Home Yanga SC TIMUATIMUA MAKOCHA NDANI YA YANGA HAIJENGI BALI INABOMOA

TIMUATIMUA MAKOCHA NDANI YA YANGA HAIJENGI BALI INABOMOA

 

UTAMADUNI kwa kila timu ndani ya ardhi ya Bongo kwa miaka ya hivi karibuni umekuwa ni tofauti hasa pale mwendo unapokuwa ni mbovu ghafla.


Zipo timu ambazo zimekuwa zikiwafuta wale wafanyakazi wanaowazunguka. Pia zipo timu ambazo zimekuwa zikiwasimamisha wachezaji pamoja na nyingine kuwafuta kazi makocha.

Hili la kuwafuta kazi makocha imekuwa ni njia nyepesi kwa viongozi wengi wakiamini kwamba ni njia ya kujenga na kusahau kwamba wakati mwingine wanabomoa.

Tunaona kwamba Klabu ya Yanga ambayo ilianza msimu ikiwa na kocha wao mpya ambaye hakudumu na kumpa mikoba kocha mwingine mambo yamekuwa magumu kwake.

Ilianza msimu wa 2020/21 chini ya Kocha Mkuu, Zlatko Krmpotic ambaye naye alifutwa kazi baada ya kuongoza kwenye mechi tano ndani ya ligi.


Alishinda mechi nne na kulazimisha sare hivyo wakati anaspa timu ya Yanga ilikuwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo kama ambavyo Cedric Kaze ameiacha ikiwa na pointi 50.

Tayari kwa sasa Yanga ndani ya msimu huu wa 2020/21 imefuta kazi makocha wawili ambao sababu kubwa wanaeleza kwamba ni mwendo mbovu wa timu zao.

Ukitazama namna ambavyo walianza msimu kwa kasi kila timu ilikuwa inahofia kukutana na Yanga ndani ya uwanja ila baadaye ile kasi ikayeyuka ghafla na sasa wamebaki kutafutana wenyewe.

Ukitazama kwa ukaribu imeonekana kwamba wachezaji wake wengi wamekuwa wakicheza chini ya kiwango na hakuna ambaye anajali hilo zaidi ya kuwageukia makocha na kuwafuta kazi.

Ipo wazi kwamba makocha wameajiriwa ili wafutwe kazi ila inapokuwa ni mara kwa mara tena kwa wakati mmoja haijengi timu.

Ili timu iweze kufikia malengo ni lazima ikubali kuwa na mwalimu ambaye atadumu kwa muda mrefu atakwenda sawa na sera ya kile ambacho wanahitaji.

Inaonekana kwamba Yanga wanahitaji mafanikio ya haraka yaani wapate kocha leo kesho apeleke timu uwanjani ishinde mabao zaidi ya saba.

Pia kwenye mashindano yote ambayo watashiriki watahitaji washinde ili waweze kufurahi kwa kuwa wamekosa kutwaa ubingwa wa ligi kwa muda mrefu.

SOMA NA HII  KISA SIMBA...DJIGUI DIARA AWEKWA KANDO YANGA....NABI AFUNGUKA A-Z MAMBO YALIVYO...AMTAJA SAKHO....

Haikatazwi kufikiria mafanikio kwa kila mwalimu ila haina maana kwamba kila mechi lazima matokeo yapatikane ndani ya uwanja.

Ikumbukwe kwamba kila timu ambayo inaingia uwanjani hesabu kubwa ni kupata pointi tatu. Ipo wazi hakuna mwalimu ambaye anafikiria kuona timu yake inapoteza ndani ya uwanja.

Wale ambao wanahitaji mafanikio ya haraka ni ngumu kufikia jambo hilo kwani kila kitu kinahitaji subira ili kuweza kufika huko.

Hata timu nyingine ambazo zinaona kwamba hazipati matokeo mazuri ni lazima zifaye tathimini ya pale ambapo wanakosea ili kwenda sawa na wakati.

Makocha wawili ndani ya msimu mmoja hii haileti picha ya ushindani bali inavuruga ushindani ndani ya timu pamoja na wachezaji wenyewe.

Huenda kuna makundi ambayo yalikuwa yanamkwamisha mwalimu ashindwe kupata matokeo chanya. Ikiwa yeye ameondoka na makundi yamebaki bado tatizo litabaki palepale.

Itakuwa ngumu kufikia mafanikio ikiwa chanzo cha matatizo hakijafahamika. Ikumbukwe kwamba awali waliokuwa wakitajwa kwenye matokeo mabovu ilikuwa ni waamuzi kisha ikahamia kwa wachezaji.

Kwa kufanya hivyo na kuhamia kwa makocha bado inaonekana kwamba tatizo lipo ndani ya Yanga ila wale ambao wanatambua ukweli wa mambo wanaficha na kujiweka kwenye kivuli cha matokeo.

Bado kuna safari ndefu katika kufika pale ambapo kila mchezaji pamoja na kiongozi wa Yanga anahitaji. Itakuwa ngumu ikiwa hakutakuwa na utulivu pamoja na kukubali kwamba ushindani upo na kufungwa ni sehemu ya mpira.

Kuvunja benchi la ufundi mara kwa mara hakujengi pia bali kunavunja nguvu ya kufikia malengo ambayo yanaishi ndani ya timu kiujumla.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here