Home Uncategorized MABOSI WA YANGA HUENDA ‘WANAUMA MENO’ DILI LA DICKSON JOB KWA UWEZO...

MABOSI WA YANGA HUENDA ‘WANAUMA MENO’ DILI LA DICKSON JOB KWA UWEZO WA NINJA

 


BAADA ya muda mrefu wa kusubiri, hatimae timu ya wananchi Yanga wamefungua tena kabati lao la makombe. Mara ya mwisho Yanga wametwaa kombe ni lini? Miaka sasa imepita.

 

 Kabla hata hawajamsajili Papy Tshishimbi. Sasa hivi ameondoka na yupo zake kwao. Safari hii wanalifungua kabati lao kwa furaha zaidi kwa sababu wametwaa kombe kwa kuwalaza watani zao na wapinzani wao wa karibu, Simba.

 

 Hakuna furaha inayozidi kumfunga mtani Tanzania. Hata furaha ya kutwaa ubingwa haipendezi kama ya kumfunga mtani. Mara nyingine hata kukosa ubingwa haujali kama umemfunga mtani.

 

 Sijui hii nadharia alituachia nani. Sijui huu utaratibu ulitoka wapi. Kama wewe unafahamu niandikie sababu.

 

Kama ilivokuwa kwa Simba, Yanga wanachukua hili taji bila ya uwepo wa wachezaji wao wengi wa kikosi cha kwanza. Bakari Nondo Mwamnyeto, Lamine Moro, Yassin Mustapha na Feisal Salum ni baadhi ya mastaa wa Yanga ambao hawakuwepo Zanzibar.


 Kukosekana kwao kulitokana na sababu mbalimbali, wengi wakiwa katika majukumu ya timu ya taifa, wengine walipewa likizo kama Lamine Moro.

 

 Hakukuwa na sababu ya kwenda na wachezaji wa kikosi cha kwanza kupambania milioni 15. Hii pesa hata hailipi mshahara wa wachezaji watano wa Simba au Yanga. Ingekua labda bingwa anachukua kitita kinachotosha walau kujiendesha kwa mwezi mmoja.

 

 Simba isingekubali kuwaachia akina Chama na Bwalya waende likizo. Nadhani waandaji wa haya mashindano wanaweza kufikiria namna ya kuyaongezea thamani zaidi kwa kuongeza zawadi zaidi.

 

Tofauti na thamani, pia tumezidi kuona ukubwa wa tofauti iliyopo kati ya vilabu vya Zanzibar na Bara. Ni wazi kwamba vilabu kutoka bara vipo vizuri zaidi kushinda vilabu vya Zanzibar. Unaweza kutaja sababu nyingi za uwepo wa hii tofauti, lakini sababu kubwa ni moja, uwekezaji.

 

 Unapozungumzia uwezekaji kichwani mwako linakuja neno moja tu. Lipi hilo? Pesa! Na hiyo ndiyo sababu ya tofauti kubwa iliyopo kati ya vilabu vya Zanzibar na bara. Wakati watu wa bara wakikazana kuweka pesa kununua wachezaji na kuendesha vilabu, bado watu wa  visiwani wamebaki nyuma.

SOMA NA HII  SENZO AMJIBU MOO DEWJI, ATAJA MKATABA WA LUIS MIQUISONE SIMBA SC

 

Sijui ni kwasababu gani hasa ukizingatia Zanzibar wapo matajiri wengi tu. Labda kwa kuwa bado hawaamini kuwa soka ni biashara inayolipa kuliko biashara nyingi sana duniani.

 

Mwisho kabisa naweza kuwazungumzia wachezaji wa Simba na Yanga waliopata nafasi ya kucheza katika kombe la mapinduzi. Kama nilivozungumza hapo awali, wachezaji wengi wa Simba na baadhi wa Yanga waliocheza Zanzibar ni wale wa kikosi cha ziada.

 

Hakuna mashindano mengi Tanzania, yanapotokea mashindano kama haya, ndiyo nafasi ya kuwakumbuka wachezaji wasiopata nafasi mara kwa mara. Kwa mchezaji anayejielewa hutumia nafasi kama hizi kumshawishi mwalimu kuwa anahitaji nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

 

 Nililiona hilo kwa wachezaji wengi wa Simba na Yanga. Walijitoa sana na kujituma sana kuwauliza waalimu kwa nini hawawapi nafasi mara kwa mara. Bado nawaza Cedric Kaze atamuambia nini Abdalah Shaibu Ninja atakapokuwa anamnyima nafasi hata ya benchi.

 

 Kwa aliyoyafanya Zanzibar, hata viongozi waliolazimisha dili la Dickson Job watakuwa wanauma meno wakisema, “Kumbe Ninja angeweza tu kufanya kazi?” Ndivyo inavotakiwa kuwa kwa mchezaji mwenye kiu ya kucheza. Sitaki kumzungumzia Ibrahim Ajib, yeye anajua maisha aliyoyachagua. 


Imeandikwa na Oscar Oscar ipo ndani ya Gazeti la Championi Jumamosi