Home Azam FC SUALA LA USAJILI WAACHIWE MAKOCHA, MAPAMBAO YAENDELEE

SUALA LA USAJILI WAACHIWE MAKOCHA, MAPAMBAO YAENDELEE


 ORODHA ya wachezaji ambao  wataripoti kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi kwa sasa ipo wazi.


Kim Poulsen Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, yeye ametaja kikosi hicho kwa ajili ya kuanza maandalizi rasmi hivyo ni muhimu kwa wachezaji ambao wameitwa watimize majukumu yao kwa wakati.


Kikubwa ambacho kinatakiwa ni wachezaji kutambua kwamba Watanzania wanahitaji kuona matokeo chanya kwa kila mchezo ambao watacheza.


Kuwa katika mechi ya kirafiki na kupata matokeo mazuri ni nafasi ya kuweza kujenga hali ya kujiamini na kuwa na mwendo mzuri kwa wakati ujao.


Baada ya kikosi kutajwa tunaona kwamba kila mtu anakuwa na chaguo lake akihitaji kuona baadhi ya wachezaji ambao anawapenda kuwa kwenye kikosi.


Hilo la kuitwa ama kutoitwa libaki mikononi mwa kocha kwa sababu yeye anajua aina ya wachezaji ambao anawahitaji katika kikosi.


Kwa kumuachia kocha suala la wachezaji itapunguza ile presha ambayo huwa inaanza kwa mashabiki. Kazi ya mashabiki iwe ni kuwapa sapoti wachezaji.


Makosa ambayo watayafanya wachezaji itakuwa ni darasa kwa benchi la ufundi kujua namna gani wataboresha kikosi kwa wakati ujao.


Imani yangu ni kwamba Poulsen amekuwa akifuatilia wachezaji hasa kwenye mechi za ligi pamoja na mashindano mengine jambo ambalo linampa fursa ya kuchagua wachezaji ambao anawahitaji.


Wakati ujao nina amini kwamba atakuja kupata wachezaji ambao watampa matokeo kwani suala la kuchagua ni gumu na huwezi kuwachagua wachezaji wote.


Jambo la msingi kwa wale ambao hawajatwa ni kuongeza juhudi ili kuweza kupata nafasi ya kuitwa katika kikosi kupambania bendera ya Tanzania.


Hakuna ambaye ana namba ya uhakika katika kikosi cha timu ya taifa kila mmoja ana uwezo wa kuwa katika kikosi ila jambo la msingi ni nafasi pamoja na kujituma bila kuchoka.


Muhimu ni kuona kwamba wachezaji kwenye mchezo huo mnapambana kusaka matokeo na kupata matokeo chanya hilo ni jambo ambalo Watanzania wanahitaji.

SOMA NA HII  AZAM FC WAIVUTIA KASI MBEYA CITY


 Pia kwa sasa tunakwenda kwenye lala salama ambapo ligi itakapomeguka kwa msimu huu kinachofuata ni suala la usajili,

Hapa huwa kunakuwa na sarakasi nyingi kwa timu kushindwa kusimamia ripoti za makocha jambo ambalo limekuwa likileta matokeo ya kushangaza.


Ipo wazi ukiangalia aina ya wachezaji wengi ambao walisajiliwa na timu nyingi wakati uliopita ni wachache ambao walitumika na kuonyesha kile ambacho timu ilikuwa inahitaji.


Kwa maana hiyo ni kwamba wachezaji wengi walisajiliwa kwa uhitaji wa baadhi ya viongozi ama wakati mwingine kuamua kukomoana jambo ambalo halipo sawa.


Kinachotakiwa kwa sasa ripoti zikitolewa na benchi la ufundi zifanyiwe kazi na usajili uzingatie ripoti ya mwalimu na sio mapendekezo ya kiongozi fulani ama kusajili ili mradi hii haitapendeza.