Home Makala KWA MKWANJA HUU CHAMA, LUIS WANGEACHAJE KUSEPA MSIMBAZI?

KWA MKWANJA HUU CHAMA, LUIS WANGEACHAJE KUSEPA MSIMBAZI?


WE ungeweza? Hilo ni swali unalopaswa kujiuliza au kumuuliza shabiki wa soka au mdau anayehoji kuuzwa kwa waliokuwa nyota watatu kwenye Ligi Kuu Bara kina Luis Miquissone na Clatous Chama wa Simba na winga wa Yanga, Tuisila Kisinda.

Miquissone ameuzwa kwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri wakati Chama na Kisinda wamejiunga na RS Berkane ya Morocco.

Ni kweli nyota hao kila mmoja alikuwa na mchango mkubwa kwenye timu yake hususan msimu uliopita na tukianza na Chama ambaye licha ya kufunga mabao matano na kutoa pasi za mabao ‘asisti’ tatu kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na kuifanya Simba ifike robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu uliopita, pia aliibuka kinara wa asisti kwenye Ligi Kuu Bara akitoa pasi za mabao 15 na kupachika mabao manane.

Miquissone naye alikuwa moto akifunga mabao matatu na kuasisti mara tatu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akifunga mabao tisa na ku-asisti mara 10 Ligi Kuu Bara.

Kwa upande wa Kisinda alikuwa na msimu mzuri ndani ya Yanga akifunga mabao matano na kutoa asisti tano kwenye Ligi Kuu Bara na kuisaidia timu yake kumaliza ligi katika nafasi ya pili.

Kila shabiki alitamani kuwaona nyota hao wakisalia katika vikosi vyao msimu ujao, lakini wameuzwa. Sio kuuzwa tu, bali wameuzwa kwa pesa ndefu ambazo Kibongo ni ngumu kwa kiongozi yeyote wa soka kuziacha

Nje ya kuuzwa kwao, ikumbukwe soka ni biashara na ndio kitu pekee wanachotegemea wachezaji kwa kiasi kikubwa kuendesha maisha na familia.

Kupitia makala hii, Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa mauzo ya wachezaji hao na faida zitakazopata pande zote tatu – kwa maana ya wachezaji, klabu walizotoka na wanakoenda kisha kupitia namba zilizopo hapa chini utatujibu kuwa wewe ungekuwa Yanga au Simba ungeweza kuwabakisha?

LUIS MIQUISONE

Taarifa lilizonazo Mwanaspoti ni kwamba, Miquissone ameuzwa kwa Al Ahly kwa Dola 1,000,000 ambazo ni zaidi ya Sh2.3 bilioni na atakuwa akipokea mshahara wa Dola 34,000 kwa mwezi sawa na Sh80 milioni – pesa ambazo kwa msimu uliopita zingeweza kulipa mishahara ya kikosi chote cha Simba.

Nje ya mkwanja huo, pia imeelezwa Miquissone atakuwa anapewa Dola 20,000 (sawa na Sh46.3 milioni) kama bonasi ya kufanya manunuzi yeye na familia yake. Hapo bado hayajatajwa marupurupu mengine atakayoyapata akiwa ndani ya Al Ahly. Hilo ndilo dili la thamani kubwa kufanywa na Simba tangu kuanzishwa kwake, je Simba wangekataa ofa hiyo?

TUISILA KISINDA

Waarabu wamefunga kazi kwa Mkongomani huyu baada ya kutoa Dola 300,000 (takriban Sh693 milioni) ili atue RS Berkane ya Morocco. Hilo ni dili kubwa kuwahi kufanywa na Yanga kwani mkwanja mkubwa ambao timu hiyo iliupata kwa miaka ya hivi karibuni ni Euro 70,000 (sawa na Sh190 milioni) baada ya kumuuza Heritier Makambo kwenda Horoya ya Guinea.

Ikumbukwe kwamba Yanga ilitumia Dola 100,000 (sawa na Sh231 milioni) kuwanunua Kisinda na Mukoko Tonombe kwa pamoja mwaka jana – pesa ambayo haifiki hata nusu ya mkwanja waliomuuza Kisinda kwenda RS Berkane.

