Home news KABLA YA KRISMASI…CHAMA KUTUA SIMBA…SAKHO, NYONI, WAWA NA ABDULSWAMAD KUTEMWA…ISHU IKO HIVI…

KABLA YA KRISMASI…CHAMA KUTUA SIMBA…SAKHO, NYONI, WAWA NA ABDULSWAMAD KUTEMWA…ISHU IKO HIVI…


KABLA pilau la Krismasi, Simba itakuwa imefanya uamuzi katika mambo matatu ya msingi kama kila kitu kitaenda sawa. La kwanza ni ambalo kila Mwanasimba analisubiri kwa hamu. Usajili wa Clatous Chama kurejea Simba utakuwa umekamilika na wiki hii atatua Dar es Salaam kuzitulia roho za mashabiki.

Ingawa inajulikana Yanga wako kwenye mazungumzo ya karibu sana na wakala wa Chama, lakini Simba iko kwenye hatua nzuri ya kumrejesha Msimbazi, staa huyo aliyekosa namba RS Berkane anakocheza pia winga nyota wa zamani wa Yanga, Tuisila Kisinda.

Habari za uhakika ambazo zimepatikana ni kwamba, Simba imepania kumaliza dili hilo kabla ya Jumamosi hii, lakini bado wamepanga kuachana na beki Paschal Wawa huku ubora alioonyesha kwenye dabi, ukimnusuru Onyango.

Pili, Simba itaachana na Duncan Nyoni na Pape Ousmane Sakho ambao Kocha Pablo Franco amewaambia viongozi; “Wa kawaida sana hawa.”

Wachezaji hao wawili wa kigeni wameshindwa kuibeba Simba kwa ubora ambao viongozi na mashabiki walitegemea na badala yake wamekuwa wakionekana wa kawaida.

Kwenye ripoti ya Pablo aliyokabidhi wiki iliyopita amependekeza kusajiliwa nyota wapya watatu, kiungo mshambuliaji (namba nane), namba kumi ambayo nafasi hiyo imechukuliwa na Chama pamoja na straika.

Tatu, Simba itamtoa kwa mkopo kipa wake, Jeremiah Kisubi ambaye ameomba arejeshwe Prisons kwa mkopo akapate nafasi ya kucheza, kwani tangu atue Msimbazi hajawahi kukaa hata benchi tu.

Pablo amepanga kufanya mabadiliko kadhaa ya kiufundi kwenye dirisha dogo ili kurudi kwa kasi Januari ambayo amekuwa akitabiri ushindani mkali.

Simba ina uhakika kwamba Chama akitua wakiongezeka na mastaa wengine uhai utarejea kwenye timu na kutetea ubingwa wake sambamba na kufanya vizuri hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. 

Mmoja wa viongozi wa waandamizi wa Simba amesema kwamba wanajua kuna mawasiliano ya Chama na Yanga, lakini wao wanajua walichofanya.

“Chama anarudi kujiunga na Simba, kwani kocha kampendekeza, anamhitaji na viongozi wameona kweli umuhimu wa kiungo huyo ambaye pia yeye mwenyewe anatamani kurejea kwenye klabu yake aliyoachana nao wakati wa dirisha kubwa la usajili na katika kuelekea hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika tunamhitaji sana,” alidokeza kiongozi huyo.

Kuhusu Duncan Nyoni na Pape Sakho  alisema wameshindwa kutoa changamoto mpya katika kikosi na kuonyesha tofauti yao dhidi ya wazawa huku thamani zao zikiwa juu.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUSEPA SIMBA...UNAAMBIWA MBRAZILI KAKOMAA NA MAMBO HAYA 5..MPAKA KIELEWEKE..

“Ili Chama arejeee Sakho na Duncan lazima waondoke, kwani Simba tayari imefikisha idadi ya nyota wa kigeni wanaopaswa kusajiliwa na timu kwa kuwa Sakho kwa kipindi kirefu amekuwa  majeruhi kitu ambacho kinamfanya mwalimu ashindwe kumtumia mara kwa mara na ishu nyingine ni gharama sana kuwa na watu ambao tunaweza kupata mtu mmoja anayeweza kupiga kazi nzuri.

“Duncan naye ni mchezaji wa kawaida sana ndio maana imekuwa ngumu kwake kupata namba katika kikosi cha kwanza kwani amekuwa akianzia benchi tangu ajiunge na klabu yetu,” alisisitiza kigogo huyo aliyekataa kutajwa jina huku akidai kuna mabadiliko makubwa yanakuja Simba.

Kwa upande wa wachezaji wazawa klabu hiyo imepanga kuachana na kiungo mkabaji Abdulswamad Kassim baada ya kushindwa kuonyesha makali yake tangu asajiliwe katika dirisha kubwa.

“Abdulswamad ni mchezaji mzuri japo imekuwa ngumu kwake kuonyesha makali yake kwa kuwa hajapewa nafasi ya kucheza ndio maana wameona wampe nafasi ya kwenda kwingine ili akionyesha kiwango anaweza kurudishwa.”

Kwa upande wa makipa, Jeremiah Kisubi ameomba uongozi umtoe kwa mkopo ili aweze kupata nafasi ya kurudisha  makali yake kwani ameshindwa kufurukuta mbele ya Aishi Manula ambaye anacheza huku kina Benno Kakolanya na Ally Salim wakisubiri.

“Kisubi ameuomba uongozi atolewe kwa mkopo kwani anaamini akitoka anaweza kurejesha ubora wake aliouonyesha msimu uliopita akiwa katika kikosi cha timu ya Prisons na sasa hapati kabisa namba katika kikosi cha timu hiyo,” alisema,

Katika hatua nyingine mchezaji wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema Chama ni mchezaji mzuri ambaye kwa muda alikuwa katika kikosi cha mabingwa hao watetezi wa ligi alifanya majukumu yake ipasavyo.

“Ukiangalia tangu Chama ameondoka katika kikosi cha Simba hakuna mchezaji aliyeweza kuziba nafasi yake kwa kutimiza majukumu kiwanjani. Kama atarejea ni moja ya usajili bora kwao,” alisema Pawasa.

Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza alisema Simba ilikuwa ikicheza kutokana na ubora wa Chama ila tangu alipoondoka katika timu wameshindwa kurudi katika makali waliyokuwa nayo msimu uliopita.

“Chama ni aina ya mchezaji mwenye uwezo haswa wakati Simba inapokuwa inashambulia anaweza kufanya vitu vya maana kufunga mabao muhimu, kutoa pasi ya bao au kuanzisha shambulizi kwa usahihi,” alisema Baraza aliyekuwa katika orodha ya tatu bora ya makocha kwa msimu uliopita.