Home Makala ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE KUHUSU ISHU YA AJIBU KUTUA AZAM…ADAI NI SAWA NA...

ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE KUHUSU ISHU YA AJIBU KUTUA AZAM…ADAI NI SAWA NA SIKIO LA KUFA…


MAISHA yalienda kasi ndani ya siku moja wiki iliyopita. Simba walitangaza kuvunja mkataba wa Ibrahim Ajibu Migomba. Waliafikiana na mchezaji mwenyewe. Siku hiyo hiyo kabla jua halijazama Ajibu akatangazwa kuwa mchezaji wa Azam.

Haikuwa bahati mbaya. Simba waliafikiana na Azam. Simba waliafikiana na Ajibu. Azam pia waliafikiana na Ajibu. Ina maana mchezaji ameondoka Simba bure kwenda Azam ingawa alibakiza mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Inaonekana Simba walimchoka Ajibu. Hawakujali anakokwenda. Kama wangejali sana, katika dunia ya kisasa, wangejaribu kupiga chenga ili waambulie chochote katika dili la Ajibu na anakokwenda. Ina maana wangejaribu kumuuza. Hata hivyo, inaonekana walikuwa wamemchoka sana.

Ilianzia lini? Sijui. Walimchukua baada ya kumaliza mkataba wake Yanga. Kule Yanga si ajabu ndipo Ajibu alicheza soka lake bora maishani. Sawa, msimu mmoja kabla hajaenda Yanga Ajibu alikuwa katika ubora wake Msimbazi. Machale yakamcheza kwamba asisaini mkataba mpya.

Ni kweli hatimaye akapata pesa yake ndefu ya kwanza katika soka. Akaenda Yanga. Akawa staa mkubwa Yanga. Alicheza soka bora lakini alijikuta akicheza soka bora katika timu ambayo haikuwa na nguvu sana. Mastaa walikuwa yeye, Herrietier Makambo na Fei Toto.

Ajibu alipewa hadi unahodha. Akajikuta pia akipewa jukumu jingine la kuchangisha michango kwa ajili ya timu ambayo ilikuwa hoi kiuchumi. Kumbuka kwamba GSM hawakuwepo. Hawajawahi kuwa katika Yanga yenye Ajibu.

Labda kama wangekuwepo basi Ajibu asingerudi Simba. Ni kweli mkataba wake ulipomalizika Ajibu alirudi zake Simba. Kumbuka kwamba hii ilikuwa ni mara ya pili ndani ya miezi 24 Ajibu alikuwa akiondoka katika klabu nyingine kubwa kama mchezaji huru. Kama ana mtu anamsimamia basi karata zake alikuwa amezichanga vema.

Kurudi Simba safari hii kulimaanisha kwamba Ajibu alikuwa na vita nzito kuliko alikotoka, Yanga. Ilimaanisha kwamba Ajibu alikuwa anakwenda katika kikosi kilichosheheni mastaa wakubwa tofauti na Simba aliyoiacha.

Ina maana kwamba alipaswa kubadilika kitabia. Kuna wanaodai kwamba Ajibu ni mvivu. Uvivu wake usingeweza kuonekana Yanga kwa sababu timu ilikuwa hohehahe ndani na nje ya uwanja. Kwanini umshutumu kwa uvivu mchezaji ambaye haumlipi vema?

Ndani ya Simba Ajibu hakuwa na maajabu na wala hakuonekana kuwa na kiu ya kusimama ahesabiwe. Wachezaji wazawa waliosimama na kuhesabiwa katika eneo la kiungo walikuwa Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Hassan Dilunga. Wote hawa hawamfikii Ajibu kwa kipaji.

Ukiachana na Chama, alipotua Rally ‘Soft Touch’ Bwalya nafasi ya Ajibu ndio ilitoweka kabisa. Sio nafasi ya uwanjani, nafasi ya walau kuingia akitokea katika benchi. Ikaendelea kuwa hivyo mpaka Chama alipoondoka huku mkataba wa Ajibu ukikata roho.

