Home Uncategorized YANGA RUKSA KUSEPA NA MSHAMBULIAJI HUYU WA GHANA

YANGA RUKSA KUSEPA NA MSHAMBULIAJI HUYU WA GHANA


 UONGOZI wa Namungo umefunguka kuwa, utakuwa tayari kumuachia mshambuliaji wao raia wa Ghana, Steven Sey katika kipindi cha dirisha dogo kwa klabu yoyote ambayo itamuhitaji na kufikia mwafaka mzuri.

 

Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga, ni miongoni mwa timu ambazo zinatajwa  kuwa kwenye mpango wa kumsajili nyota huyo ili kuimarisha safu yao ya ushambuliaji ambayo inaonekana kuwa butu kwa sasa.

 

Safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na Michael Sarpong, katika Ligi Kuu Bara imefunga mabao sita kati ya 17 yaliyofungwa na timu hiyo, huku Sarpong akiwa nayo manne.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Mwenyekiti wa Namungo, Hassan Zidadu, amesema licha ya Sey kuwa na mkataba wa miaka miwili ndani ya klabu hiyo, lakini wapo tayari kumuachia kwa timu ambayo itaweka mezani dau nono.

 

“Tumesikia hizo taarifa za baadhi ya klabu kuhitaji huduma ya Steven Sey, lakini mpaka sasa hakuna klabu yoyote ambayo imekuja mezani kwa ajili ya mazungumzo ya kufanya biashara ya uhamisho huo, lakini hata mchezaji mwenyewe hajatuambia kama amepata ofa yoyote.

 

“Lakini ningependa pia kuweka wazi kwamba bado tuna mkataba wa miaka miwili na mchezaji husika lakini hilo halizuii biashara kufanyika.


“Hivyo kama kuna timu itaonesha uhitaji wa huduma yake tunawakaribisha mezani na tutakuwa tayari kumuachia Sey kama tu klabu itakayomuhitaji italeta ofa inayoeleweka na kufuata taratibu stahiki za usajili,” alisema Zidadu.


Sey ana mabao mawili kwenye Kombe la Shirikisho ambayo alifunga kwenye mchezo wa awali dhidi ya Al Rabita ya Sudan Kusini.


Mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Azam Complex na Namungo ilishinda mabao 3-0 na kutinga hatua inayofuata baada ya CAF kufuta mchezo wa marudinao kutokana na wapinzani wao kushindwa kutimiza masharti kuhusu waamuzi.

SOMA NA HII  SINGIDA UNITED YAIPA SOMO LA KUTOSHA DODOMA FC