Home Uncategorized SENZO AFUNGUKA A-Z KUHUSU SAKATA LA KICHUYA FIFA..AMTAJA KIGOGO WA SIMBA ALIYEHUSIKA

SENZO AFUNGUKA A-Z KUHUSU SAKATA LA KICHUYA FIFA..AMTAJA KIGOGO WA SIMBA ALIYEHUSIKA


WAKATI mashabiki wa soka wakiwa bado kwenye sintofahamu juu ya sakata la winga Shiza Kichuya aliyefungiwa miezi sita na klabu yake ya zamani, Simba nayo kutozwa faini ya Sh 294 milioni, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amefichua mchongo mzima.

Senzo amevunja ukimya zikiwa zimepita siku kadhaa tangu sakata hilo lilivyoibuka, huku mabosi wa Msimbazi wakimtupia mpira wakidai aliyedili na usajili huyo ni Mshauri Mkuu huyo wa sasa wa Yanga na kushangaa sakata lilivyo wakati hadi ITC ya mchezaji ilipatikana ili acheze Simba.

Viongozi wenye ushawishi ndani ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Mulamu Nghambi ndio waliokaririwa wakisema suala la Kichuya kufungiwa wao wanalishangaa kwani walipoomba ITC ya mchezaji huyo walipewa na ndio maana akacheza.

Mabosi hao pia walikata kulisema kwa undani kwa madai hawaelewi chochote kilichotokea kwani wakati huo Mtendaji Mkuu wa klabu yao alikuwa ni Senzo aliyehamia Yanga kwa sasa, ndipo Mwanaspoti likaamua kumsaka Mshauri huyo wa Yanga, naye akaamua kuanika anachokijua.

Awali Mwanaspoti lilimtafuta Senzo kwa mara ya kwanza baada ya klubumburuka kwa sakata hilo, lakini ilishindikana kutokana na bosi huyo kuwa safarini kwenda Shinyanga akiwa na timu yao kwa mchezo uliopigwa Jumamosi dhidi ya Mwadui katika mfululizo wa Ligi Kuu Bara.

SENZO HUYU HAPA

Hata hivyo, juzi kabla ya mechi hiyo, alipotafutwa tena alipatikana kwa njia ya simu na kuweka wazi kila kitu kinachohusiana na suala zima la Kichuya, lililodaiwa na wanene wa Msimbazi kwamba alihusika nalo enzi akiwa klabu kwao.

Senzo alisema suala zima la usajili wa Kichuya lilitokana na Try Again ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kutaka mchezaji huyo asajiliwe, huku kukiwa hakuna mahitaji ya winga kwa wakati huo.

“Hakukuwa na mahitaji ya winga kwa wakati ule, lakini alilazimisha na mchezaji akasajiliwa, wote tulikuwa tunajua kwamba kocha hahitaji winga kwa wakati ule,” alisema Senzo raia wa Afrika Kusini na kufichua, Simba ilianza kumtaka Kichuya kwa mkopo na kutuma maombi klabu yake (yaani Pharco FC), lakini kilichotokea mkopo huo ulichelewa kujibiwa na Wamisri hao.

“Kichuya anasimamiwa na Wakala anayejiita Savas, wakala huyo ndiye alitumika kwenda Pharco na huyo ndiye aliyemtoa Simba na kumpeleka Misri, siri kubwa ya mkopo kuchelewa ilitokana na mchezaji pamoja na msimamizi wake kudai kwamba Pharco wamevunja mkataba wao.”

“Nilimpigia simu mwakilishi wa klabu na aliniambia kabisa kwamba mchezaji hajavunjiwa mkataba, licha ya Kichuya kusisitiza kuwa, amevunjiwa mkataba,” alifafanua Senzo.

Senzo alisema hawakuishia hapo kwani waliamua kwenda FIFA na huko ndiko waliruhusiwa kumtumia mchezaji huyo na kweli walipata ITC ambayo ilimruhusu mchezaji kucheza.

