Home Ligi Kuu SUALA LA KUBEBA MATOKEO UWANJANI LISIPEWE NAFASI

SUALA LA KUBEBA MATOKEO UWANJANI LISIPEWE NAFASI

 


MASHABIKI wengi kwa sasa ambao wanajitokeza ndani ya uwanja kushuhudia mpira wanabeba matokeo mfukoni.Jambo hili linafanya pale mambo yanapokuwa tofauti waanze kulalamika na kumtafuta mchawi.

Hapa hakuna mchawi ambaye anapaswa kuanza kutafutwa baada ya mchezo hasa pale matokeo yanapokuwa tofauti na vile ambavyo ulikuwa unafikiria.

Ukweli ni kwamba mpira ni dakika 90 na kila timu ambayo inaingia ndani ya uwanja inakuwa imejipanga kupata ushindi kwenye mchezo huo.

Namna ambavyo wapinzani wanakuwa wanatafuta pointi tatu ipo hivyo hata kwa wale wenyeji wa mchezo hivyo kila mmoja ana nafasi ya kushinda ama kupoteza pamoja na kuambulia sare.

Hili siku zote huwa ninaongea hapa kwamba hakuna timu ambayo inauhakika wa kushinda mechi zake zote ndani ya uwanja.

Jambo hili likae kwa mashabiki kwenye na wafuatiliaji wa mpira ambao bado wanaamini kwamba timu zao zina haki ya kushinda wakati wote.

Makosa ambayo yanatokea ndani ya uwanja ni sehemu ya mchezo kwani hakuna ambaye anaweza kufanya kila kitu kwa usawa. Waamuzi nao ni binadamu wanakosea.


Ila kwa waamuzi ambao wanashindwa kutafsri sheria 17 za mpira kwa makusudi hili ni tatizo. Unajua ikiwa inatokea timu inashindwa kupata matokeo kutokana na mpango wa mtu ndani ya uwanja inaumiza.

Tunahitaji kuona soka letu linazidi kupanda chati kutoka hapa lilipo. Ipo wazi kwamba miongoni mwa ligi pendwa Afrika Mashariki huwezi kuiweka kando ligi yetu.

Na inafuatiliwa na watu wengi nje ya Tanzania. Sasa kama wengi wanaifuatilia ligi ya Bongo kwa nini mtu mmoja aamue kufelisha mambo ndani ya uwanja.

Ninachojua mimi ni kwamba kila Mtanzania anapenda kuona mpira mzuri ukichezwa. Ili uweze kuleta ladha ni lazima hata waamuzi pia nao wafanye kazi yao kwa umakini.

Kwa yule ambaye atakuwa amepewa dhamana ya kuongoza mchezo ni muhimu kufanya kazi kwa juhudi na kutimiza majukumu yake.

Hakuna timu inayopenda kufeli ndani ya uwanja licha ya kwamba wanajua kuna matokeo aina tatu. Sare, kufungwa na kufunga hakuna matokeo mengine tena.

Kwa matukio ya ugomvi ambayo yamekuwa yakitokea ndani ya uwanja ukianza na mzunguko wa kwanza na sasa yameanza kuonekana mzunguko wa pili.

SOMA NA HII  KMC YAIVUTIA KASI NAMUNGO FC

Hapana inatosha kwa sasa kushushudia ugomvi, tena kwenye sekta ya michezo hapana isiwe hivyo. Tanzania ni amani na upendo sasa kwa nini mashabiki ama wachezaji kuleta ugomvi.

Ikumbukwe kwamba watu wengine wanapenda kuona mpira uwanjani hawana fursa hii. Janga la Corona limebadili upepo wa mambo ila kwa hapa Tanzania, Mungu anatupigania.

Sasa hapo shabiki unapata fursa ya kwenda uwanjani kisha unaanza kuitumia vibaya nafasi hiyo. Unataka upewe nini kingine kwa mfano ili uweze kufurahi?

Ikiwa kwa sasa kuna muda wa kwenda uwanjani na kushangilia basi na iwe hivyo na sio kuanza kuleta vurugu ambazo hazina umuhimu.

Sapoti yenu ni kubwa hilo mnapaswa pongezi ila hili suala la kugombana kwa kuwarushia  waamuzi chupa za maji na kutaka kuwazingira waamuzi hili sio sawa.

Kinachotakiwa kwa sasa ni kila timu kufanya maandalii mazuri ambayoa yataifanya timu kuwa imara na pale ambapo itakuwa na mchezo mbeleni iweze kufanya vizuri.

Hapo panahitajika umakini kuanzia kwa benchi la ufundi  mpaka wachezaji kukubali kwamba watakubaliana na matokeo watakayopata ndani ya uwanja.

Mashabiki pia wanapaswa kuwa makini na kuelewa kwamba kila timu ambayo inaingia ndani ya uwanja lengo lake namba moja ni kushinda.

Masuala ya kufikiri kwamba timu hii tunaifunga mabao mengi ama kufikiria kwamba uwezo wenu ni mkubwa kuliko mpinzani hilo ni kosa pia.

Pia ninatoa rai kwa mashabiki kuendelea kujitokeza uwanjani na wachezaji kulinda matokeo pale ambapo wanakuwa wameanza kupata ushindi.

Nina amini kwamba mashabiki wa Tanzania ni wasikivu wanapenda mpira hivyo na suala hili pia walifikishe salama kwa kuwa inaewezekana kuweza kufikia mafanikio ambayo wengi wanayafikiria.

Wakati uliobaki kwa sasa mzunguko wa pili ambao ni mzunguko wa kila timu kujua kipi ambacho wanakihitaji ndani ya ya uwanja , ni muhimu kufanya kazi kwa juhudi.

Suala la kubeba matokeo mfukoni ni mwanzo wa vurugu na fujo kwa mashabiki baada ya dakika 90 kukamilika.