Home Makala KOSA LA MSIMU ULIOPITA….HIVI NDIVYO YANGA WANAVYOLIPIKA TENA MSIMU HUU BILA KUJIJUA…

KOSA LA MSIMU ULIOPITA….HIVI NDIVYO YANGA WANAVYOLIPIKA TENA MSIMU HUU BILA KUJIJUA…


NIANZE na kuwakumbusha namna msimu uliopita ulivyokuwa laini kwa Yanga na hasa mwanzoni lakini mwishoni mambo yakawa tofauti kabisa.

Mwanzoni, Yanga ilianza mechi kwa kuonekana ilikuwa timu bora na haina mpinzani, Kocha Zlatko Krmpotić aliifanya kazi yake vizuri sana na akafanikiwa kushinda mechi nne na sare moja. Akaondolewa na Cedric Kaze akapewa jukumu la kuendeleza hajazi.

Hadi mwisho wa mzunguko wa kwanza, gumzo lilikuwa ni unbeaten, Yanga haikuwa imepoteza hata mechi moja. Watu wakawa wanajadili namna gani itakwenda hadi mwisho wa msimu bila ya kupoteza hata mchezo mmoja.

Suala la ubingwa likawa na uhakika na ikaonekana hakuna tena wa kuizuia Yanga kutokana na mwendo iliokuwa inakwenda. Nawakumbusha, mwisho mambo yakawa tofauti kabisa, Simba wakawa mabingwa na Yanga wakalazimika kutumia nguvu nyingi angalau kushika nafasi ya tatu.

Hali hiyo imeanza tena msimu huu, ninaamini ni mashabiki au watu walewale ambao wamesahau haraka sana funzo walilolipata katika mpira, tena ni msimu uliopita tu!

Baada ya Yanga kuanza vizuri na hadi sasa ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja, suala la ubingwa likawa na uhakika hata kabla ya mechi 10. Imekwenda leo Yanga inaongoza, ikiwa kinara baada ya mechi 11, gumzo la ubingwa linaendelea na tukaelezwa timu hiyo inakwenda kuchukua makombe yote msimu huu.

Hii jeuri ilianza baada ya Yanga kuwatwanga Simba katika Ngao ya Jamii kwa bao 1-0 na kubeba ngao. Gumzo kubwa ni kwamba hakuna wa kuizuia Yanga msimu huu, hili linawezekana.

Nasema linawezekana kwa kuwa hakuna ubishi, Yanga wana timu nzuri, wachezaji wazuri lakini kiuhalisia bado hawajawa bora kwa asilimia mia maana bado timu yao inapaswa kujengwa na haswa katika suala la kuunganishwa.

Mambo ni mengi na wakati mwingine ni vigumu kuamini kwamba mpira unaweza kubadilika na mambo yakaenda mlama katika kipindi ambacho haukuwa unategemea hata kidogo. Tukubaliane, kuwa Yanga inachuana na Simba ambayo imekuwa bora zaidi kwa misimu minne mfululizo.

Lazima Yanga wajiridhishe na ubora ambao utakwenda kwa muda mrefu kidogo badala ya performance ya wiki tatu au mwezi kuwachanganya na kuamini kwamba wao hakuna wa kuwazuia.

SOMA NA HII  KISA SARE YA 0-0....MAAMUZI YA YANGA KUELEKEA MECHI IJAYO HAYA HAPA...

Angalia mfano mzuri, kosa la msimu uliopita linataka kufanana na hili lakini watu hawajaliona. Angalia mara baada ya Yanga kuvuliwa ubingwa wa Mapinduzi, gumzo limetawala kuhusiana na mambo kadha wa kadha, kuanzia kwa kocha na baadhi ya wachezaji.

Ukweli ni kwamba kuna kero, hasa hili suala la kocha kidogo kaondoka, baadhi ya wachezaji kila baada ya muda mfupi, kiguu na njia kurejea nyumbani na kadhalika. Wanahitajika kubaki katika kituo cha kazi na wapambane.

Vizuri kuwaeleza, vizuri kuhoji lakini ninachowakumbusha Yanga, suala la utulivu baada ya kosa fulani kutokea ni muhimu sana maana kama wataendelea kulaumu hivyo, watajichanganya wenyewe kama ilivyokuwa msimu uliopita baada ya zile sare mfululizo na baada ya hapo ndipo Yanga ilipoteza mwelekeo na Simba wakapita kama kimondo, wakawazidi na kwenda kuchukua ubingwa.

Yanga wakiona wamekosea jambo, mfano sasa wameshindwa kuchukua Mapinduzi Cup tena, lawama hazitaisha, wataendelea kulaumiana na kuzodoana na kama ulivyoona, baadhi kuwazomea wachezaji wao na kadhalika, hadi watafikia katika kiwango cha kujichanganya na mwisho hata kwenye ligi, wataanza kuboronga.

Kuna makosa yamefanyika, kikubwa sasa ni kuangalia walipoteleza na warekebishe kwa mujibu wa makosa na nguvu walekeze kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports badala ya kuwekeza katika kulaumiana, kukatishana tamaa na dhihaka zilizopitiliza, watapotea tena na mwisho wa msimu watajikuta hawana cha kujivunia zaidi ya Ngao ya Jamii!

Makala haya yaliandikwa kwanza kwenye wavuti la Globalpublishers