Home Uncategorized YANGA YAJA NA MIFUMO MITATU YA KAZI

YANGA YAJA NA MIFUMO MITATU YA KAZI


 KOCHA Mkuu wa Yanga, Mserbia, Zlatko Krmpotic, amepata dawa ya timu jeuri baada ya kuongeza mifumo miwili ya uchezaji ili kuhakikisha anapata ushindi katika michezo yao inayofuata ya Ligi Kuu Bara.

 

Hiyo ni baada ya kupata ushindi wao wa kwanza kwa mbinde katika mchezo wao wa pili wa ligi uliopigwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es , ambao ulimalizika kwa Yanga kuifunga Mbeya City bao 1-0 lililofungwa na Mghana, Lamine Moro dakika ya 87.

 

Kocha huyo, awali alianza kibarua cha kukinoa kikosi hicho akitumia mfumo wa 4-4-2, kabla ya kuongeza miwili ya 4-5-1 na baadaye kuongeza wa 4-3-3 akiwatumia washambuliaji watatu katika kutafuta ushindi wa kwanza.


Mserbia huyo katika dakika ya 60 za mchezo, ndiyo alionekana kubadili mifumo kwa kumuingiza Muangola, Carlos Fernandez ‘Carlinhos’ ambaye alionekana kubadili mchezo na baadaye kuwaingiza washambuliaji wawili kwa mpigo, Yacouba Songne na Ditram Nchimbi.

 

Kuingia kwa Yacouba na Nchimbi kulibadili mfumo kutoka 4-4-2 na kuwa 4-3-3, akiwatumia washambuliaji watatu waliocheza pamoja na Mghana Michael Sarpong na kuongeza mashambulizi kwenye goli la Mbeya City na kufanikiwa kupata ushindi huo.

 

Katika kipindi cha kwanza, kocha huyo alionekana kuwatumia viungo wengi kwa kutumia mfumo wa 4-5-1 akimtumia mshambuliaji mmoja pekee ambaye ni Sarpong, huku viungo wakiwa ni Haruna Niyonzima, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mukoko Tonombe, Deus Kaseke na Tuisila Kisinda.


Kocha huyo mara baada ya kubadili mfumo huo kwa kumuingiza Carlinhos, kulimzuia Sarpong kuufuata mpira nyuma na badala yake muda wote kuonekana katika eneo la goli la wapinzani kwa ajili ya kutafuta bao.

 

Mara baada ya mchezo huo, kumalizika, Krmpotic alisema kuwa: “Nilibadili mifumo hiyo ya uchezaji kwa kuchezesha 4-3-3 kwa maana ya kuwachezesha washambuliaji watatu kwa ajili ya kuongeza mashambulizi kwenye goli la wapinzani baada ya kuwaona Mbeya City wakikaa nyuma golini kwao kumi, mfumo huo ulitupa matokeo mazuri ya ushindi huu wa bao 1-0.”

SOMA NA HII  SABABU YA BERNARD MORRISON KUACHWA BONGO IPO HIVI