Home news MABOSI SIMBA WAAMUA LIWALO NA LIWE…WAWACHANA WACHEZAJI KWA KUHUJUMU …TRY AGAIN ‘ANG’AKA...

MABOSI SIMBA WAAMUA LIWALO NA LIWE…WAWACHANA WACHEZAJI KWA KUHUJUMU …TRY AGAIN ‘ANG’AKA KINOMA’…


KIKOSI cha Simba kimesharejea jijini Dar es Salaam kikitoka kupasuka bao 1-0 mbele ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, lakini unaambiwa mara baada ya mechi hiyo ya Kaitaba, mastaa wa timu hiyo wakiwekwa kitimoto.

Simba ilipoteza mchezo huo wa pili kwa msimu huu na kuifanya ipoteze jumla ya pointi 14 hadi sasa katika mechi zao 13 ilizocheza na kitendo hicho kiliwatibua mabosi wa klabu hiyo waliosafiri na timu hadi mjini Bukoba mkoani Kagera.

Mara baada ya dakika 90 za kiporo hicho kumalizika, huku Simba ikilala kwa bao la nyota wao wa zamani, Hamis Kiiza ‘Diego’, mabosi hao waliitisha kikao kizito na mastaa wa timu hiyo na kuweka kitimoto kwa muda wa saa moja na robo.

Kwa mujibu wa chanzo makini kutoka ndani ya Simba, inaelezwa wachezaji wa Simba walibanwa kwenye kikao hicho kizito mara baada ya mlo wa usiku katika hoteli waliyofikia.

Kikao hicho kinadaiwa kuanza saa 2:00 usiku na kumalizika zaidi ya saa 3:15 usiku, huku wachezaji wengi wakitoka wakiwa vichwa chini kutokana na kupewa makavu na mabosi hao walionekana kukerwa na matokeo ya timu hiyo kwa sasa.

Chanzo hicho kinasema kikao hicho kilihusisha wachezaji tu na mabosi waliowawashia moto walikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’, Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, Mjumbe wa Bodi, Mohammed Nassor Kigoma na Crescentius Magori.

“Baadhi ya wachezaji (majina tunayo) walielezwa bayana kwamba wanachomesha na kushindwa kujituma, huku wachache wa kigeni wakicheza kama hawana wanachokitafuta uwanjani,” chanzo hicho kilisema.

Naye mmoja wa viongozi (jina tunalo) alithibitisha ni kweli waliwachana baadhi ya wachezaji kutojituma na kujitolea tofauti na viwango vyao vilivyo, wengine kutokuwa na uchungu na timu.

“Kuna ambao hawana uchungu na timu kabisa wanacheza kama hakuna kitu wanataka, kuna wanaofanya makosa yale yale na kuigharimu timu, tumewambia wote na kuwaeleza hii si timu ya namna hiyo,” alisema kigogo huyo na kuongeza;

“Baada ya kuwaambia ukweli huo tumewaeleza Simba si timu ya kufungwa namna hii na kushindwa kupata matokeo mazuri katika mechi tatu mfululizo huku tukiwa katika kiwango cha chini kabisa.”

SOMA NA HII  MSHAMBULIAJI NAMBA MOJA KMC AOMBA KURUDI SIMBA

Kigogo huyo alisema kufungwa kwa Simba sio ishu, kwani hata msimu uliopita walipoteza mechi tatu, lakini muda mwingi wapinzani walipata wakati mgumu kwa kuwashambulia na kutafuta bao tofauti na ilivyo msimu huu.

“Kuna wachezaji wameshuka viwango kutokana na mambo yao ya nje ya uwanja tumewaeleza hilo na wanatakiwa kuachana na mambo hayo mara moja kwani tunaweza kuchukua hatua kali dhidi yao,” alisisitiza kigogo huyo.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo alisema kuna baadhi ya wachezaji walikutana na joto ya jiwe pale pale kiwanjani kabla ya kufika kambini kutokana kile walichotoka kukionyesha uwanjani.

“Kuna mengine makali zaidi tumewaeleza hawa wachezaji wetu na hatukuishia hapo tumewaambia tutachukua hatua kali dhidi yao kama wataendelea hivi ikiwamo kukatwa mishahara pamoja na kuzuia posho zao,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;

“Tumeamua kuwa wakali na kuongea maneno makali kama hayo ili nao wachezaji wetu waone jinsi gani kuna watu wengi wanaumia huku nyuma yao kutokana na kile ambacho kinaendelea uwanjani.”

MSIKIE TRY AGAIN

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema; “Si jambo la kawaida kwa Simba kupata matokeo kama haya mfululuzo, inaumiza lakini ni wakati wa kutulia na kuangalia nini cha kufanya.”

Kuhusu kocha Pablo Franco kunyooshewa vidole na baadhi ya mashabiki, Try again alisema kocha hana shida.

“Kocha amechukua ubingwa wa Mapinduzi, amefanya vizuri kwenye mechi nyingi tangu alipojiunga na Simba, sioni tatizo la kocha.

“Japo nasisitiza si jambo la kawaida kwa Simba kupoteza mechi mfululizo, inaumiza na yanamuumiza kila mwana Simba hivyo tunaangalia nini cha kufanya.

“Kama klabu tutafanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi, mashabiki na wapenzi wa Simba watulie Simba ina viongozi makini na tutapata majibu sahihi kwenye hili,” alisema.

Kuhusu kuuweka rehani ubingwa, Try Again alisema upepo unaotokea kwenye timu yao sasa hautawarudisha nyuma.

“Ndio kwanza tuko kwenye mechi za mzunguko wa kwanza, bado tuna mechi nyingi msimu huu ambazo tunaamini tukijipanga vizuri tutatetea ubingwa wetu msimu huu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here