“Baada ya Simba kumpata Kichuya, Pharco walienda kufungua mashtaka FIFA kwamba mchezaji ameondoka na pesa kisha kaenda timu nyingine huku akiwa sio mchezaji huru, Simba waliandikiwa barua, lakini hawakuwa wakiifuatilia tatizo lilianzia hapo.”

SOMA NA HII  MANCHESTER UNITED YAKUBALI YAISHE KWA POGBA

Aliongeza kwa kusema FIFA waliwatumia barua pepe za klabu pamoja na yake ambayo anaweza kuingia mtu yeyote wa klabu hiyo.

“Hizo ni akaunti maalum kwa klabu nami baada tu ya kuondoka walizifunga, chochote wanachokihitaji kwenye barua pepe yangu wanaweza kukiona,” alisema Senzo na kudai kushangaa kutupiwa mpira wakati jambo lilikuwa wazi hata kwa viongozi wote wa Simba.

Mwanaspoti linafahamu, Simba ilitumiwa barua ya kwanza Julai 6, 2020 wakiombwa kutoa maelezo juu ya mchezaji huyo lakini hawakujibu chochote.

Julai 29, 2020 walikumbushwa tena kwa barua pepe, huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwanasheria wa Simba, Michael Mhina nao wakitumiwa nakala ambapo Simba walipewa muda wa siku nne kujibu tuhuma hizo pamoja na maelezo ya mchezaji.

Baada ya Julai 29, 2020 kutumwa barua hiyo, siku tisa mbele Senzo alijiuzuru katika klabu hiyo na kujiunga na Yanga.

Mwanaspoti lilimbana kuhusu kuondoka kwake, alisema kwa upande wake alikuwa akijitahidi kumaliza tatizo hilo kwa kufuata ushauri mpaka wa wanasheria wa nje, lakini hakuwa akipewa ushirikiano.

“Niliomba ushauri kutoka kwa wanasheria wa nyumbani Afrika Kusini, nikatumiwa barua pepe ambayo hata Mwanasheria wa klabu ya Simba alikopiwa, kiukweli sikuona sehemu yoyote Simba walitaka kujibu, kwani FIFA wao walikuwa wanataka jibu tu lakini haikuwa hivyo,” alisema Senzo na kuongeza; “Kwa sasa sula hilo halinihusu, kwani nipo sehemu nyingine na naendelea na kazi yangu.”

SAKATA LENYEWE

Mapema wiki iliyopita ilitolewa taarifa kwamba FIFA kupitia Kamati ya Usuluhishi na Migogoro ilitoa hukumu kwa Simba kuitaka iliipe Pharco Sh 294 milioni ndani ya siku 45 kuanzia Novemba 24, 2020 ilipotolewa hukumu hiyo, huku Kichuya naye akifungiwa kucheza miezi sita.

Kichuya aliyesajiliwa Simba misimu minne iliyopita aliuzwa Pharco FC iliyopo Daraja la Pili mapema mwaka jana kwa mkataba wa miaka minne, kisha klabu hiyo ikampeleka kwa mkopo ENPPI iliyopo Ligi Kuu aliyoichezea kwa nusu msimu kabla ya kumrejesha tena Pharco.

Mabosi wa Pharco inadaiwa walikuwa wakijiandaa kumtoa tena kwa mkopo kwa kukosa kwake nafasi kikosini, kitendo kilichomfanya Kichuya aamua kurejea Msimbazi kwenye dirisha dogo la msimu uliopita kabla ya kusajiliwa Namungo ikiwa ni mchezaji huyu na mambo kutibuka FIFA.

Katika hukumu yake, FIFA ilifafanua iwapo Simba itashindwa kulipa fedha hizo itafungiwa kusajili kwa miaka miwili na ikilipa basi Kichuya ataruhusiwa kucheza bila kutumikia adhabu hiyo.

Mabosi wa Simba mapema walisema watakutana siku yoyote ili kujadili suala hilo, kisha watalitolea ufafanuzi na kauli kwa umma.

Credit – Mwanaspoti