Home news SIMBA YAWAVUTIA KASI WABOTSWANA

SIMBA YAWAVUTIA KASI WABOTSWANA


 ZIKIWA zimesalia siku tano tu kabla ya mchezo 
wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, ameweka wazi kuwa tayari amepitia rekodi za video za wapinzani wao na wametambua upungufu wao.

Katika mchezo huo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba inatarajiwa kuanzia ugenini Jumapili ya Oktoba 17, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana.

Huo utakua mchezo wa kwanza kwa Simba kwenye michuano hiyo msimu huu, baada ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa timu 10 ambazo hazikucheza hatua ya awali, huku wapinzani wao Galaxy wakianzia hatua ya awali ambapo waliiondosha Zilimadjou ya Comoro kwa jumla ya mabao 5-1.

Kuhusu maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo huo, Gomes amesema: “Kuhusu wapinzani wetu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika Jwaneng Galaxy nimepata nafasi ya kuwaangalia kwenye michezo yao miwili ya mwisho, ikiwemo mchezo wa hatua ya awali dhidi ya Zilimadjou na michezo ya kirafiki dhidi ya timu za Afrika Kusini.

“Natambua kuwa wana wachezaji wengi ambao wapo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Botswana, lakini pia najua kuwa kwa msimu huu wamejiwekea malengo ya kufika hatua ya makundi ya michuano hii.

“Hivyo ni wazi tunakabiliwa na mchezo mgumu, lakini tupo tayari kupambana na malengo yetu makubwa ni kuhakikisha tunashinda mchezo wa kwanza ugenini, ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya makundi.”

Kikosi cha Simba kwa sasa kinaendelea na maandalizi kuelekea kwenye mchezo huo ili kuweza kupata matokeo chanya.


SOMA NA HII  KIBEGI CHA SIMBA CHAINGIZA KIASI HIKI CHA PESA