BERNARD Morrison kiungo mshambuliaji ndani ya kikosi cha Simba amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Yanga kwa sasa hawaufikirii na badala yake hesabu zao ni kwenye mchezo wao dhidi ya Azam FC.
Morrison alianza kikosi cha kwanza kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Mbeya City uliochezwa Uwanja wa Mkapa na ubao ulisoma Simba 4-1 Mbeya City.
Mchezo wao ujao ni dhidi ya Azam FC ambao ni Kombe la Shirikisho hatua ya nusu fainali kisha baada ya mchezo huo unaofuata ni wa ligi dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Julai 3, Uwanja wa Mkapa.
Mzee huyo wa kuchetua ambaye alipofanyiwa mabadiliko alikwenda kukaa kwa muda kwenye benchi la wachezaji wa Mbeya City alisema kuwa wanafurahia kufanya vizuri kwenye mechi zao.
“Tunafurahi kupata matokeo, ila kuhusu mechi yetu dhidi ya Yanga hiyo kwanza hatuifikirii zaidi maandalizi yetu ni kwenye mchezo wetu dhidi ya Azam FC.
“Baada ya mchezo huo hapo tutajua tutakuwa na maandalizi ya namna gani ila kwa sasa tunafikiria zaidi kuhusu Azam FC,” amesema.
Bao lake alilowatungua Namungo FC, akiwa nje ya 18 bado linashikilia rekodi ya kuwa bao bora kwake ndani ya ligi kwa msimu wa 2020/21.