Home Simba SC KUHUSU WACHEZAJI WATAKAOACHWA SIMBA, GOMES AMEFUNGUKA HAYA..

KUHUSU WACHEZAJI WATAKAOACHWA SIMBA, GOMES AMEFUNGUKA HAYA..


KOCHA wa Simba, amewahakikisha maisha ndani ya Msimbazi mastaa 17 wazawa. Amelithibitishia Soka la Bongo kwamba hatawagusa kabisa kwenye usajili ujao labda wao wenyewe wazingue.

Gomes amesisitiza kwamba kila akiangalia timu nyingine za Ligi Kuu haoni wachezaji wazawa wenye kitu cha ziada kushinda mastaa wake 17 akimaanisha na wale wanaosugua benchi.

Simba wamebakiza mechi tisa za Ligi Kuu Bara, wanapambana ili watetee ubingwa wao lakini kuna wachezaji watano wazawa ambao mikataba yao inamalizika mwisho mwa msimu ambao ni Ibrahim Ajibu, Miraji Athumani, Beno Kakolanya, Gadiel Michael na Ally Salim.

Ukiondoa wachezaji 11 wa kigeni ndani ya Simba wanabaki wazawa 17 ambao ni Aishi Manula, Kakolanya, Shomary Kapombe, David Kameta, Mohammed Hussein, Gadiel, Kennedy Juma, Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Jonas Mkude na Mzamiru Yassin.

Wengine John Bocco, Hassan Dilunga, Ajibu, Said Ndemla, Ally Salim na Miraji. Gomes hajagusia upande wa wachezaji wa kigeni kusisitiza wabaki ingawa kuna baadhi yao wapo njiapanda akiwemo Francis Kahata aliyekuwa na mkataba wa kucheza mechi za kimataifa tu na unamalizika mwishoni mwa msimu, Perfect Chikwende hajaonyesha kiwango bora kama matarajio yao huku Chris Mugalu naye akitajwa.

Pamoja na viwango vyao, upande wa Mugalu amekuwa akipewa nafasi kikosi cha kwanza na Gomes ingawa upande wa mabosi wa timu hiyo hawana imani naye ya moja kwa moja.

Wachezaji hao mbali ya mikataba yao kumalizika pia hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi hicho.

Akizungumza na Soka la Bongo, Gomes alisema kuwa hatamani kuona mchezaji mzawa anaondoka kwenye kikosi chake kwani anawakubali na kuwaelewa labda utokee uamuzi mwingine.

“Kuhusu kuwatumia mara kwa mara hilo linatokana na mahitaji ya timu kulingana na mechi husika kwani bado tuna michezo mingi, watatumika hata wakati mwingine.

“Naamini kwa muda ambao nimefundisha Simba na kufuatilia timu nyingine kwa wachezaji wa ndani walio kwangu ni bora kwa maana hiyo nahitaji kuendelea kuwa nao.

SOMA NA HII  MO DEWJI AAMUA KUIKOMESHA YANGA...MASTAA SIMBA WAOGA NOTI...ATAKA KIKAO CHA HARAKA NA MGUNDA...

“Kama ikitokea kuna ambaye anafikiria jambo lingine au kufanya mazoezi tofauti na ambavyo nahitaji na anataka kuondoka Simba sitamzuia ila binafsi sitaacha mzawa yeyote,” alisema Gomes.

Hata hivyo, mabosi wa Simba wameanza kuwaongezea mikataba nyota wao kadhaa wakiwemo Mohamed Hussein, Kennedy Juma, Shomary Kapombe, John Boco na Paschal Wawa huku wakiwa kwenye mazungumzo na Kakolanya ambaye ni kipa wa zamani wa Yanga na Prisons.

Katika hatua nyingine, kocha wa makipa, Mbrazil Milton Nienov naye amewaambia mabosi wake kuwa anahitaji makipa wake Kakolanya na Salim kuhakikisha wanabaki kikosini.

Milton alisema ushindani na viwango vinavyoonyeshwa na makipa wake watatu hana hofu navyo hata kama ikitokea, Aishi Manula amekosekana kwenye mchezo wowote.

Alisema walikuwa na udhaifu kiasi aliowakuta nao lakini kwa sasa wameimarika na kubadilika kama anavyohitaji.

“Nikiendelea nao watakuwa imara zaidi ndio maana sitaki kuona Kakolanya na Salim wanakwenda kokote natamani waongezewe mikataba.

“Tulimkosa Manula mechi ya ugenini na Al Merrikh alicheza Kakolanya ambaye alifanya vizuri huku benchi alikuwepo Salim, lango la Simba lipo salama,” alisema Milton.