Home Taifa Stars KUFUZU AFCON KUNAHITAJI NGUVU KUBWA, STARS PAMBANENI

KUFUZU AFCON KUNAHITAJI NGUVU KUBWA, STARS PAMBANENI


 NGUVU kubwa kwa sasa kwa kikosi cha Stars ipo kwenye maandalizi ya mechi zao za kufuzu AFCON ambapo kwa sasa kimeweka kambi nchini Kenya.

Kazi kubwa kwa wachezaji ni kuweza kupambana kwa ajili ya taifa ili kuweza kushinda mechi zao zote mbili na kutimiza malengo ya kufuzu AFCON kwani sio kazi nyepesi.

Mechi ile ya kwanza kwa Kocha Mkuu Kim Poulsen ya ushindani itakuwa dhidi ya Equaatorial Guinea ambayo hii itakuwa ugenini na inatarajiwa kuchezwa Machi 25.

Mchezo huu ni muhimu kwa Stars kuweza kupata ushindi ili kufufua matumaini ya Watanzania kuweza kufuzu Afcon na kila kitu kinawezekana.

Njia pekee ya kuwapa furaha mashabiki ni kushinda na kucheza kwa juhudi isiyo ya kawaida katika kusaka matokeo. Muhimu kujituma na kutimiza majukumu kwa wakati.

Ikiwa kila mmoja atatimiza majukumu yake itakuwa ngumu kwa timu kupoteza na ugenini kazi inaonekana imekuwa kazi kwa Stars kupata matokeo.

Hali hiyo hata mwalimu mwenyewe aliona na aliweka wazi kwamba kuna tatizo mahali. Kikubwa ambacho kinatakiwa kufanyika ni vijana kupambana kutimiza majukumu yao.

Ni wakati mwingine wa kuweza kuonyesha kwamba hamkuwa kambini kupoteza muda bali kufanya maandalizi mazuri kwa wakati.

Tunaamini kwamba muda ambao mlipata kwa ajili ya maandalizi umekwenda sawa na tayari mpo tayari kwa ajili ya kuingia uwanjani kusaka ushindi.

Tunawatakia kila la kheri kwenye kupeperusha bendera ya Tanzania. Wakati wenu ni sasa kufanya kazi kwa vitendo na kila la kheri iwe kwenu kwa wakati huu.

Jambo moja ambalo Watanzania wanalitegemea kutoka kwenu ni matokeo ya ushindi. Ikiwa itakuwa hivyo basi tabasamu litarudi na matumaini ya kupenya mbele yataonekana.

Wakati ambao tunapita kwa sasa kwa Stars ni mgumu hasa ukizingatia kuwa kupata matokeo ugenini imekuwa ni shida.

Ili kuweza kurudi kwenye ubora wa kupata matokeo ugenini ni lazima milango ya ushindi ifunguke wakati huu ambao upo mbele yetu.

Mechi ya kwanza ina umuhimu kisha ile ya pili itakuwa ni muhimu zaidi katika kukamilisha hesabu zetu za kutinga hatua ya mbele ya michuano hii.

SOMA NA HII  TANZANIA U-20 WAANZA SAFARI YA MATUMAINI KUFUZU AFCON....

Rai yangu kwa wachezaji kujipanga vizuri na kutumia vema maelekezo ambayo wanapewa na benchi la ufundi. Safu ya ulinzi inaonekana imekuwa haina uimara sana sawa na ile ya ushambuliaji hivyo muhimu ni kuwa tayari.

Kila mchezaji acheze kwa juhudi huku akitambua kwamba Watanzania wanawaombea dua na wanahitaji kuona timu inashinda.

Nguvu kubwa kwenye kusaka matokeo uwanjani ianze sasa na ikiwa timu itashinda mchezo wake ugenini itavunja ule uteja wa kushindwa kupata matokeo ugenini.

Kitu pekee ambacho kinatoa nguvu kwenye kupata matokeo ugenini ni kujiamini na kutimiza majukumu ambayo wamepewa na benchi la ufundi.

Ipo wazi kwamba wachezaji wa timu zote mbili wanahitaji kupata ushindi hivyo hilo likae pia kwenye vichwa vya wachezaji wa Stars kwamba wanaingia kwenye pambano ambalo wapinzani wao wanahitaji ushindi.