Home Yanga SC DAKIKA YA 80, MOLINGA BADO ANAONGOZA KWA WASHAMBULIZI YANGA

DAKIKA YA 80, MOLINGA BADO ANAONGOZA KWA WASHAMBULIZI YANGA


UMEONA kuhusiana na safu ya ushambuliaji ya 
Yanga, kuna taarifa kuna mshambuliaji anaweza kuondoka na inawezekana kuna mchezaji mwingine anaweza kuondoka.

Hadi sasa katika safu hiyo ya ushambuliaji ya Yanga, hakuna mchezaji ambaye amefikisha angalau mabao 11. Inawezekana kabisa katika wapya, Yacouba Songne anaweza kufikisha idadi hiyo kutokana na mwendo wake kuwa mzuri.

Kufikisha inawezekana, jiulize anaweza kuvuka idadi hiyo ya mabao na kumfanya kuwa ana idadi kubwa ya mabao ya kufunga kuliko aliyekuwa mfungaji bora wa msimu uliopita, Papaa Molinga.

Raia huyu wa DR Congo alifunga mabao 11 katika Ligi Kuu Bara akiwa anaitumikia Yanga iliyokuwa na matatizo mengi na kikosi ambacho hakikuwa na nguvu kama kikosi hiki kilichoundwa upya.

Maoni ya wadau wengi wapenda soka waliamini Molinga kwa kuwa alifanya vizuri akiwa na Yanga ambayo haikuwa na wachezaji wengi bora, angekuwa msaada kwa Yanga msimu huu.

Bahati mbaya, viongozi wa Yanga waliokuwa wanafanya usajili, waliamini muarobaini ilikuwa ni kuachana na wachezaji wengi wa kikosi hicho akiwemo mfungaji wao bora wa msimu.

Molinga aliachwa na Yanga yeye mwenyewe akiwa haamini kama uongozi wa Yanga ulifikia kumuacha. Yeye aliona haikuwa sawa lakini hakuwa na namna yoyote ya kuweza kujiokoa na kubaki Yanga.

Moja ya maoni niliyoyatoa wakati huo kwamba Yanga wanapaswa kubaki na Molinga kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao licha ya kwamba kikosi cha Yanga wakati huo hakikuwa na nguvu kubwa na kilihitaji marekebisho.

Inawezekana marekebisho yalikuwa makubwa sana na Yanga walijitahidi kubadilisha mambo,leo aliyeletwa katika nafasi ya Molinga kwa maana ya Michael Sarpong ameshindwa, zaidi ya mechi 15 ana mabao manne na dalili zote zinaonyesha ataondoka Yanga.

Tuseme sasa ni dakika ya 80 na Molinga bado anaongoza kwa idadi ya mabao ya kufunga kwa washambuliaji wa Yanga waliokuwepo msimu uliopita na hawa wapya katika msimu huu.

Ligi ndio inakwenda ukingoni na unaona kuna kila dalili utasikia siku moja huenda Molinga au Herietier Makambo ambaye alikuwepo Yanga kabla ya Molinga, mmoja wao akirejea kwenda kuokoa jahazi la kikosi hicho katika ufungaji.

SOMA NA HII  YANGA WAKOMAA NA PACHA WA NZEGELI.... ISHU IKO HIVI

Kuna jambo la kujifunza hapa kwamba wakati mwingine ni vizuri kuwapa nafasi ambao ulishawapa nafasi na wakaonyesha namna fulani ya kufanya vizuri kuliko kwenda kukimbilia wachezaji wapya ambao hawajawahi kufanya kazi na wewe hata mara moja.

Maana yake iko hivi, mchezaji ambaye amekuwa na kikosi chako amejifunza utamaduni wa kikosi kwa maana ya ubora na upungufu, namna ambavyo anaweza kupambana na mabeki wa timu kadhaa za Ligi Kuu Bara na pia katika michuano mingine.

Washambulizi wapya wengi wa Yanga wamekuwa hadithi, hata wale viungo washambulizi nao wameshindwa kuwa na msaada mkubwa na kikosi cha Yanga licha ya kwamba wamekuwa na majina makubwa na mbwembwe nyingi.

Kwa maana ya takwimu, Molinga bado ni bora zaidi ya Carlinhos, bado ni bora dhidi ya Saido Ntibazonkiza, zaidi ya Abdulrazak Fiston na bado bora zaidi ya Sarpong. 

Unaona, pekee, Yacouba ndiye anakwenda kumkaribia mkali huyo na katika mechi chache zilizobaki, huenda akafikia idadi ya mabao aliyofunga msimu uliopita, acha tusubiri huku tukiendelea kupokea funzo kutoka kwa Molinga.