Home news KWA TAARIFA YAKO…SIMBA WANAWEZA KUWEKA REKODI HII BAB KUBWA AFRIKA LEO WASIPOFUNGWA…

KWA TAARIFA YAKO…SIMBA WANAWEZA KUWEKA REKODI HII BAB KUBWA AFRIKA LEO WASIPOFUNGWA…


Ushindi au sare dhidi ya RS Berkane huko Morocco leo utaifanya Simba kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutopoteza mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi ya klabu Afrika kwa misimu miwili mfululizo.

Msimu uliopita, Simba haikupoteza mechi zote tatu za mwanzo za makundi ilipotinga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita ugenini, ikaifunga Al Ahly bao 1-0 kisha ikatoka suluhu katika mechi ya tatu dhidi ya Al Merrikh. Na safari hii japo inashiriki hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrikahaijapoteza mechi mbili za mwanzo za kundi D ilipoanza kushinda kwa mabao 3-1 nyumbani kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na US Gendarmerie Nationale.

Hata hivyo ili kuweka rekodi hiyo Simba itapaswa kufanya kazi ya ziada katika mchezo huo kutokana na ubora na uzoefu wa wapinzani wao ambao ni timu ya tatu tishio nchini Morocco kwa sasa.

Berkane sio tu ina historia katika mashindano hayo ikiwa imetwaa ubingwa wake mara moja kwenye msimu wa 2019/2020 lskini pia imefanya uwekezaji mkubwa na kusajili nyota kutoka maeneo mbalimbali Afrika na benchi la ufundi linaloongozwa na mmoja kati ya makocha bora wazawa Afrika, Florent Ibenge.

Simba wanapaswa kujipanga zaidi kutowaruhusu Berkane kuingia mara kwa mara kwenye eneo lao la hatari kwani ni timu ambayo imekuwa ikishambulia hasa kwa kupiga mashuti zaidi pindi inapokuwa katika boksi la timu pinzani ingawa wakati mwingine imekuwa ikipiga mashuti ya mbali.

Ni timu inayotegemea zaidi kujenga mashambulizi yake kwa kutumia mipira mirefu inayopigwa kutokea nyuma kwenda kwa washambuliaji wake wenye uwezo mkubwa wa kuwazidi ujanja mabeki na kufunga pale wanapolitazama lango.

Katika mechi mbili ilizocheza dhidi ya Gendarmerie na Asec Mimosas, RS Berkane imepiga mipira mirefu 74 ikiwa ni wastani wa mipira 37 kwa mchezo huku ikipiga krosi 13 ikiwa ni wastani wa krosi 6.5 kwa mechi.

SOMA NA HII  BAADA YA INONGA KUMNYANYASA MAYELE JUZI...MASHABIKI SIMBA WAFANYA YAO HUKO...

Pasi fupifupi za chini zimeonekana kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Berkane na kama Simba watajipanga wanaweza kuzitumia kuwamaliza.

Berkane imekuwa na takwimu bora nyumbani na kuthibitisha hilo katika mechi 10 zilizopita za mashindano hayo imeshinda nane na sare mbili.

Katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika ambazo Simba imecheza ugenini, imeshinda tatu, kutoka sare tatu na kufungwa nne.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema hesabu zao ni kupata ushindi au sare ugenini.

“Tunaongoza kundi na bila shaka hii ni mechi ambayo tunahitaji kupata ushindi au hata pointi moja ili tujiweke katika mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali,” alisema Pablo.