunihitaji, lakini bado hawajanifuata kiofisi.”
SOMA NA HII  MABOSI MANCHESTER CITY WAKUBALIANA KUMPA NAMBA MPYA NYOTA WAO MPYA