Pale Simba walionekana kuchanganyikiwa. Kulikuwa na mambo mawili. Jambo la kwanza ni uvumi kwamba Ajibu alikuwa anarejea Yanga. Kuna ambao walisema ‘bora aende’ lakini kuna wale ambao walikuwa wanasita wakiamini kwamba Ajibu alicheza soka bora akiwa Yanga na huenda kama angerudi basi na kismati chake kingerudi Jangwani.

SOMA NA HII  TUSIPOTEZE MUDA...HAWA QATAR NI KAMA TAIFA STARS TU...TOFAUTI YAO NA SISI NI UTAJIRI TU..

Jambo jingine lilikuwa lile la kuondoka kwa Chama. Kwamba labda Chama alikuwa kizingiti kikubwa kwa Ajibu na sasa ulikuwa wakati pekee wa Ajibu kutamba Msimbazi. Labda sasa Ajibu angeamka na kudai ufalme wake Simba.

Hili la pili liliwafanya watu wa Simba wampe mkataba mwingine Ajibu ingawa naambiwa ulikuwa mkataba wa kijanjakijanja. Klabu ilijiweka katika nafasi nzuri ndani ya mkataba. Haikutaka kujifunga sana kwake na ilimpa mkataba ambao angelipwa vizuri kama angekuwa anacheza.

Sikio la kufa halisikii dawa. Haikutokea hivyo. Ajibu aliendelea kuwa yule yule tu. Katika timu ambayo ilikuwa imeondokewa na Chama na Jose Luis Miquissone, Ajibu aliendelea kukosa nafasi. Wakati mwingine hata benchi alikuwa hakai.

Majuzi hapa alijaribu kufufua matumaini katika pambano dhidi ya Namungo. Aliingia uwanjani kipindi cha pili akaleta ujanja ujanja ndani ya dakika chache Simba wakapata bao dakika za majeruhi. Akaondoka uwanjani akiimbwa. Nilikuwa katika eneo la maegesho ya magari wakati mashabiki wakiwa wanatamani kumbeba.

Baadaye maisha yalirudi kama zamani. Nadhani kuna mambo mengine pia yalikuwa yanaendelea kambini kiasi kwamba Simba wakaamua kunyoosha mikono kwa Ajibu. Si ajabu walijua mapema kwamba anataka kwenda Azam lakini wala hawakujali. Na hawakujali pia kuambulia chochote katika dili yenyewe.

Hata kama alikuwa haendi Azam lakini hawakujali pia kama angeenda Yanga au angeenda nje ya nchi katika klabu ambayo ingeweza kuwalipa pesa. Hatimaye wamejivua na wameachana naye. Inaweza ikawa mara ya mwisho kabisa Ajibu kuvaa jezi ya Simba.

Na sasa ametua Azam. sio wachezaji wengi ambao wamewahi kucheza timu hizi tatu. Simba, Yanga na Azam. kwa haraka haraka nawakumbuka Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, Deo Munishi Dida. Wengine unaweza kuwakumbuka kwa muda wako.

Katika wote hawa, Ajibu anaingia Azam akituachia maswali mengi. Kwa mujibu wa Wikipedia ana umri wa miaka 25 tu lakini usishangae kwanini Azam wamempa mkataba wa mwaka mmoja. Nadhani sifa zake zinajulikana kila alikopita.

Ndani ya miezi 12 ijayo ni wakati ndio utakaoamua kama lilikuwa ni dili sahihi kwa Ajibu kwenda Azam. wakati utaamua kama lilikuwa dili lenye maslahi kwa Azam au Ajibu mwenyewe. Mpaka sasa ni dili lenye manufaa zaidi kwa Ajibu kwa sababu kama asingeweza kucheza nje na Yanga pia hawamuhitaji basi timu pekee ambayo angeweza kwenda ni Azam.

Lakini kwa Azam wenyewe ni wakati wa kusubiri na kuona kama Ajibu ataamka na kuongeza ubunifu katika eneo lao la kiungo cha ushambuliaji. Katika ubora wake Ajibu anaweza kuifanya kazi hiyo kwa umakini kabisa. Lakini ndio mpaka aamue.

Makala haya yaliandikwa na Edo Kumwembe kisha yakachapishwa awali kweye tovuti la Mwanaspoti