Home Simba SC KAMA HUU NDIO ‘UBABU’ WA ONYANGO, BASI SIMBA SC IMELAMBA DUME..!!

KAMA HUU NDIO ‘UBABU’ WA ONYANGO, BASI SIMBA SC IMELAMBA DUME..!!


MUONEKANO wa beki wa Simba, Mkenya Joash Onyango ulimfanya mashabiki wampokee kama mchezaji ambaye umri wake upo jioni, jina la babu lilitawala siku za mwanzo, lakini ameamua kujitetea mwenyewe.

Onyango alitaniwa sana kama ilivyokuwa kwa Meddie Kagere aliyetoka naye timu ya Gor Mahia ya Kenya, waliyekuwa wanamuita babu, lakini akajivua jina hilo baada ya kuibuka mfungaji bora misimu miwili mfululizo na akawa straika tishio zaidi Ligi Kuu Bara.

Gazeti la Mwanaspoti linakuchambulia jinsi ambavyo Onyango ameamua kujivua jina la babu kama Kagere kwa kuonyesha uwezo unaozima utani wa wapinzani wao.

ULINZI NA AL AHLY

Onyango anathibitisha ubora wake katika Ligi ya Mabingwa Afrika, akionyesha Simba haikukosea kumsajili kutoka Gor Mahia ya Kenya. Alitumika kwenye kikosi cha kwanza cha kocha aliyeondoka Sven Vandenbroeck na tayari ni tegemeo la kocha mpya, Didier Gomes.

Beki huyu kisiki si mgeni katika michuano ya kimataifa. Ameshakiwasha sana akiwa na timu ya taifa lake la Kenya na klabu aliyotokea ya Gor Mahia.

Onyango alifanya kazi kubwa Simba ilipowashangaza Al Ahly ya Misri kwa kichapo cha bao 1-0 pale kwa Mkapa Jumanne iliyopita. Aliituliza safu ya ulinzi, ali-win mipira ya juu na ya chini na kumhakikishia kipa wao, Aishi ‘Air’ Manula, ulinzi wa uhakika.

Mara nyingi alikuwa anapiga mipira mbele wakati mwingine alikuwa anawapiga chenga washambuliaji wa upinzani, zaidi alifanya ‘tackling’ zenye akili bila ya kucheza faulo akiiba mpira kutokea nyuma ya straika.

Vitu ambavyo ameonyesha tangu ametua nchini, vinatosha kumshawishi kocha yeyote kumtumia katika kikosi chake cha kwanza. Na ndio maana hamna anayemshangaa kocha Mfaransa Gomes kumuamini mwamba huyu katika kikosi chake cha kwanza.

MAKOSA YANGA

Mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga ina presha kubwa kwa wachezaji, mashabiki na viongozi. Onyango ndiye aliyesababisha penalti iliyopigwa na Micheal Sarpong dakika ya 30, baada ya kumshika Tuisila Kisinda alipomshinda mbio.

Kupitwa kwa kasi ya umeme na Tuisila anayeaminika kuwa winga mwenye kasi zaidi nchini, pamoja na staili yake ya kupaka rangi nyeupe ndevu zake alipokuwa kwao Kenya, ukijumlisha na muonekano wake, vilizidisha utani kutoka kwa mahasimu wao Yanga.

SOMA NA HII  HUKO SIMBA NAKO PA MOTO BALAAH....MASHINE HII YA MAGOLI KUTOKA COLOMBIA KUTUA TZ MUDA WOWOTE..

Hata hivyo, Onyango alipunguza kebehi za wapinzani kwa kufunga kwa kichwa bao la ‘usiku’ lililowapa Simba sare ya 1-1 dhdi ya Yanga siku hiyo na kufuatia na kucheza kwa kiwango bora katika mechi za michuano yote ambayo Simba inashiriki.

Aliulizwa swali baada ya mechi hiyo, kwamba anachukuliaje wanavyomuita babu? Alijibu hana shida na majina na ikiwezekana waongeze jingine lakini atawajibu kwa matendo uwanjani.

“Ni mtazamo wao, siwezi kuwazuia kuongea kile wanachojisikia, kazi yangu ni kucheza hivyo wanaweza wakaniita wawezavyo sitahangaika na hilo.”