Home Taifa Stars KUSHINDWA KUANZA KWA KASI MWANZO KUNAIFELISHA STARS, LAZIMA JAMBO HILO LIFANYIWE KAZI

KUSHINDWA KUANZA KWA KASI MWANZO KUNAIFELISHA STARS, LAZIMA JAMBO HILO LIFANYIWE KAZI


KUSHINDWA kupata matokeo chanya kwenye mechi za mwanzo ni kosa ambalo limefanywa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Mchezo wake wa mwisho wa kusaka nafasi ya kuweza kushiriki kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika, (Afcon) iliweza kututoa kimasomaso Watanzania kwa kupata ushindi mbele ya Libya.

Ushindi huo haujawa na maana kubwa kwa sababu lengo la Stars kufuzu Afcon limekwama kutokana na kushindwa kufikia pointi za kutosha kuwapa nafasi kushiriki mashindano hayo makubwa.

Mwanzo wa kusuasua katika kusaka ushindi yameipa Stars maumivu na kuwafanya mashabiki kuzidi kugumbikwa na ganzi kwa kuwa walikuwa wanahitaji ushindi.

Nina amini kwamba benchi la ufundi limeona matatizo yalipo na namna ambayo itawafanya waweze kupata matokeo wakati ujao mapema.

Tumeona kwamba pointi 7 zimetufanya tubaki Bongo huku wale wenye pointi 9 Equatorial Guinea wakipata fursa ya kushiriki Afcon.

Kwa namna moja tumehusika kuwapa ushindi Equatorial Guinea kwa kuwa kwenye mchezo ambao tuliwafuata ugenini tulipoteza pointi zote tatu muhimu.

Licha ya kwamba tulipoteza kipindi cha pili na tena dakika za lala salama bado haitupi nafasi ya kuweza kwenda Cameroon tutabaki hapahapa tulipo mpaka wakati ujao.

Makosa ambayo yametokea kwa msimu huu ni muhimu yakafanyiwa kazi na benchi la ufundi ili wakati ujao tuwe na suluhisho ambalo litatufanya Watanzania kufurahia mashindano ya kimataifa.

Tunaona kwamba ni tatizo kubwa kwenye ushambuliaji kuweza kufunga huku safu ya ulinzi nayo ikiwa inaruhusu makosa ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakiwekwa sawa na mlinda mlango.

Hapa pia bado viungo nao wanaonekana kushindwa kukosa ule ubunifu wa kutengeneza nafasi kwa washambuliaji ili waweze kufunga mabao mengi zaidi.

Benchi la ufundi nalo liliweka wazi kwamba nafasi ambazo zimekuwa zikitengenezwa ni chache nazo pia zimekuwa hazitumiki ipasavyo.

Maana yake ni kwamba kila mahali kuna mapungufu na haya yamekuwa yakiigharimu timu kiujumla katika kusaka ushindi kila wakati.

Kwa wachezaji ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza ama kuitwa timu ya taifa ni muhimu kuwa na mbinu za kutengeneza nafasi na kuzitumia nafasi ambazo wanazipata.

SOMA NA HII  TANZANIA YATWAA UBINGWA WA CECAFA U 23, KOCHA AWAPA TANO

Ni ngumu kupata nafasi tatu ama nne ugenini kwa sababu mbinu kubwa kwa soka la Afrika imekuwa ni kujilinda zaidi na kushambulia kwa kushtukiza.

Katika hili ni muhimu kufanyiwa kazi ili wakati ujao kusiwe na makosa haya ambayo yanasababishwa matokeo mazuri ya mwisho kuwa mapambo na hayana faida kwa namna yoyote.

Nilipata bahati ya kuufuatilia mchezo wa mwisho dhidi ya Libya Uwanja wa Mkapa, kwa kweli hali haikuwa nzuri kwa namna ambavyo ilipokewa na mashabiki.

Licha ya kwamba ulikuwa ni mchezo wa kufuzu Afcon bado waliona ni sawa na mchezo wa kirafiki. Wana haki ya kuona hivyo kwa sababu hakuna ambacho kilikuwa kinashindaniwa zaidi ya timu zote mbili kukamilisha ratiba.

Basi nina amini kwamba wachezaji wamejifunza na wamepata kitu ambacho kitawaongezea nguvu wakati ujao kupambana mwanzo mwisho kwenye mechi zote.

Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) linapaswa litazame kwa ukaribu maandalizi ya mechi za ugenini na kuweza kutegua mitego yote ya manyanyaso ambayo yanafanywa kwa wachezaji.

Kwa kuwatumia wachezaji wazoefu pamoja na kuandaa mazingira mapema kwa mechi za ugenini itakuwa ni fursa ya kuweza kuondoa baadhi ya mateso ambayo wachezaji wanaweza kuyapitia.

Wachezaji wenyewe wameweka wazi kwamba wamekuwa wakishindwa kupata matokeo chanya kwenye mechi za ugenini kutokana na kuonewa wanapokuwa huko.

Rekodi inawahukumu kwa sababu kwenye mechi za ugenini imekuwa tatizo kwa Stars kushinda hata mechi za kirafiki kwa miaka ya hivi karibuni hapo kuna jambo la kulitazama.

Ikumbukwe kwamba kabla ya kuvaana na Equatorial Guinea, Stars ilicheza na Kenya mchezo wa kirafiki na ilipoteza dhidi ya Kenya kwa kufungwa mabao 2-1.

Imani yangu ni kwamba kutakuwa na mabadiliko makubwa wakati ujao na kutengeneza timu imara ambayo itakuwa na mwendo mzuri katika kusaka ushindi.

Pia wachezaji nao wana kazi ya kufanya wanapopewa majukumu uwanjani kwa kujituma bila kuogopa kwa ajili ya kupambania jezi ya timu ya taifa ya Tanzania.

Kila kitu kinawezekana ikiwa kutakuwa na mipango makini na endelevu. Mashabiki na Watanzania wanahitaji ushindi hapo ndipo furaha yao ilipo.