Home Simba SC HIVI NDIVYO CAF WALIVYOITAJIRISHA SIMBA…WAJAZWA BILIONI 6.7 KWA SIKU 1,460

HIVI NDIVYO CAF WALIVYOITAJIRISHA SIMBA…WAJAZWA BILIONI 6.7 KWA SIKU 1,460


KUANZIA 2018 hadi sasa, Simba imepitia katika kipindi cha neema kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata katika mashindano ya kimataifa na yale ya ndani, ikitwaa mataji matatu ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam pamoja na matatu ya Ngao ya Jamii.

Kimataifa, timu hiyo imeweza kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili na ni msimu wa 2018/2019 ilipotolewa na TP Mazembe kwa kichapo cha jumla cha mabao 4-1, lakini ikaja tena kufika hatua hiyo msimu uliomalizika na ilikwama mbele ya Kaizer Chiefs iliyowatoa kwa kuwafunga jumla ya mabao 4-3

Kwa kuingia huko robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili, Simba imevuna jumla ya Dola 1,300,000 (Sh3 bilioni) kama zawadi za kutinga hatua hiyo na kila msimu imepata Dola 560,000 (Sh 1.5 bilioni) Pia imeweza kuwaweka sokoni nyota wake na hiyo imezaa matunda baada ya kuwauza wachezaji wake wawili tegemeo, Luis Miquissone anayeenda Al Ahly kwa Dau la Dola 1milioni (Sh2.3 bilioni) na Clatous Chama aliyeuzwa RS Berkane kwa Dau linalotajwa kuwa Dola 600,000 (Sh 1.4 bilioni)

Ukijumlisha kiasi cha fedha Simba ilichovuna kwa kipindi cha miaka mitatu kwa kutinga hatua ya robo fainali mara mbili na kuwauza Chama na Miquissone, timu hiyo itakuwa imekusanya kiasi cha Sh6.7 bilioni.

Sh6.7 bilioni ni fedha ambazo Simba inaweza kuzitumia kugharimia uendeshaji wake kwa msimu mmoja tu kutokana na kupanda kwa thamani ya timu hiyo, pia ikiamua iitumie kwa matumizi mengine inaweza kufanyia mambo mbalimbali ya kimaendeleo.

VIWANJA VITANO

Uwanja wa Gwambina uliopo Misungwi, Mwanza, umejengwa kwa thamani ya takribani Sh900 milioni ukiwa na eneo la kuchezea lenye nyasi asilia, majukwaa yanayoingiza mashabiki wapatao 11,000 na sehemu ya maegesho ya magari

Kwa mzigo ambao Simba wamekusanya ndani ya miaka mitatu, wanaweza kujenga viwanja vyenye hadhi hiyo kama vitano na wakabaki na chenji ambayo wanaweza kufanyia shughuli nyingine.

SOMA NA HII  WAKATI MAMBO MENGINE YAKIENDELEA HUKO SIMBA, KIKOSI KIMESHUKA KAMBINI LEO KWAAJILI HII

HOSTELI 3 KAMA CHAMAZI

Azam FC ndio timu yenye hosteli za kisasa zaidi zinazotumiwa na kikosi chao cha wakubwa na vile vya vijana, pia zina bwawa la kisasa la kuogelea na ukumbi wa mazoezi (GYM), ukumbi wa chakula na ule wa mikutano.

Inakadiriwa ujezi wa hosteli hizo umegharimu Sh2 bilioni hivyo katika Sh 6.7 bilioni, Simba inaweza kujenga hosteli katika maeneo matatu tofauti zenye hadhi kama zile zilizopo Azam Complex. Inakadiriwa hoteli moja ya nyota tatu inaweza kugharimu Sh3 bilioni kama gharama za chini.

Simba inaweza kuamua kujenga hoteli mbili za nyota tatu na ikawa na chanzo endelevu cha mapato katika klabu hiyo.

MABASI 60 YA ABIRIA

Gharama ya basi moja la kisasa lenye siti za kukaa abiria 40, linagharimu takribani Sh104 milioni hivyo Simba inaweza kununua jumla ya mabasi 62 na kufanya biashara ya usafirishaji inayoweza kuiingizia klabu kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya hicho walichokipata ndani ya miaka mitatu.

AKADEMI YA MAANA

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linajenga vituo viwili vikubwa vya soka hapa Dar es Salaa huko Kigamboni na kingine huko Tanga kwa gharama za jumla za Sh9 bilioni ambavyo vitakuwa na viwanja vya mazoezi vya nyasi bandia na asilia, hosteli za kulala, mabwawa ya kuogelea, kumbi za chakula, kumbi za mikutano na sehemu za kupumzikia.

Kupitia Sh 6.7 bilioni Simba ilizoingiza ndani ya miaka mitatu, inaweza kujenga kituo kimoja kikubwa cha soka na ikafanya uwekezaji wa soka kwa vijana ambao baadaye wanaweza kuuzwa na kuipa klabu kiasi kikubwa cha fedha.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Musa Hassan ‘Mgosi’ alisema; “Mpira ni fedha. Ukiona mafanikio kama hayo basi ujue uwekezaji ambao mwenyekiti wa bodi, Mohammed Dewji na klabu imeufanya ndio unaozaa matunda hivyo naamini miaka michache ijayo tutapiga hatua kubwa zaidi.”

Wadau mbalimbali wamesisitiza kwamba uwekezaji wa Simba pamoja na kujiwekea malengo ndio vitu vimewafikisha hapo walipo.

Chanzo- Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here