Home Makala ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE KUHUSU UWEZO WA MORRISON….ADAI WACHINA WAMETUPIGA TZ…

ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE KUHUSU UWEZO WA MORRISON….ADAI WACHINA WAMETUPIGA TZ…


NILIANDIKA hapa wiki chache zilizopita. Jinsi mataifa ya Afrika Magharibi yalivyotuacha mbali kisoka. Jinsi wachezaji kibao wa Afrika Magharibi wanavyoweza kuingia katika vikosi vyetu vya timu za taifa ukanda huu lakini hawafikiriwi makwao.

Mfano halisi niliutolea kwa Bernard Morrison. Angeweza kuvaa jezi za Taifa Stars, Malawi, Zambia, Msumbuji, Rwanda, Kenya, Uganda, Zimbabwe na hata Burundi. Lakini kwao Ghana hafikiriwi. Wanafikiriwa akina Jordan Ayew na wengineo.

Juzi katika Uwanja wa Taifa Morrison alikuwa akithibitisha ninachokiamini. Katika pambano dhidi ya Red Arrows ya Zambia, michuano ya kombe la Shirikisho, Morrison aliichukua mechi akaiweka mfukoni mwake. Aliacha gumzo.

Tangu Emmanuel Okwi wa enzi zake, pengine hii ilikuwa mechi bora zaidi ya uwezo binafsi wa mchezaji mmoja uwanjani kwa timu ya Tanzania. Ndiyo, ni Morrison ndiye aliyeamua mechi hii baada ya kuwa mbovu kutoka na mvua kubwa iliyonyesha.

Alianza kwa kuchangia bao la kwanza. Ni yeye ndiye ambaye alitengeneza faulo, kisha akaipiga mwenyewe. Mpira ukauacha ukuta ukaenda katika nguzo ya kushoto ya golikipa na kutinga wavuni. Hapo alikuwa amefanya marudio ya kile kile alichowafanyia Simba misimu miwili iliyopita akiwa na jezi ya Yanga.

Siku ile alikuwa amefanyiwa madhambi na Jonas Mkude, akauchukua mpira mwenyewe akautenga na kumfunga Aishi Manula. Tofauti ni siku ile alipiga juu na juzi alipiga chini. Lango lilikuwa lile lile tu la Kaskazini mwa Uwanja wa Taifa.

Bao la pili lilifungwa na Meddie Kagere. Nashangaa Kagere alikuwa bize kudansi huku akidengua badala ya kumkimbilia Morrison na kumwambia ‘Shukrani’. Kazi yote ilikuwa imefanywa na Morrison ambaye alikuwa amepiga chenga kama tano hivi kabla ya kumpigia Kagere ambaye aliegesha mguu tu na kufunga.

Haishangazi kuona kundi kubwa la wachezaji wa Simba walimkimbilia Morrison na sio Kagere. Wanajua kazi aliyofanya. Ni mambo yale yale ambayo tumewahi kumuona Lionel Messi akiyarudia mara nyingi Ulaya lakini ni nadra kuona mchezaji wa klabu zetu akiyafanya uwanja wa Taifa. Morrison alifanya.

Baada ya hapo kama kawaida yake Morrison akazua kioja cha kukosa penalti. Labda kwa sababu hakufanyiwa madhambi yeye na ndio maana hakuona uchungu wa kuipiga penalti hiyo. Aliyefanyiwa madhambi alikuwa Hassan Dilunga.

Wachezaji wa Simba wana matatizo gani katika suala la upigaji wa penalti? Msimu huu John Bocco amekosa, Erasto Nyoni amekosa, Morrison amekosa. Kuna kitu gani? Huwa hawana maandalizi ya akili kabla ya kupiga?

Morrison alikosa penalti nyepesi kuliko mabao ambayo alikuwa amefunga juzi. Penalti yake ilitabirika kwa kipa wa Arrows. Ilipaswa kuumaliza mchezo ndani ya dakika 30 tu mwanzo. Kifupi Simba wangeweza kuongoza 3-0 ndani ya dakika 30 tu.

Baadaye alikuja kujirekebisha katika kipindi cha pili baada ya mchezo kukaa 2-0 kwa muda mrefu. Ni bao hili ndilo ambalo inawezekana litakuwa limeipitisha Simba katika hatua hii. Inawezekana ushindi wa mabao 3-0 ukawa ni maji marefu kwa Arrows kuliko matokeo yangeendelea kubakia 2-0 mpaka mwisho wa mchezo.

