Home Uncategorized SIMBA V KAGERA LEO NI NGOMA NZITO UHURU, MITAMBO YA MABAO HII...

SIMBA V KAGERA LEO NI NGOMA NZITO UHURU, MITAMBO YA MABAO HII HAPA

 


HATUMWI mtoto dukani lazima dakika 90 ziamue nani mbabe ndani ya uwanja hasa kwa hawa wanaume wanapokutana ndani ya uwanja.

Simba ikiwa na presha ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara inawakaribisha Kagera Sugar ambao presha yao ni kujinusuru kwenye mstari wa kushuka daraja hapo lazima ngoma ya kitoto isikeshe.

Cheki namna balaa litakavyokuwa Uwanja wa Uhuru kwa timu hizi kusaka pointi tatu:-

Simba presha tupu

Mabingwa watetezi Simba kwa sasa ipo kwenye presha kubwa hasa kutokana na kupoteza mechi zake mbili mfululizo jambo ambalo linawapasua kichwa kwa sasa ukizingatia kwamba Novemba 7 inakutana na muziki wa Yanga ambayo ipo kwenye kasi yake.

 

Tatizo kwa Kagera Sugar

Safu ya ulinzi inayoongozwa na Ally Mtoni,’Sonso’ na David Luhende ndani ya mechi 9 ambazo ni dakika 810  imeruhusu mabao 11. Ina wastani wa kuokota bao kila baada ya dakika 73.

 Inakutana na safu ya Simba inayoongozwa na Joash Onyango ikiwa imefungwa mabao manne ndani ya mechi 8 ambazo ni dakika 720 ikiwa na wastani wa kuokota bao kila baada ya dakika 180.


Wachezaji wenye matokeo mguuni

Nahodha wa Simba, John Bocco akiwa kwenye ubora wake ni ngumu kuzuilika.Ni mzawa wa kwanza kufunga zaidi ya mabao 100 ndani ya ligi. Tayari gari limewaka ametupia mabao matatu ndani ya ligi.

Clatous Chama ni mtambo kwa Simba, mechi mbili ambazo hakuwepo mabingwa watetezi walipata tatu mbele ya wajeda kwa kunyooshwa na Tanzania Prisons kisha wakaambulia kichapo mbele ya Ruvu Shooting zote ikiwa ni bao 1-0.

Amerejea mbele ya Mwadui FC Simba ikashinda mabao 5-0 huku yeye akitoa pasi moja na kumfanya afikishe jumla ya pasi nne na mabao mawili ndani ya ligi msimu wa 2020/21.

Kwa Kagera Sugar kijana mzawa, Yusuph Mhilu gari limewaka tayari, kibindoni ana jumla ya mabao manne akiwa kwenye orodha ya wazawa wenye mabao mengi ndani ya ligi.

Hawa hapa kwa Kagera Sugar:-

Rekodi zinaonyesha akishawasha moto kuzimika huwa ni baada ya mechi tatu kama ambavyo alianza kutupia kwa msimu wa 2020/21. Alianza mbele ya KMC kisha aliwatungua Azam FC na bao lake la tatu aliwatungua Namungo. Alikwama mbele ya Mbeya City na Dodoma Jiji.

SOMA NA HII  MTUPIAJI WA NAMUNGO AFUNGUKIA USAJILI WAKE YANGA

David Luhende huyu ni beki mkali wa mipira iliyokufa ana bao moja kibindoni alimtungua kipa namba moja wa Azam FC, David Kissu na ana pasi moja ya bao.

Dakika zao 540 zilikuwa moto

Ndani ya misimu mitatu hakuna timu ambayo wamekutana uwanjani hakuna sare iliyopatikana zaidi ya ushindi.Kwenye mechi sita ambazo wamekutana uwanjani ambazo ni dakika 540, Simba imeshinda mechi nne huku Kagera Sugar ikishinda mechi mbili.

Jumla yamepatikana mabao 11 ikiwa ni wastani wa kila dakika 49 timu hizi kushuhudia bao likiokotwa wavuni. Simba ilifunga mabao saba na Kagera Sugar ilifunga jumla ya mabao 4.

Matokeo yao haya hapa:-2017/18, Kagera Sugar 0-2 Simba. Simba 0-1 Kagera Sugar. 2018/18 Kagera Sugar 2-1 Simba, Simba 0-1 Kagera Sugar. 2019/20, Kagera Sugar 0-3 Simba, Simba 1-0 Kagera Sugar.

 

Kitakachovutia

Timu zote mbili mechi zao mbili za ligi hakuna ambayo iliambulia ushindi, Kagera Sugar ikiwa inasaka pointi sita iliambulia pointi moja huku Simba wao wakipoteza pointi sita zote.

Kagera Sugar ililazimisha sare ya bila kufungana na Dodoma Jiji kisha ikakubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City. Zote ikiwa Uwanja wa Kaitaba.

Simba ilichezeshwa ligwaride na Tanzania Prisons Uwanja wa Nelson Mandela na kupapaswa na Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru mechi zote ilikuwa ni mwendo wa 1-0.

Kitakachoongeza mvuto zaidi ni kwamba mechi zao zilizopita wote wamesepa na pointi tatu wakiwa nyumbani, Kagera Sugar ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba ilishinda mabao 5-0 dhidi ya Mwadui FC, Uwanja wa Uhuru.

Mwendo wao kwenye ligi

Simba imecheza jumla ya mechi nane, imeshinda mechi tano, imechapwa mechi mbili na sare moja ikiwa na pointi 16 kibindoni nafasi ya tatu.

Kagera Sugar imecheza mechi  9 imeshinda mechi mbili, sare mbili amepoteza mechi tano na pointi zake kibindoni ni nane nafasi ya 16.

 

Neno la Sven

Sven Vandenbroeck, Kocha Mkuu wa Simba alisema:”Kila mchezo kwetu tunachoangalia ni kuona namna gani tutapata pointi tatu, ushindani ni mkubwa nasi ni lazima tushindane.”

Neno la Mecky

Mecky Maxime, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar alisema:”Kila mchezo una mbinu zake, kwangu mimi ninaweza kuwaambia mashabiki kwamba wajitokeze kuona burudani.”

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here