Home Simba SC KUMBE! WACHEZAJI WAMEMGOMEA MKUDE SIMBA

KUMBE! WACHEZAJI WAMEMGOMEA MKUDE SIMBA


 PAMOJA na kamati ya nidhamu ya Simba kutoa tamko la kumtaka Jonas Mkude kuingia kambini mara baada ya kusikiliza na kuamua juu ya tuhuma zake za utovu wa nidhamu, imebainika wazi kuwa wachezaji wenzake wamemgomea kuingia kambini hadi akose michezo 10.


 Mkude alisimamishwa na uongozi wa Simba,Desemba 28,2020 kwa madai ya kuonyesha tabia ya utovu wa nidhamu, jambo ambalo lilipelekwa kamati ya nidhamu ya klabu hiyo, ambayo inaongozwa na Kamanda Mstaafu wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Selemani Kova, kumpiga adhabu kulipa faini ya Sh mil 1, karipio kali na kuwekwa katika kipindi cha uangalizi cha miezi sita huku ikimtaka aombe radhi.

 

Chanzo chetu kutoka ndani ya kambi ya Simba, kimeeleza  kwamba, wachezaji wa klabu hiyo kwa jumla wamepinga kurejeshwa kambini kwa Jonas Mkude kwa madai ya kuwa hadi amalize adhabu yao waliyompa ya kuwa nje ya kikosi hadi mechi 10 zitakapomalizika.

 

“Mkude kwa sasa hawezi kuingia kambini kutokana na uongozi wa wachezaji kwa jumla kukataa kumruhusu kurejea hadi atakapomaliza kutumikia adhabu yao waliyompa ya kutohusika kwenye mechi 10 za timu.


 “Kauli yao imeleta malalamiko kwa baadhi ya viongozi huku wengine wakijaribu kuwashawishi wachezaji ili wamruhusu kuingia mazoezini, jambo ambalo wamegomea na kuutaka uongozi kama utalazimisha basi hata wao siku wakitenda makosa wasiadhibiwe kwa namna yoyote ile kama Mkude atarejea kambini kabla ya kumaliza kutumikia adhabu yao hiyo,” kilieleza chanzo.

 

Tangu asimamishwe mpaka sasa Mkude amekosa mechi nane ambazo Simba wamecheza za michuano yote hivyo amebakiza michezo miwili kabla ya kurejeshwa rasmi.

SOMA NA HII  PHIRI KAMA UTANI ILA NDO ANAKUJA IVO