Home Yanga SC YANGA WASIMAMISHA MAZOEZI KWA SABABU YA MAGUFULI

YANGA WASIMAMISHA MAZOEZI KWA SABABU YA MAGUFULI

 


KUFUATIA kifo cha cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, uongozi wa Yanga, umelazimika kusitisha mazoezi yake ya kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara, hadi pale shughuli za kuaga kwa mwili zitakapokamilika.

 

Yanga iliingia kambini  Machi 13 mwaka huu, ikiwa chini ya Juma Mwambusi aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya kocha wao wa zamani Cedrick Kaze ambaye alifutwa kazi Machi 17 akiwa jijini Arusha baada ya kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Polisi Tanzania.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ameweka bayana kuwa, wamesitisha ratiba za mazoezi ya timu hiyo, tangu Machi 18 mwaka huu, mara tu baada ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutangaza kifo cha Hayati Dkt. Magufuli, hivyo watatoa taarifa za kurejea kwa mazoezi tena mara tu baada ya shughuli za kuaga mwili kumalizika.

 

“Ifahamike kwamba hatujavunja kambi, ila tumesitisha ratiba za mazoezi ya timu, hadi hapo baadaye, baada ya shughuli za kuaga mwili wa kiongozi wetu kukamilika hapa jijini Dar es Salaam, tumelazimika kufanya hivyo mara tu baada ya kutangazwa kwa kifo.

 

“Imekuwa ni ngumu sana kwetu kuendelea na program za mazoezi hivyo tumesitisha kwa muda hadi hapo baadaye tutakapolitazama hili upya tutatoa taarifa za lini tutarejea mazoezini,” alisema Bumbuli.

SOMA NA HII  VIDEO: KIUNGO WA YANGA TONOMBE MUKOKO AFUNGUKIA ISHU YAKE YA KAIZER CHIEFS