NGUMI kali ya kati kwenda juu (Uper Cut) ya Saul ‘Canelo’ Alvarez ilitosha kumchakaza Billy Joe Saunders akishindwa kuinuka kutoka kwenye kiti chake baada ya raundi nane za pambano lao la kuwania taji la ubingwa wa dunia la umoja ‘Unification bout’.
Baada ya Saunders kuachia mwanya, Canelo raia wa Mexico alirusha ngumi mithili ya risasi ambayo ilisababisha uvimbe wa haraka juu ya jicho la kulia la Bondia huyo wa Uingereza.
Kocha wa Saunders aliamua kusimamisha pambano hilo, kwani bondia wake hakuweza kuona tena kwa wakati huo.
Huku akishuhudiwa na watu takriban elfu 73,126 waliohudhuria pambano hilo Saunders alishindwa kabisa kunyanyuka kwenye kiti kuendelea na pambano hilo.
Alvarez mwenye umri wa miaka 30 alisema, alipoenda kwenye kona yake ya kupumzikia alimwambia Kocha wake Eddie Reynoso kwamba anahisi amevunjika shavu kutokana na hali aliyokua akiihisi kwenye kinywa chake.