KOCHA mkuu wa klabu ya Simba, Didier Gomes licha ya kushinda katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Jwaneng Galaxy, ameendelea kuwapa mbinu wachezaji wake kushinda mabao zaidi katika mchezo wao wa marudiano utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba ilishinda 2-0 dhidi ya Galaxy mchezo uliopigwa Jumapili ya wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa Botswana.
Juzi Jumanne Gomes alikuwa na mazoezi machache kwa wachezaji wake baada ya kocha wa viungo Adel Zrane kuanza na kuwapa mazoezi ya viungo ili miili yao iachie.
Mastaa John Bocco na Hassan Dilunga ndio walionyesha umahiri wa kutupia na kufanya mechi mazoezi kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mbinu ya kutumia magoli mawili iliwafanya washambuliaji wa Simba wawe wepesi kwenye kucheza kwa kuonana lakini pia kukaba bila kutegeana kwenye dakika zote walizokuwa wanacheza.
KAPOMBE, ZIMBWE JR KUMALIZA MECHI
Wakati Gomes anaendelea kutoa programu zake, wachezaji Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ a.k.a Zimbwe Jr. wao walikomaa na mazoezi yao ya kupiga mipira iliyokufa ambayo kiufundi ilionekana pia ni tatizo la Galaxy kwenye mechi iliyopita.
Zoezi hilo alianza Tshabalala peke yake kwa kuchukua mipira mitatu na kukaa umbali mrefu na alikuwa akipiga kwa umakini na ndipo Kapombe akaenda kuungana naye.
Baada ya Kapombe kuongezeka na kuonyesha wote wapo makini katika zoezi hilo, kocha wa viungo Adel Zrane aliwekea vizuizi ambavyo vilikuwa vinawapa wakati mgumu kwenye upigaji lakini bado wachezaji hao waliendelea kufunga.
Hiyo ni kama neema kwa Simba kwani msimu uliopita wachezaji ambao walikuwa hodari wa kupiga mipira iliyokufa ni Clatous Chama na Luis Miquissone ambao tayari wameshaondoka katika timu hiyo.
KANOUTE APEWA PROGRAMU MAALUM
Kiungo Sadio Kanoute na yeye alikuwa amepewa programu maalum na kocha wa viungo Adel Zrane katika mazoezi ya juzi jioni wakati wenzake wakiendelea na mazoezi mengine.
Kanoute alifungwa kamba na kuwekwa katika chuma huku akitakiwa atumie nguvu nyingi kwenda mbele kwa kukimbia zoezi ambalo lilichukua takribani dakika 10.
Zrane alikuwa akimsimamia kwa umakini kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufasaha na mchezaji huyo hakumuangusha hata kidogo kocha wake wa viungo.
GOMES AFUNGUKA
Gomes alisema jambo kubwa anajivunia kuona wachezaji wake wamepata ushindi katika mchezo uliopita kwani kufunga ugenini sio jambo jepesi hasa katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tulikuwa vizuri kwenye ulinzi, wachezaji wangu walifuata kile ambacho niliwaelekeza, tulikuwa bora kwenye mipira iliyokufa na tulipata mabao mawili,” alisema Gomes na kuongeza:
“Bado tuna kazi ya kufanya katika mchezo huu kwa kuweka nguvu na nidhamu kubwa kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo ujao na kuhakikisha tunafuzu.”