SOMA NA HII  ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE KUHUSU UWEZO WA MORRISON....ADAI WACHINA WAMETUPIGA TZ...

Pia katika dili hilo, Kisinda atavuna Dola 150,000 (sawa na Sh346 milioni) huku pia Yanga ikipata ofa ya kuweka kambi bure nchini Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa. Kiuhalisia ilikuwa vigumu kwa Yanga kutomuuza mchezaji huyo.

CLATOUS CHAMA

Kabla ya kuonekana akiwa amevalia jezi ya RS Berkane sambamba na Kisinda, kiungo huyu fundi alikuwa kwenye mawindo ya Far Rabat ya nchini Morocco inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroeck.

Inaelezwa kuwa Far Rabat ilikuwa tayari kutoa Dola 600,000 (sawa na takriban Sh1.3 bilioni) kama ada ya uhamisho, lakini dili hilo likapigwa chini na mabosi wa Simba na kuamua kumpiga bei RS Berkane.

Kwa mantiki hiyo huenda Simba imelipwa pesa zaidi ya Sh1.3 bilioni kumuachia Chama na taarifa za ndani ni kwamba, kambi ya Simba inayoendelea Morocco ni moja ya makubaliano yaliyofanywa na pande hizo mbili katika dili la Chama.

WASIKIE WADAU

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hersi Said anasema mpira hivi sasa ni biashara, hivyo kinachoendelea ni sehemu ya utamaduni wa soka.

“Ili timu iwe kubwa lazima iwe na wachezaji wenye ubora wa kushindana na wale wa timu nyingine kubwa. Yanga ni timu kubwa, hivyo inazingatia hilo,” anasema Hersi.

“Pili, biashara ya kuuza na kununua wachezaji inafanyika duniani kote. Hii ndio dhana ya soka la kisasa nje ya wadhamini. Inabidi timu ipate faida kupitia biashara ya wachezaji, hivyo binafsi sioni kama ni vibaya kuuza na kununua.”

Mjumbe Kamati ya Usajili na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori anasema ilikuwa vigumu kukataa ofa kubwa kutoka timu zilizowataka Chama na Luis.

“Kiwango cha fedha anachokwenda kulipwa Miquissone ni karibu mara nane alivyokuwa analipwa hapa, hivyo ilikuwa ni ngumu kwetu kumzuia asiondoke. Anaenda timu kubwa na analipwa vizuri, tulijiandaa kabisa kumuacha,” anasema.

“Ila kwa ishu ya Chama ni kitu ambacho kimekuja tukiwa hatuna mpango kabisa. Msukumo umetoka kwa mchezaji mwenyewe ambaye alituambia kuwa kwenye maisha yake ya soka hajawahi kucheza misimu mitatu kwenye timu, hivyo anaomba kuondoka.

“Tuliwaza tukimzuia huyu mchezaji ndio kwanza kasaini mkataba mpya wa miaka miwili kwa gharama kubwa na bado anakoenda (RS Berkane) atapata pesa mara tatu ya huku, halafu tukiendelea tukimuacha atakuwa na kinyongo na kushindwa kufanya vizuri, na isitoshe ameshatupa kila kitu kwa miaka mitatu hivyo tukaamua acha tumuache aende.”

Magori anasema Chama alikuwa mchezaji mkubwa na alivyokuja Simba ameongezeka kukua, hivyo kuondoka kwake sio kitu rahisi kupokewa kwenye masikio ya wapenda soka na ndio maana mijadala imekuwa mingi.

Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Abdalah Kibadeni anasema biashara ya wachezaji haiepukiki duniani kote.

“Soka siku hizi ni biashara, sio kama tulivyokuwa tunacheza enzi zetu. Wachezaji hawa tunaowaona maisha yao yanategemea soka, hivyo wakipata sehemu yenye maslahi mapana zaidi inabidi waende ilhali pande zote zitaafikiana na kufanya biashara yenye tija. Hili haliepukiki,” anasema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here