Home Makala LUSAJO MKUMBUSHE MNATA ASIRUDIE TABIA YAKE KWA MASHABIKI

LUSAJO MKUMBUSHE MNATA ASIRUDIE TABIA YAKE KWA MASHABIKI


 KWENYE mchezo wa Ligi Kuu Bara mbele ya Ruvu Shooting mdogo wake Reliants Lusajo anayecheza ndani ya Namungo alifanya kitendo ambacho hakikuwa na uungwana hata kidogo kwa mashabiki wake.

Ni Metacha Mnata ambaye pia yupo kwenye kikosi cha U 23 kinachoshiriki mashindano ya CECAFA.

Bahati mbaya sana kwa kitendo ambacho alikifanya alikutana na rungu la moja kwa moja la kufungiwa kwa muda usiojulikana na mabosi wake wa Yanga kwa kile walichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.

Hata Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) nalo halikumuacha salama lilimpiga faini ya laki tano pamoja na kufungiwa kwenye mechi tatu.

Haina maana kwamba nakubali kwamba alichokifanya haikuwa utovu wa nidhamu hapana ila ukiangalia mzunguko wa matukio ambayo yalikuwa yanatokea ndani ya Yanga acha kabisa.

Kuna tukio moja ambalo liliwahi kutokea kwa mchezaji Said Ntibanzokiza ambaye ni raia wa Burundi kuonyesha ishara ya kuomba mabadiliko baada ya kufunga bao mbele ya Gwambina FC.

Mchezaji huyo mwenye uwezo mkubwa alifanya hayo mbele ya Juma Mwambusi ambaye alikuwa ni Kaimu Kocha zama hizo kwa kuomba afanyiwe mabadiliko kwenye mchezo na alionekana kukasirika kwa kitendo cha kuanzia benchi, kilichofuatiwa aliongea kwa kusema kwamba ilikuwa ni sehemu ya mchezo.

Kwa kuwa sasa ilikuwa ni zamu ya mzawa Metacha Mnata ambaye yupo kwenye kikosi cha taifa kwa vijana chini ya miaka 23 nina amini kwamba ilikuwa ni tabia ya kuiga matukio ya wakubwa ila bahati mbaya alifanya jambo gumu.

Muhimu kuona kwamba kwa wakati ujao hasa baada ya kuona jina lake ni miongoni mwa wachezaji ambao wana kazi ya kupeperusha bendera ya taifa kwenye mashindano ya CECAFA U 23 anabadilika na kuacha kabisa.

Ikitokea amepata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza kisha kwa bahati mbaya akashindwa kutimiza kazi yake ya kuzuia bao akafungwa, basi asirudie tabia yake iliyopita kwa mashabiki lazima awaheshimu mashabiki.

Uwepo wa Lusajo, Yusuph Mhilu kutoka Kagera Sugar na Sospeter Israel huyu kutoka Azam FC hawa rekodi zinaonyesha kwamba wana zaidi ya miaka 23 hivyo wana kazi ya kumuongoza kijana wao Mnata asirudie yale aliyofanya mbele ya mashabiki baada ya kuruhusu mabao mawili na timu yake ilishinda mabao matatu.

SOMA NA HII  WAWAKILISHI KIMATAIFA KAZI BADO IPO

Jambo la msingi kwa kila mchezaji ambaye ameitwa katika kikosi cha timu ya taifa kinachonolewa na Kocha Mkuu, Kim Poulsen wapambane kufanya kweli.

Ni Julai 19, kikosi kiliingia kambini ili kuweza kuona kwamba maandalizi yanaanza mapema kuelekea mashindano ya CECAFA U 23.

Nidhamu iwe msingi kwa kila mchezaji kufanya vizuri na kutimiza majukumu yake bila kuchoka kwani ni muhimu kuona kwamba taifa linapata matokeo chanya na wale ambao watapata kazi ya kuanza kikosi cha kwanza watafute matokeo.

Kila kitu kinawezekana na kila jambo lipo mkononi mwa wachezaji imani yetu ni kuona kwamba wachezaji ambao wamepewa nafasi ya kuitwa wanatimiza majukumu yao.

Suala la kuitwa wasindikizaji kwenye kila mashindano muda wake umekwisha jambo ambalo tunahitaji kwa sasa ni ushindi hakuna jambo lingine.