Home Simba SC SIMBA SASA YAWACHIMBA MKWARA YANGA ISHU YA UBINGWA WA SHIRIKISHO

SIMBA SASA YAWACHIMBA MKWARA YANGA ISHU YA UBINGWA WA SHIRIKISHO


BAADA ya kufanikiwa kutetea kwa mara ya nne kombe la Ligi Kuu Bara, sasa uongozi wa klabu ya Simba umeweka wazi kuwa malengo yao ni kuhakikisha wanatetea tena kombe la michuano ya Shirikisho Julai 25, mwaka huu mbele ya Yanga.

Simba Jumapili iliyopita iliutangaza rasmi kwa mara ya nne mfululizo ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union, na kufanya wafikishe pointi 79 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi ya msimu huu.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana katika fainali ya kombe la Shirikisho, itakayochezwa katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma Julai 25, mwaka huu.

Huu utakuwa mchezo wa pili ndani ya mwezi mmoja kwa Simba na Yanga kukutana msimu huu, huku Yanga wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mchezo wa kiporo cha Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam Julai 3, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kuiongoza Simba kutetea ubingwa huo kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes amesema: “Tunafurahi kwa kuwa tumefanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, hii inaonyesha ni kwa kiasi gani timu hii imekuwa bora kwa miaka minne mfululizo iliyopita, sasa tunajiandaa ili kuhakikisha tunakamilisha malengo ya kutetea kombe la Shirikisho.”

Naye mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu amesema: “Malengo yetu ni kutwaa makombe kwenye kila michuano tutakayoshiriki, tumefanikiwa kwenye ligi, na sasa shabaha yetu ni kutetea ubingwa wetu wa kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga.

“Tunajua walitufunga katika mchezo wetu uliopita wa ligi, lakini nikuhakikishie kuwa tutajipanga vizuri kushinda kombe la Shirikisho Julai 25, mwaka huu.”

SOMA NA HII  KISA MAKOSA YA KINIDHAMU...GOMES ACHUKUA MAAMUZI HAYA KUHUSU JONAS MKUDE