Morrison aliukwepa mpira uliorushwa na Mohamed Hussein Tshabalala katika upande wa kushoto na kuuchomokea upotua mgongoni mwake. Alisereraka vyema zaidi akaingia katika boksi na kujikuta ametazama na kipa wa Arrows. Akafanya kile ambacho mara nyingi tumekuwa tukikiona Ulaya. Akampitisha kipa tobo. Hili lilikuwa bao ambalo lilimaliza mechi vyema.

SOMA NA HII  YA CHAMA NA MANARA..MO DEWJI ASIOGOPWE AKUMBUSHWE ANAPOKOSEA

Kama angekuwa amefunga ile penalti basi angeweza kuwa ameondoka na mpira. Sikumbuki mara ya mwisho ambayo mchezaji wa timu ya Tanzania ambaye aliondoka na mpira katika mechi ya kimataifa kama hii ya juzi. Labda Mrisho Ngassa wakati alipocheza na vibonde fulani kutoka Comoro miaka kadhaa iliyopita.

Kwa ujumla haikuwa mechi nzuri ambayo unaweza kuichambua. Wazambia walimlalamikia mwamuzi kutoka Uganda na walikuwa na haki hiyo.

Kuna wakati mwamuzi aliwauma lakini haikuwa katika matukio makubwa kama penalti na kadi nyekundu. Nadhani vyote vilistahili.

Mwamuzi aliwanyonga Wazambia katika baadhi ya matukio ya ndani ya uwanja. Kwa mfano, kuna rafu ambayo alichezewa Sadio Kanoute na mchezaji wa Arrows alipewa kadi ya njano. Rafu kama ile ile aliicheza Jonas Mkude kando ya uwanja lakini hakupewa kadi yoyote.

Mwishowe licha ya mvua kubwa bado Simba walionekana kuwa timu bora uwanjani kutokana na kushambulia kwa hamu zaidi na kwa idadi kubwa zaidi. sijajua vyema mipango ya kocha wa Arrows kabla ya kuanza kwa mechi lakini wazi kwamba alibadilisha mbinu zake baada ya mvua kunyesha.

Wazambia ni watu wanaoweka mpira chini lakini kutokana na mvua waliamua kumwacha mtu mmoja mbele na kupiga mipira mirefu. Hawakuwa na mipango mingi mibadala, pia walishindwa kujilinda vema na kunusa hatari ya mtu anayeitwa Morrison.

Kuna maangalizo mawili baada ya mechi hii. kwanza kabisa ni kwamba pambano hili bado halijafanya. Mechi ya marudiano itafanyika katika uwanja mkavu pale Lusaka na hapana shaka Wazambia watahitaji mabao ya haraka haraka kwa ajili ya kuiweka mechi katika uhai.

Ukiwasoma tu unaamini wanaamini wanaweza kufanya hivyo. Kama kuna timu ilifanya hivyo dhidi ya Simba uwanja wa Taifa wiki chache zilizopita itakuwa wao?

Simba wawe na tahadhari na Arrows. Mechi bado haijaisha. Lolote linaweza kutokea Zambia na waongeze umakini katika kujihami na kutafuta bao la ugenini ambalo wageni walishindwa kulipa katika pambano la juzi pale Temeke.

Tahadhari nyingine ni ya kawaida tu. uwanja huu wa Marehemu Mkapa tulipigwa na Wachina? Nadhani jibu ni ndio.

Ni uwanja wa kisasa uliojengwa na Wachina katika miaka ya karibuni. Ulipaswa kutumia Teknolojia mpya. inakuaje uwanja ujae maji baada ya mvua kunyesha?

Wenzetu huwa wanajenga viwanja vya kisasa ambavyo ni ngumu kujaa maji hata ikinyesha mvua kubwa iliyopitiliza.

Kuna aina ya ujenzi ambao unapaswa kutoa maji uwanjani moja kwa moja (drainage system).

Tusione jambo la kawaida tu kwamba mvua ikinyesha basi yanajaa uwanjani. Sio jambo la kawaida.

Lazima tuwaulize Wachina kwa nini walishindwa kutujengea uwanja ambao haujai maji pindi mvua inaponyesha.

Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here